Ndugu Wananchi;
Kesho ni siku muhimu sana na ya kihistoria kwetu Watanzania. Tutaadhimisha miaka 61 tangu waasisi wa Taifa letu, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, walipofanya kitendo cha kishujaa cha kuunganisha nchi zetu mbili na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Sote hatuna budi kuendelea kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa rehema zake ambazo zimetuwezesha kuvuka salama zaidi ya miongo sita ya Muungano.
Watanzania wenzangu, tunayo kila sababu ya kujipongeza kwa kuweza kuudumisha Muungano wetu ambao ni wa kipekee barani Afrika. Kama alivyowahi kusema Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere: "Tanzania ni lulu ya pekee kabisa katika historia ya Afrika huru." Heshima na hadhi hii ya kuwa na Muungano thabiti, imara usiyoyumba wala kutetereka si juhudi za Serikali pekee, bali ni juhudi za Watanzania wote ambao kwa pamoja tumeamua kuendeleza na kukuza udugu, mshikamano na umoja wetu kama Taifa. Kwa ujumla, tumeamua kulinda Wakfu huu wa Muungano tulioachiwa na Wazee wetu.
Nimetumia neno WAKFU kwa kuwa Tunu hii ya Muungano wa Tanzania uliasisiwa, umelelewa, na unatunzwa vyema ili uwe madhubuti na wa kudumu. Muungano huu si mali ya mtu, ila unamilikiwa na Watanzania wote. Tumuombe M/Mungu aendelee kuwapa mapumziko mema ya milele Waasisi wa Muungano huu, pamoja na viongozi wote waliotangulia mbele ya haki. Aidha, tunawashukuru sana Viongozi wote ambao katika nyakati za utumishi wao kwa Taifa letu, waliulinda Muungano wetu na kuukabidhi kwetu ukiwa Imara.
Ndugu Wananchi,
Hakika sote tu mashahidi wa mafanikio na hatua kubwa za kimaendeleo ambazo nchi yetu imepiga tangu mwaka 1964. Ni imani yangu ya dhati kwamba tukiendelea na umoja na mshikamano tulionao, Muungano wetu utaendelea kustawi kwa manufaa ya Watanzania wote.
Wakati mliponikabidhi dhamana ya kuliongoza Taifa hili niliahidi kwamba Serikali ninayoiongoza itaendeleza mema yaliyopita, kuimarisha yaliyopo na kuleta mema mapya. Muungano wetu ni moja kati ya mema tuliyoyakuta ambapo Serikali imesimama imara katika kuulinda, kuuimarisha na kuudumisha. Hivyo basi, ni jambo jema kufanya maadhimisho ya sherehe za Muungano kila ifikapo tarehe 26/4 ya kila mwaka. Kwa mwaka huu, maadhimisho yatafanyika katika mikoa yote ya Tanzania na viongozi mbalimbali wa Serikali wataungana na wananchi katika shughuli za uzinduzi wa miradi ya maendeleo. Pamoja na hayo, yamefanyika makongamano, michezo mbalimbali na shughuli za kitamaduni nchi nzima.
Kwa kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu nchini kwetu, Serikali imeamua kuyapa maadhimisho haya kaulimbiu isemayo "Miaka 61 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania: Muungano Wetu ni Dhamana, Heshima na Tunu ya Taifa: Shiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025".
Katika ngazi ya kitaifa, kesho tarehe 26, kwa niaba ya Serikali na Wananchi kwa ujumla, nitatunuku nishani za Muungano kwa Watanzania wenzetu kama ishara ya kutambua utumishi na mchango wao katika ujenzi wa Taifa letu na katika kudumisha Muungano wetu.

Ndugu Wananchi;
Ndani ya kipindi cha miaka 61 ya Muungano wetu, Serikali zetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zimeendelea kushirikiana kwa karibu, kubadilishana uzoefu na kusaidiana kwa dhati. Ushirikiano huu umechochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kidiplomasia. Tumeweza kuimarisha amani, na mshikamano wa Kitaifa.
Kuwepo kwa mafanikio hayo haina maana kwamba hatuna changamoto. La muhimu ni kwamba tumejiwekea mfumo mzuri wa kutatua changamoto zinapojitokeza. Hapa, nataka niipongeze Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kusimamia vyema masuala ya Muungano, na nina washukuru wote waliofanya makongamano ya kueleza faida, mafanikio na changamoto zilizojitokeza katika kipindi chote na jinsi zilivyofanyiwa kazi.
Ndugu Wananchi,
Ndani ya miongo 6 tumeweza kulinda Uhuru wetu na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar dhidi ya matishio mbalimbali. Aidha, Tanzania imeendelea kushuhudia mabadiliko ya uongozi kidemokrasia, ambapo kila baada ya miaka mitano hufanyika uchaguzi wa viongozi wa kitaifa na wa serikali za mitaa.
Zaidi ya hayo, Muungano wetu unaendelea kuzingatia misingi ya utawala bora katika nyanja mbalimbali ikiwemo utawala wa sheria, haki za binadamu, uwazi, uwajibikaji na maridhiano. Demokrasia yetu imeendelea kukua na kuimarika hususan kupitia Falsafa yetu ya R-Nne (4Rs) ambayo itaendelea kuwa nyenzo muhimu ya kukuza ushiriki na ushirikishwaji wa wananchi kwenye masuala muhimu kwa mustakabali wa nchi yetu. Hata hivyo, nataka kusisitiza kama ambavyo nimekuwa nikisema katika majukwaa mbalimbali kwamba kutekelezwa kwa R-Nne kunaenda sambamba na kuzingatiwa kwa Katiba na sheria za nchi. Kamwe falsafa hii haiwezi kuwa kisingizio cha kuvunja sheria au kujenga mazingira yanayohatarisha amani, usalama na utulivu wa nchi yetu.
Dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inasimamiwa na mihimili mitatu ambayo ni; Serikali, Bunge na Mahakama. Kwa pamoja kama nchi, tumeamua pia uendeshaji wa shughuli za nchi yetu ushirikishe taasisi nyingine za ndani na nje ya nchi, taasisi za Serikali na zisizo za Serikali, taasisi za kidini na za kiraia. Shughuli zote zinazofanywa na taasisi hizi, zinaongozwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katiba ya Zanzibar, Sheria na kanuni zinazotungwa, na miongozo na makubaliano mbalimbali ya Kitaifa na Kimataifa.
Nyenzo hizi nilizozitaja zimeeleza masharti na mipaka ya kazi kwa taasisi mbalimbali zinazofanya shughuli zake hapa nchini. Ili kuiwezesha Serikali kuendelea kulinda haki za kiraia ikiwemo haki ya kujieleza na kutoa maoni, ni vyema sote tusivuke nje ya mipaka yetu. Tusisahau kwamba mfumo wa Dola yetu ni kuongozana, kusimamiana na kuwajibishana.
Ndugu wananchi;
Mwaka wa 61 wa Muungano wetu umeangukia kwenye mwaka tunaokabiliwa na jambo kubwa la kidemokrasia nchini. Tutafanya uchaguzi wa kuwachagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, pamoja na Madiwani.
Ni matumaini yangu kuwa, tutaendelea kudumisha sifa ya nchi yetu kuwa ni kitovu cha amani na nchi ya kidemokrasia iliyojengeka juu ya misingi ya uhuru na haki. Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa mahitaji yote ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi yanapatikana kwa ukamilifu na kwa wakati. Aidha, tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika kwenye mazingira ya utulivu na amani katika kipindi chote cha matayarisho hadi wakati wa uchaguzi, ili kuwa na uchaguzi huru na wa haki.
Wito wangu kwenu Wananchi: mjitokeze kwa wingi kushiriki katika mchakato mzima wa uchaguzi, kuanzia kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura, kujitokeza kugombea na hadi kupiga kura.
Niwatake viongozi, wanachama na wafuasi wa vyama vya siasa, tuzingatie taratibu na sheria za nchi. Uchaguzi huu uwe ni fursa ya kuimarisha zaidi umoja na demokrasia yetu ili tupate viongozi bora na walio imara. Kamwe tusiruhusu uchaguzi uwe chanzo cha migogoro, chuki, mivutano na uvunjifu wa amani ndani ya vyama, baina ya vyama au nchini kwa ujumla. Niseme kuwa, hakuna alie juu ya sheria na wote tunatakiwa kuendesha shughuli zetu za kisiasa tukizingatia kuwa Amani na Usalama wa nchi ndio kipaumbele cha kwanza.
Ndugu wananchi;
ninapohitimisha hotuba yangu, nataka niwakumbushe kwamba wajibu wa kulinda, kutetea na kudumisha Muungano ni wa kila Mtanzania. Waasisi wetu, Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume waliakisi Muungano kwa kauli na matendo yao. Nasi hatuna budi kudumisha Tunu hii ya Taifa letu kwa kuimarisha misingi ya udugu, uzalendo, amani, mshikamano na umoja wa Kitaifa. Hizo ndizo nguzo zinazoleta umadhubuti na uimara wa Muungano huu. Tuilinde misingi hii ili tuweze kufikia matamanio ya waasisi wa Taifa letu ya kuwa na Taifa moja lenye nguvu zaidi kiuchumi, kisiasa, kijamii na Kidiplomasia.
Kesho, tunapofikia kilele cha maadhimisho ya miaka 61 ya Muungano wetu, katika Mikoa na Wilaya zetu Tanzania nzima, nitumie fursa hii kukutakieni Watanzania wote Maadhimisho mema ya Miaka 61 ya Muungano.
Mungu ibariki Tanzania
Mungu ubariki Muungano Wetu
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza