Mheshimiwa Samia Suluhu, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiwa wa Baraza la Mapinduzi,
Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi na Mama Mwinyi, Rais mstaafu wa Awamu ya Pili.
Mheshimiwa Othmani Chande, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mheshimiwa Mama Salma Kikwete, mke wa Rais mstaafu wa Awamu ya Nne.
Mheshimiwa Karume, Rais mstaafu wa Zanzibar,
Waheshimiwa Mawaziri Wakuu wastaafu waliopo hapa, Mheshimiwa mama yetu Karume,
Mheshimiwa Spika wa Baraza la Wawakilishi,
Wakuu wa vyombo vya usalama wote mliopo hapa wakiongozwa wa CDF.
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Waheshimiwa mabolozi,
Waheshimiwa mawaziri,
Waheshimiwa viongozi wa dini,
Waheshimiwa wa vyama mbalimbali vya siasa…nimemuona hapa Mheshimiwa Lipumba na viongozi wengine walioko.
Waheshimiwa wabunge,
Waheshimiwa waalikwa wote, ndugu wananchi wenzangu, mabibi na mabwana Asalaam Alleikum, Bwana Yesu Asifiwe, Tumsifu Yesu Kristo.
Leo ni siku muhimu sana. Nafahamu kwa siku ya leo sikutakiwa kutoa hotuba, lakini nimeona angalau niwasalimu kidogo.
Leo ni siku muhimu kwa sababu tunaadhimisha miaka 55 ya kupata uhuru wetu ambao tuliupata tarehe 9 Desemba 1961. Wakati tunapata uhuru wapo waliouona kabisa uhuru tukisherehekea mwaka 1961.
Natambua Mzee wangu Mwinyi wakati huo alikuwa na miaka 36 hivi au 37, mimi nilikuwa na miaka miwili, kwa hiyo sikujua hata siku ya kupata uhuru. Lakini inawezekana wengine hawakuuona kabisa, kwa sababu wamezaliwa baada ya uhuru. Kwa hiyo, tuliopo hapa wengi tumezaliwa baada ya uhuru. Ukiondoa wachache wakiongozwa na Mzee wetu Mwinyi na mama Karume na wengine wengine labda walikuwa na miaka mitatu mingine mitano na kadhalika.
Kwa hiyo, leo ni siku muhimu sana kwetu sisi sote. Hivyo basi Watanzania wote hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na kuiona siku ya leo na kuendelea kuilinda nchi yetu.
Sambamba na kumshukuru Mwenyezi Mungu, tuwakumbuke pia wazee wetu wote ambao walijitoa muhanga kupigania uhuru wa nchi yetu hususani wazee 17 waanzilishi wa chama cha TANU wakiongozwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Kama isingekuwa ujasiri na ustamilivu wao, huenda hadi leo tungekuwa bado tunatawaliwa. Kwa hiyo, tunashukuru sana kwa sababu walijitoa kwa hiari yao kuweza kuutafuta uhuru wa Tanzania ili tuweze kuwa huru.
Hii ni mara yangu ya pili ya maadhimisho haya kufanyika tangu nimechaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Tanzania. Najua mtajiuliza kwamba ni mara ya pili kivipi wakati leo ndiyo nimekuja hapa kwa mara ya kwanza!
Mara ya kwanza ilikuwa mwaka jana (2015). Najua hatukufanya sherehe kama hizi, lakini tuliadhimisha kwa kufanya usafi nchi nzima. Ile nayo ilikuwa sherehe.
Napenda niwafahamishe ndugu zangu, kwamba sherehe za mwaka jana ilibidi tuziadhimishe kama tulivyofanya kwa sababu mbili; Sababu ya kwanza sherehe zenyewe zilikuwa zifanyike mwezi mmoja baada ya mimi kuapishwa. Kwa hiyo hata baraza langu na watendaji wangu wengine nilikuwa bado sijawateua.
Lakini sababu ya pili nilipoambiwa gharama za sherehe hizo mwaka jana zilikuwa bilioni 4. Nikawa ninajiuliza bilioni 4 kuna mambo yapi yatakayofanyika? Itakuwa ni kuwalipa wageni, itakuwa ni chakula, patakuwa na posho na kadhalika.
Nilipouliza hizo posho na chakula watakula chakula Watanzania wote? Wakasema ni wale wachache tu watakaokuwa wamealikwa. Ndiyo maana nikaamua hizo bilioni 4 ziende zikapanue barabara la Ali Hassan Mwinyi ambalo linapitiwa na Watanzania wote.
Inawezekana niliwakosea Watanzania ninaomba mnisamehe. Lakini kama uamuzi ule ulikuwa wa msingi kwa kupunguza msongamano. Kwa hiyo hizo fedha bilioni 4 tulizielekeza kwenda kupunguza msongamano wa barabara la Ali Hassan Mwinyi ambalo kwa sasa limepunguza msongamano na Watanzania wengi wanalitumia na watalitumi miaka katika maisha yao yote.
Sherehe za miaka 55 nimeamua zifanyike kwa sababu kwanza gharama zake ni ndogo sana. Kwanza hakuna hata chakula baada ya sherehe hii, hakuna dhifa ya Taifa. Kwa hiyo tukishamaliza hapa tumemalizana.
Lakini pili niliamua sherehe hii niifanye hapa Dar es Salaam kwa sababu ninaamini kwamba hii itakuwa sherehe ya mwisho kufanyika hapa Dar es Salaam.
Ni matumaini yangu sherehe ya mwaka kesho, itafanyika Makao Makuu ya nchi ambayo ni Dodoma. Kwa hiyo kwa wapenda gwaride, itabidi sasa wasafiri kwenda Dodoma wakashuhudie shamrashamza hizi nzuri ambazo tumezishuhudia leo zilizooneswa na majeshi yetu.
Ndugu zangu, wananchi mliopo hapa na Watanzania, ningependa tu niseme kwamba sherehe za uhuru ni tukio muhimu sana katika Taifa. Hivyo tutaendelea kuipa umuhimu siku hii na kuiadhimisha.
Lakini kwa wakazi wa Dar es Salaam kama nilivyosema, inawezekana hii ikawa ndiyo sherehe yao ya mwisho.
Katika kipindi cha miaka 55 ya uhuru wa nchi yetu, tumepata mafanikio makubwa sana na mengi. Nafahamu wapo wenye kubeza mafanikio tuliyoyapata.
Lakini ukweli ni kwamba tumepata mafanikio makubwa, Tanzania ya leo ni tofauti na Tanzania ya mwaka 1961. Kwanza tumelinda uhuru wa nchi yetu, tumelinda mipaka yetu, mipaka yetu yote iko salama.
Tunafanya mambo yetu sisi wenyewe bila kuingiliwa. Wapo waliojaribu kutishia uhuru wetu lakini wameshindwa.
Tupo imara, tumedumisha amani. Umoja na mshikamano wa nchi yetu tangu tumepata uhuru nchi yetu imebaki na amani na wananchi wamebaki kuwa wamoja. Hatubaguani kwa misingi ya rangi au dini au kabila, au itikadi ya vyama.
Tumejenga na kudumisha Muungano wetu. Ni vyema Watanzania wote tukajipongeza kwa hatua hizi tulizozifikia.
Ndugu zangu Watanzania, katika kipindi cha miaka 55 tumejenga miundombinu mbalimbali ya kiuchumi ikiwamo barabara, madaraja, vivuko, meli, reli, viwanja vya ndege, miradi ya umeme, maji na kadhalika.
Huduma za jamii kama vile afya na elimu zimeboreshwa, na kusogezwa karibu kwa wananchi. Baadhi yetu tunakumbuka jinsi ambavyo zamani ilitulazimu kutembea umbali mrefu kufuata huduma za shule au hospitali. Tumeweza Watanzania. Na tumeweza kweli kweli. Nchi yetu pia imeng’aa kimataifa. Kutokana na mchango wake katika harakati za ukombozi wa bara la Afrika. Kutafuta amani na kupinga uonevu duniani.
Napenda kutumia nafasi hii kuwapongeza sana viongozi mbalimbali wa awamu za nchi yetu kwa kazi kubwa walizofanya na kuwezesha kupatikana mafanikio haya.
Wa kwanza ni Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, wa pili ni Mzee wetu Karume, watatu Mzee wetu Ali Hassan Mwinyi ambaye yuko hapa bado kijana kweli na anaonekana kijana kuliko mimi, na ikabidi anipe siri yake lakini siri aliyoniambia ni kwamba lazima niwe na wake wawili.
Lakini pia Mzee Mkapa, pamoja na mzee aliyemaliza muda wake hivi karibuni Mzee Jakaya Mrisho Kikwete. Kwa hiyo kwa niaba yenu napenda niwapongeze sana viongozi hawa, lakini pia niwapongeze viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mawaziri Wakuu wastaafu, Mawaziri wastaafu, Makatibu Wakuu, Wakuu wa wilaya, mikoa, na wote ambao walishiriki kwa njia moja au nyingine kutufikishia maendeleo haya ambayo leo tunayasherehekea miaka 55 ya uhuru wetu.
Ndugu zangu Watanzania, licha ya mafanikio tuliyoyapata ni dhahiri kuwa bado zipo changamoto na matatizo ya umasikini, ukosefu wa ajira, upatikanaji wa huduma za jamii, rushwa na kadhalika.
Napenda kutumia fursa hii kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendelea na kuziendeleza jitihada zote zilizofanywa na Serikali zilizotangulia. Lakini pia tutajitahidi kwa nguvu zote katika kutatua hizo changamoto ambazo nina uhakika tumeanza kuzishughulikia.
Serikali ya Awamu ya Tano iliingia madarakani mwezi Novemba mwaka jana (2015) baada ya kufanyika uchaguzi wa mwezi Oktoba.
Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu, nilinadi ilani ya uchaguzi ya CCM ambayo ilisheheni mambo mengi na wananchi wakaamua kutupa. Niliahidi kujenga misingi imara ya kuifanya nchi yetu kuwa ya uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025.
Kulingana na Dira yetu ya Taifa ya Maendeleo, niliahidi kupambana na uzembe na ubadhirifu serikalini pamoja na kuboresha huduma za jamii afya, elimu na maji na kadhalika.
Ndugu zangu Watanzania tumeanza. Katika bajeti ya mwaka huu ambayo tulionayo, ambao thamani yake ni bilioni 29.5 tulitenga aslimia 40 ya fedha zote ziende kwenye miradi ya maendeleo. Katika miradi hiyo ya maendeleo, tumeanza kuiwekea mikakati ili kuhakikisha kwamba nchi yetu inajengeka kiuchumi kikamilifu.
Miradi hiyo inahusisha miradi ya umeme, ambapo kuna miradi kadhaa hata Dar es Salaam na maeneo mbalimbali kwa Dar es Salaam Kinyerezi, Kinyerezi 1, Kinyerezi 2, Kinyerezi 3 ambayo tunaendelea nayo katika kuhakikisha kwamba tunapata umeme wa kutosha.
Katika miundombinu, katika bajeti hii zimetengwa zaidi ya trilioni 5.6, tumetenga trilioni 1 kwa ajili ya kujenga reli ya kisasa. Na tenda zimeshatangazwa, nina uhakika tutaanza na kilometa 200 ambazo lengo ni kuhakikisha tunaiunganisha Tanzania na nchi jirani za Rwanda, Burundi, Uganda, Kigoma, Mwanza na reli ya standard gauge ambayo inabeba uzito mkubwa zaidi.
Katika suala la usafiri wa anga, tumekwishanunua mpaka sasa hivi ndege sita. Ndege tatu ni za aina ya Q 400 Bombardier ambazo zina uwezo wa kubeba abiria 76. Ndege mbili ni za aina na CS30 ambazo zitaanza kutumika kwa mara ya kwanza Afrika, zilikuwa zinatumika kule Swiss Air ambazo zenyewe zina uwezo wa kubeba watu kati ya 137-150.
Ndege hizo zitakuja kwenye mwezi wa tano au wa sita mwaka 2018. Lakini ndege nyingine kubwa zaidi ambayo tumeshaanza mipango ya kulipa fedha ni aina ya Boing 787 8-Generation ambayo ina uwezo wa kubeba watu 262.
Tumefanya hivyo kwa lengo la kujenga uchumi na utalii wa nchi yetu. Huwezi ukazungumzia kuimarisha utalii wakati huna usafiri wa ndege unaoutegemea wewe.
Kwa hiyo, hiyo ni baadhi ya mikakati ambayo tunaendelea nayo, lakini katika sekta ya afya. Napo bajeti ya afya imeongezeka. Na katika bajeti ya mwaka huu fedha zilizotengwa kwa kununulia madawa zimeongezeka toka bilioni 31 hadi bilioni 250.
Katika sekta ya elimu nako tumeongeza fedha. Na tumeanza kutoa elimu bure, kwa kutenga bilioni 18.77 kila mwezi ambapo zinasaidia kutoa elimu bure shule ya msingi hadi sekondari.
Lakini katika elimu ya vyuo vikuu tumeongeza pia bajeti kutoka bilioni 340 zilizotengwa mwaka jana hadi bilioni 483 na hivyo kuongeza idadi ya wanafunzi watakaojiunga na chuo kikuu kutoka 98,000 hadi kufikia 125,000.
Kwa sababu ya hilo, wanafunzi waliongezeka katika kujiunga na shule za msingi sasa wameongezeka kwa asilimia 88, sekondari asilimia 26. Lengo ni kuhakikisha kwamba tunawapa elimu kwa kiwango kikubwa kwa Watanzania wote.
Bajeti pia katika makusanyo yameanza kuongezeka, kutoka makusanyo ya bilioni 850 hadi wastani wa makusanyo ya trilioni 1.2.
Ndugu zangu, tunafanya haya yote na mengine sikuyataja hapa kwa lengo la kuiweka Tanzania mpya. Pamoja na mazuri haya yote ambayo tumekuwa tukijitahidi kuyafanya, changamoto zimeendelea kuwapo.
Baadhi ya changamoto ni pamoja pia na ufisadi na rushwa ndani ya baadhi ya watendaji. Ambapo wakati tunazungumzia kuhusu mshahara na wafanyakazi kuamua kuwapunguzia payee kutoka asilima 11 hadi asilima 9 tumejikuta mpaka sasa hivi tuna wafanyakazi 19,000. Tumekuwa tukitoa fedha kwa ajili ya TASAF kwa kaya zilizo masikini. Mpaka sasa hivi, kaya zilizo masikini hewa zimefika 55,000. Wakati tunajitahidi kuboresha wanafunzi kwa kusoma bure tumejikuta mpaka sasa hivi tuna wanafunzi hewa 65,000. Na mambo mengine mengi.
Kwa hiyo, napenda kuwathibitishia ndugu zangu Watanzania, juhudi tunazozichukua na ambazo tumeanza kuzichukua katika Serikali ya Awamu ya Tano ni kwa lengo la kuboresha maslahi ya Watanzania wote, wala si kuboresha maslahi ya Watanzania wachache ambao walikuwa wamezoea kula jasho la watu wengine.
Kwa hiyo, tutaendelea kuchukua hatua kali ikiwa ni pamoja na kuwatumbua hadharani – wale waliokuwa wamezoea kutumbua hadharani mali za Watanzania.
Lakini tutaendelea kuchukua hatua kali katika masuala ya rushwa. Kwa sababu rushwa ni kansa.
Napenda nitumie nafasi hii kulishukuru sana Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na vyombo vya utoaji haki kwa kupitisha sheria ya kupambana na rushwa. Tutaisimamia vizuri, nilishazungumza na Jaji Mkuu, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na vyombo vingine – Polisi na PCCB – kuweza kuhakikisha kwamba vinatenda haki.
Lakini pia, wale wanaostahili kupata malipo yao kutokana na kutufikisha hapa waweze kushughulikiwa kikamilifu. Lakini pia Serikali ninayoiongoza imepanga kuhakikisha kwamba tunaondoa uonevu. Hasa uonevu kwa wananchi wanyonge.
Kwa hiyo, tutaendelea kushirikiana na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi wanyonge ili waweze kufaidika na Tanzania yao.
Ndugu angu Watanzania, wakati tunaadhimisha miaka hii 55 ya kupata uhuru, ombi langu kwenu tuendeleze kudumisha amani yetu.
Amani ndiyo msingi mkubwa wa maendeleo, bila amani hakuna maendeleo. Hivyo basi tuendelee kulinda amani yetu na kufichua watu wenye nia ya kuhatarisha amani yetu.
Sambamba na kulinda amani yetu, hatuna budi kudumisha na mshikamano wetu ambao ndiyo nguvu na silaha yetu kubwa kama Taifa. Lakini pia tuendelee kuulinda muungano wetu ambao ni silaha kubwa ya umoja wetu ili Tanzania tuendelee kwenda mbele.
Mwito wangu pia kwa Watanzania ni vyema tunaendelea kufanya kazi, kila mmoja wetu lazima afanye kazi kwa bidii kama ambavyo kaulimbiu yetu ya Hapa kazi tu inavyoeleza.
Uwe mkulima, uwe mfanyakazi, uwe mfugaji, uwe mvuvi, uwe mfanyabiashara na kadhalika sisi wote tujipange kutekeleza haki yetu ya kufanya kazi. Na iwe kazi iliyo halali.
Wazee wetu walipambana kwa kutuletea uhuru, sisi wa kizazi cha sasa tunao wajibu wa kufanya kazi kwa bidii ili kulijenga Taifa letu kwani hatuna shangazi, babu, mjomba atakayeweza kutuletea maendeleo ya nchi yetu.
Maendeleo ni lazima tuyafanye na tuyalete sisi wenyewe kwa ajili ya kufanya kazi.
Ndugu zangu Watanzania na ndugu zangu wana-Dar es Salaam, leo ilikuwa ni siku ya kwenye sherehe. Ni siku ya sherehe ya kuzaliwa uhuru wetu, huwa ni siku ya kufurahi.
Nipende kuwashukuru sana kamati ya maandalizi ya sherehe hii, imefanya kazi nzuri, lakini nipende kuyashukuru majeshi yetu yote ambayo yameonesha umahiri mkubwa. Na sisi wote tutatoka hapa tukijua kuna majeshi ambayo yako kweli mbele kwa ajili ya kulinda nchi yetu.
Wameonesha umahiri mkubwa, gwaride zuri na mambo yote mazuri. Hongereni sana makamanda mnaoongoza vikosi mbalimbali ambao mmetoa burudani ya leo. Niwashukuru sana viongozi mbalimbali, wazee kwa vijana, kinamama ambao wamejitokeza kwa wingi sana katika siku hii muhimu ya kusherekea uhuru wetu wa miaka 55.
Niwashukuru Mabalozi kutoka nchi mbalimbali ambao wamejitokeza hapa kuja kushiriki na sisi. Niwashukuru sana wananchi wa Dar es Salaam chini ya uongozi mahiri wa Mkuu wa Mkoa, Ndugu Makonda, kwa kuzipamba sherehe hizi muhimu sana.
Niwashukuru sana vikundi mbalimbali vya ngoma pamoja na nyimbo, vikundi vya Makomandoo na wengine wote walioshiriki hapa na kuifanya sherehe hii muhimu.
Ndugu zangu Watanzania, napenda kuwahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kufanya kazi na tutafanya kazi kweli kweli. Kwa bahati nzuri viongozi wote niliowateua kunisaidia kazi akiwamo Waziri Mkuu, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa ni wachapakazi.