Sehemu ya hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa wakati wa uzinduzi wa reli ya kisasa, Aprili 13, 2017 Pugu jijini Dar es Salaam.
Inakadiliwa kuwa wakati wa ujenzi wa reli hii takriban watu 600,000 watapata ajira, wakiwemo 30,000 ambao watapata ajira za moja kwa moja. Reli hii itakapokamilika inatarajiwa kutoa ajira takribani milioni moja kupitia viwanda, na kukua kwa sekta nyingine za kiuchumi. Zipo nyingine nyingi, hivyo basi niwasihi Watanzania wenzangu kujipanga ili kuweza kunufaika na mradi huu.
Ndugu zangu wageni waalikwa na ndugu viongozi, ujenzi wa reli hii yenye urefu wa kilometa 1,219 umegawanywa kwa vipande vitano. Kipande cha kwanza ni hiki ambacho leo tunaweka jiwe la msingi ambacho kinatoka hapa Dar es Salaam hadi Morogoro na kitakuwa na urefu wa kilometa 300.
Eidha awamu hii itahusisha ujenzi wa stesheni sita ambazo kubwa pia zitajengwa pale Ruvu, ambazo zitahusisha na kujenga ‘dry port’ pale Ruvu na kupunguza pia hatua mbalimbali za msongamano katika Jiji la Dar es Salaam.
Reli hii itakuwa ya kisasa kabisa na yenye uwezo mkubwa. Mheshimiwa Waziri na watendaji wa ujenzi wa RAHACO wameeleza kuwa injini za treni hii zitatumia umeme pamoja na dizeli.
Mwendo kasi wake utakuwa kilometa 160 kwa saa, kwa treni za abiria. Lakini excel road yake yake itakuwa na uwezo wa kubeba tani 35 tofauti na ya sasa ambayo hazifiki hivyo.
Lakini pia tumeambiwa watahakikisha watamaliza ujenzi huu ndani ya miezi 30 na mwenye kampuni yake ya kandarasi amezungumza kwamba atahakikisha anamaliza kwa wakati.
Gharama za ujenzi za kipande hiki cha kilometa 300 kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ni dola za Kimarekani milioni 1.22 ambayo ni sawa na trillion 2.8. Na katika bajeti ya mwaka huu ya mwaka uliopita ambayo tunamalizia, na ninashukuru waheshimiwa wabunge wako hapa walitupitishia bajeti ya trilioni moja kwa ajili ya kuanza kugharamia.
Na mnaweza mkaona kwa hesabu za kawaida, kama itajengwa kwa miezi 30 miezi 12 ya kwanza trilioni 1, miezi mingine 12 trilioni 1, miezi mingine iliyobaki zile bilioni 800 zilizobaki. Na bahati nzuri fedha hizo zipo.
Lakini ieleweke tu ndugu zangu, saa nyingine fedha hizi huwa haziwezi kutolewa kabla kandarasi hajapatikana. Mnatambua kwa mfano katika mradi huu fedha zimetengwa katika bajeti ya mwaka huu ambazo ziko miongoni mwa asilimia 40 ya fedha za development.
Kandarasi asingeweza kulipwa kabla hajaanza mobilization na hiyo ndiyo sheria, tungeweza tukamlipa halafu akaondoka na advance payment ya asilimia 15 imelipwa wiki iliyopita ya bilioni 300. Sasa bilioni 300 amelipwa wiki iliyopita, inawezekana hili sasa linaweza likawa jibu zuri kwamba ni kwanini saa nyingine fedha za development huwa hazilipwi mapema kwa sababu ni lazima umlipe kandarasi anapokuwa kwenye saiti pamoja na kwamba fedha hizi zimetengwa kuanzia mwezi Julai, mwaka jana.
Ndugu zangu, baada ya kumuona mkandarasi na kuanza ujenzi wa kipande hiki cha Dar es Salaam sasa Serikali inaelekeza nguvu zake katika kipande kilichobaki cha Morogoro hadi Makutopora chenye jumla ya kilometa 336. Kwa bahati nzuri hivi karibuni tulitembelewa na mgeni- Rais wa Uturuki. Alipoona kwamba Tanzania tumetayarisha fedha zetu wenyewe, za nguvu zetu wenyewe, za walipa kodi Watanzania, trilioni 2.8; na kutangaza tenda zilizokuwa za uwazi, makandarasi zaidi ya 40 walijitokeza. Kwa bahati nzuri kwake ikashinda kampuni ya Uturuki. Rais wa Uturuki amesema kile kipande cha kutoka Morogoro mpaka Dodoma, ameshatuma makampuni, mabenki matano tujadiliane nayo na atatoa mkopo nafuu ili pale napo tutengeneze.
Hii inadhihirisha msemo wa kabila langu kwamba unapopata msiba lia sana ili kusudi jirani naye alie. Kwa hiyo tumelia sana majirani Uturuki wamekuja sasa kutusaidia kilichobaki. Lakini pia Rais wa Benki ya Dunia alipotembelea hapa Tanzania na jana wametoa ripoti yao kwa jinsi tunavyofanya kazi vizuri. Na bahati nzuri mwakilishi wa Benki ya Dunia yuko hapa Mama Bella- Mama Bella [Bella Bird] hebu simama wakuone hapo.
Nao sasa wameshajitolea namna ya kutusaidia katika sehemu nyingine. Lakini pia wametoa fedha kama bilioni 300 za kuanza kuikarabati ile reli nyingine iliyokuwepo ya zamani ili nayo iendelee kutumika vizuri.
Kwa hiyo ndugu zangu Watanzania ninachotaka kuwaeleza tumeanza vizuri, tunaenda vizuri, ni lazima tutembee kifua mbele kwa sababu haijawahi kutokea na wale wataalamu wanaojua kusoma kwenye mitandao wakasome kwenye mitandao ni nchi gani nyingine imejenga reli ya namna hii kwa kutumia fedha zake. Watakuta ni Tanzania.
Kwa hiyo tumeanza vizuri, Watanzania tutembee kifua mbele. Lakini ninafahamu katika usafiri wowote kwa mfano kwa ndugu zangu madereva wa malori wanafahamu.
Unapokuwa dereva wa lori, unapopakia abiria kwenye lori huhitaji kuwauliza watasimama waangalie sehemu gani wakati lori linaondoka. Wapo watakaotazama nyuma, wako watakaotazama ubavuni, wako watakaotazama ubavu mwingine, wako watakaotazama kule roli linakoelekea. Lakini wapo wengine kama utakuwa umepakia Wasukuma wanaweza kuwa wengine wanaimba mle kwenye lori huku linaondoka.
Dereva mzuri hutakiwi kusikiliza nyimbo, hutakiwi kuangalia watu walikotazama, angalia lori unakolipeleka ili lifike salama. Kwa hiyo nataka kuwahakikishia ndugu zangu na Watanzania, mimi ninajiamini ni dereva mzuri, na kwenye lori langu nimepakia watu wa aina hiyo. Wapo wanaoimba, wapo anaopiga stori humo humo kwenye lori, wako wanaotazama nyuma wakati lori linaenda mbele, wako walioangalia mbele, wako walioangalia ubavuni, wako walioangalia ubavu mwingine. Lakini nataka kuwahakikishia lori linakata kule tunakoenda na hili ni lori la maendeleo.
Hili ninawahakikishia ndugu zangu tatafika. Tulichelewa. Na katika kazi hizi ambazo tunazifanya, mara nyingi mtakaowaona wanaopiga kelele ni upande wa walioangalia nyuma, lakini lori litaenda tunakotaka, ni lori la maendeleo kwa ajili ya Watanzania na hasa Watanzania masikini.
Jana katika ripoti iliyokuwa inatolewa na Benki ya Dunia na gavana ameeleza, katika nchi zote za Afrika, nchi nyingi uchumi wake umekua kwa asilimia 1. Lakini kwa bahati nzuri katika nchi hizo, ukichukua nchi tano ambazo uchumi wake unaenda safi, Tanzania ipo ambayo uchumi wake unakua kwa asilimia 7.
Na ushahidi wa kukua kwa uchumi ndiyo hii miundombinu inayofanywa. Kwa wana-Dar es Salaam mnafahamu ni mwezi huu tu mwanzoni uliopita tulizindua barabara za juu pale Ubungo ya ghorofa tatu gharama zake ni mabilioni ya fedha.
Ukienda Tazara pale tunajenga flyover nyingine, zaidi ya thamani yake ni bilioni 100. Kwa Dar es Salaam hapa tunajenga ring roads zenye thamani ya zaidi ya bilioni 38. Tutaanza ujenzi wa flyover nyingine inayounganisha Aga Khan na Coco Beach yenye thamani ya mabilioni ya fedha na itakuwa inapita kwenye Bahari ya Hindi.
Lakini hivi karibuni tumepata mkopo wa zaidi ya bilioni 425 wa kuanza kujenga barabara za mwendo kasi katika awamu ya tatu na ya nne. Na nyingine itaanzia Gongolamboto kuelekea mjini katika awamu wa tatu yenye jumla ya kilometa 23.8. Mungu atupe nini ndugu zangu?
Uchumi unaenda. Siku za nyuma ilikuwa ni historia kwa Tanzania kuwa hata na shirika lake la ndege. Tumebana hela za mafisadi, tumebana fedha za wapiga dili, tumenunua ndege sita mpya, na hii ita-promote utalii, ita-promote biashara, lakini italipeleka lori letu lifike mahali tunakoenda.
Miradi ya miundombinu inaendelea, viwanja vya ndege vinapanuliwa, haya ndiyo tuliyoyaahidi. Ninafahamu mimi niliahidi kwa niaba ya Watanzania na wabunge hao hao ambao wengi ni wa Chama Cha Mapinduzi waliahidi kwa niaba ya majimbo yao.
Tunajua tunakoenda. Pasitokee mtu wa kubadilisha ajenda, wabadilishe mawazo yetu, tuanze kuzungumzia ajenda ambazo haziko kwenye ilani ya uchaguzi.
Kwa hiyo ndugu zangu napenda kuwashukuru sana makandarasi, pamoja na ma-consultant makampuni kutoka Korea. Ninataka mradi huu ukamilike kwa wakati.
Kwani nchi kama ya Uturuki huwezi ukajenga tu kilometa 300 kwa miezi 30 maana yake kila mwezi kilometa moja tu? It can’t be possible!
Nataka contractor pamoja na kwamba mkataba ni miezi mitatu, na kwa sababu hela hizi ni za Watanzania asilimia 100, na yeye ni kibarua wetu, ajitahidi amalize mradi huu kabla ya miezi 30. Watanzania hawa wanataka hii treni waipande na inawezekana siku ya kuifungua twende free mpaka Dodoma na ikiwezekana mpaka mbali huko.
Watu waende kwenye sherehe ya Makao Makuu Dodoma wakipita kwenye treni ya umeme ya kwanza kutengenezwa katika Afrika Mashariki na ya Kati.