Ndugu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara nchini,
Ndugu Katibu Mkuu Kiongozi,
Ndugu Wenyeviti wa sekta mbalimbali,
Wadau wakubwa wa Sekta Binafsi, Mabibi na Mabwana
Nafurahi kwa kusema, kwanza namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha sisi sote kuwapo hapa leo. Niwashukuru ninyi viongozi wa sekta binafsi na wadau wengine wa Baraza la Taifa la Biashara mkiongozwa na Mwenyekiti wenu, Mengi na kina Mafuruki pale, kwa hatua yenu ya kuwatuma mara kwa mara wasaidizi wangu mkiomba kukutana na mimi kwa lengo la kutaka kuzungumza nami, lakini pia mkisema mnataka kunipongeza.
Wakati mwingine nilikuwa najiuliza, wafanyabiashara hawa ninaowadai kodi kila siku wanataka kunipongeza kwa lipi? Lakini napenda niwahakikishie kwamba nimefarijika sana sana kukutana nanyi leo.
Nataka niwahakikishie kwamba natambua kwamba sekta binafsi ni muhimu sana katika ujenzi wa uchumi wa soko, na ninatambua pia kwamba kazi ya Serikali yoyote ile duniani ni kuhakikisha inawajengea mazingira mazuri ya biashara zenu.
Nataka kuwahakikishia kwamba Serikali yangu inakusudia kuwapunguzia aina yoyote ya vikwazo na urasimu katika masuala yote yanayohusu uwekezaji. Nafahamu tukiwa na sekta binafsi inayofanya kazi yake vizuri, sekta binafsi inayotanguliza maslahi ya taifa mbele, nchi hii haiwezi kuwa hapa ilipo kiuchumi, badala yake itasonga mbele.
Natambua umuhimu wa sekta binafsi katika ujenzi wa uchumi wa soko, natambua pia wajibu wa Serikali katika kuwahakikishia mazingira maßzuri ya kibiashara wote waliomo katika sekta binafsi.
Nataka kuwahakikishia kwamba Serikali ya Awamu ya Tano itahakikisha inawaondolea vikwazo na urasimu wa aina yoyote unaosababisha uwekezaji vitega uchumi katika nchi hii ushindwe kushamiri, hasa kwa kuondoa utitiri wa kodi na ushuru wa bidhaa kwa wafanyabiashara wadogo.
Haiingia akilini, na naomba nizungumze kutoka moyoni mwangu, lakini kama nitawakwaza nitaomba mnisamehe kwa maana inasemwa kwamba msema ukweli yeyote ni mpenzi wa Mungu.
Kwa hali halisi ilivyo ndani ya taifa letu hili, nilitegemea ninyi watu wa sekta binafsi muwe watu wa kwanza kukaa chini na kusema basi inatosha, kama taifa, hatuwezi kuendelea hivi tulivyo. Yapo mengi nimeyasikia kutoka kwenu kuhusu changamoto zinazowakabili, nami nawahakikishia nitayazingatia na kuyafanyia kazi kwa ukamilifu.
Tutaangalia pia uwezekano wa kupunguza kodi na ushuru pamoja na utitiri wa kodi zenye kero kama nilivyotangulia kusema. Nilipokuwa Kagera na Kilimanjaro wakati wa kampeni, zao la kahawa nilikuta likiuzwa kwa kutozwa kodi mbalimbali karibu 26.
Kwa sababu hiyo, wakulima wa kahawa katika maeneo hayo, hasa kule mkoani Kagera, iliwabidi sasa kusafirisha kahawa yao kwa njia ya magendo kwenda Uganda.
Lakini, ukiangalia soko la Uganda la kahawa (kimataifa) ni lile lile linalotumiwa na Tanzania, isipokuwa wenzetu hawa hawana kodi nyingi katika zao hili la kahawa ndiyo maana bei yao ni nzuri kiasi cha kuvutia wakulima wetu.
Najaribu kutoa mfano huu wa kahawa nikiwa na mifano mingi ya aina hii, mfano kwenye sekta ya sukari na kadhalika na kwenye malighafi ya mafuta (crude oil) kwa sababu hata mimi pia ninao utaalamu wa masuala ya mafuta.
Natambua hata baadhi yenu wafanyabiashara mnaoagiza malighafi kutoka nje kwa ajili ya viwanda vyenu, mnadai kuagiza malighafi wakati kumbe mnaagiza bidhaa zilizo tayari.
Haiingii akilini kwa mfano katika sekta ya madini, nchi inayoongoza katika soko la dunia kwa kuuza madini ya tanzanite iwe India na ya pili Kenya wakati madini hayo yanapatikana hapa Tanzania pekee duniani kote.
Haiwezekani mchanga unaohesabika kama ‘waste products’ (makapi) kutoka kwenye machimbo ya madini, unasafirishwa kwenda nje makontena kwa makontena eti kwa ajili ya kwenda kutenganisha mchanga na madini wakati hakuna Mtanzania anayejiridhisha ni kiasi gani cha madini kilichopatikana huko baada ya kutenganishwa.
Kwanza makontena haya ya mchanga yanasafirishwa kwa njia ya barabara hivyo kuharibu barabara zetu. Lakini sote tunafahamu kwamba katika mchanga ule wa madini huwa kuna madini mengine ya copper (shaba) na litanium na hata mercury (zebaki).
‘Boiling point’ ya kutenganisha madini haya tunaifahamu hata sisi, lakini mchanga unasafirishwa hadi bandarini baadaye kwenda Ulaya na nchi za mbali. Sekta binafsi ipo, inaona; Serikali ipo, inaona.
Niwaombe sana sana, nawapenda matajiri. Naamini nchi hii ikiwa na matajiri wazuri, hatutahitaji tena vimisaada vidogo vidogo kutoka nje, badala yake nchi hii itakuwa taifa la wafadhili kwa mataifa mengine ya nje.
Kwenye sekta ya benki kwa mfano, Dk. Kimei (Dk. Charles Kimei, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB), anafahamu. Tunazo benki kubwa karibu 54 na zote zinafanya biashara na Serikali lakini zote hizi hazijajikita chini kwenda kwa wananchi.
Juzi hapa tumejaribu kufanya uchambuzi tukakuta karibu Sh. bilioni 550 zinazozunguka katika benki hizi ni fedha za umma, ambazo kiukweli ni fedha za Serikali zinazotokana na mfumo wa Hati Fungani. Kwa hiyo, kwa maana nyingine, Serikali inafanya biashara na mabenki haya kwa kutumia fedha zake yenyewe.
Na huu ndio ukweli wenyewe. Nikitaja fedha za mashirika ya umma zilizoko huko kwenye mabenki hayo ni nyingi mno, tena nyingine hazitozwi hata riba. Mwenyekiti wenu (Dk Mengi), ametaja mfano wa kwenye viwanda na kusema vipo viwanda karibu 400 ambavyo vimetoa ajira 100,000 kwa Watanzania.
Wakati anatoa mfano huu, alikuwa anajisifia kwamba sekta ya viwanda nchini kwa sasa imetoa mchango mkubwa wa ajira kwa taifa hili kwa kuajiri watu hao 100,000.
Lakini, nikifikiria nilipokuwa Wizara ya Ujenzi, sekta moja tu ya ujenzi, ilikuwa na ajira milioni 1.13, wanaotokana na makandarasi 4,500 wanaofanya kazi za ujenzi kwenye miradi 17,762 nchini, wahandisi 1,524 na madaraja 7,211 yaliyokuwa yanajengwa nchi nzima.
Kama tulikuwa na viwanda tukavibinafsisha kwa nia ya kuongeza ajira nchini, lakini pia vinavyozalisha bidhaa ili Serikali ikusanye kodi. Eneo la Morogoro tulipanga liwe eneo la viwanda. Waliobinafsishiwa viwanda vile wengine ni viongozi wa CCM, lakini wengi wamevigeuza viwanda kuwa magodauni, wengine wamevigeuza kuwa mazizi ya mbuzi!
Nazizungumzia changamoto hizi ili kwa pamoja tujione wote ni Watanzania. Nenda kiwanda cha ngozi Mwanza, nenda kiwanda cha Kibo (Moshi) na vingine vingi tu. Tanzania yetu hii inao ng’ombe milioni 23.3, mbuzi milioni 16 na kondoo milioni sita, achilia mbali mbwa wa kule Iringa na kwingine nchini ambao idadi yao inafikia milioni 4.2.
Tanzania tulikuwa nchi ya tatu kwa kuwa na ng’ombe wengi barani Afrika, kabla ya Sudan kugawanywa na kupatikana nchi ya Sudan Kusini. Kwa sasa nchi yetu bila shaka itakuwa ni ya pili baada ya Ethiopia.
Mheshimiwa Shamte anafahamu tuna viwanda vingapi vya nyama hapa nchini. Hatuna viwanda vya aina hiyo, inatubidi tusafirishe malighafi ya ngozi na ng’ombe wazima nje ya nchi. Kuna ubaya gani kwetu sisi kama taifa kuwa na viwanda vyetu vya ngozi ili kutengeneza viatu walau vya wanajeshi wetu na polisi?
Ukweli ni kwamba wenzatu wanaojua kwamba sisi Tanzania ni wa pili barani Afrika kwa kuwa na ng’ombe wengi, lakini hatuna hata kiwanda kimoja cha ngozi, ukweli wanatucheka na kujiuliza tuna matatizo gani vichwani mwetu.
Tunaanza kuoneana wivu, naamini wengine hata humu ndani ya wanajumuiya ya wafanyabiashara mnaoneana wivu wenyewe kwa wenyewe, sina uhakika katika hili la wivu ninyi kwa ninyi, lakini ndiyo hivyo.
Sijui tuna viwanda vingapi vya maziwa hapa nchini. Tulikuwa nacho cha Brockbond kule Arusha, ambacho kilikuwa kinanunua maziwa kutoka kwa ndugu zetu wafugaji wa jamii ya Kimasai, lakini wakawa wanapeleka kuuza maziwa hayo nchini Kenya, halafu wanatuletea kutuuzia bidhaa zitokanazo na maziwa na sisi tunashangilia.
Yote haya yanafanyika ndani ya nchi hii wakati Serikali ipo, sekta binafsi ya wafanyabiashara wapo, mawaziri wapo, makatibu wakuu wapo na Rais mimi nipo. Najaribu kueleza changamoto zote hizi hapa ili mzifahamu na tuchukue hatua kwa umoja wetu.
Ndiyo maana niliposikia kwamba mnataka kuonana na mimi nilifurahi sana kwa sababu ninafahamu kwamba bila ninyi watu wa sekta binafsi, hakuna Tanzania yenye hadhi na heshima yake mbele ya jumuiya ya wafanyabiashara wa kimataifa.
Sijui kama mnafahamu, lakini ukweli ni kwamba tangu Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2015/2016 ipitishwe Juni 30, mwaka huu, hakuna fedha yoyote iliyokwisha kutolewa kwenye wizara kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Kama kutolewa, basi tutakuwa tumeanza kuzitoa kwenye wizara kuanzia mwezi huu (Novemba 2015), Katibu Mkuu Kiongozi yuko hapa, aseme. Miezi sita tangu bajeti hiyo ipitishwe, hakuna hata senti kwa ajili ya maendeleo iliyotolewa na Hazina kwa ajili ya wizara yoyote, bali zilizokuwa zikitolewa ni zile za mishahara tu na kwenye shughuli nyingine.
Kwa hiyo, ninapojaribu kusema haya na kusisitiza umuhimu wa ninyi kulipa kodi, hatufanyi haya kwa sababu ya jeuri, bali kwa nia njema ili malengo ya Watanzania yaweze kutimia.
Kwa hiyo, niwaombe sana ndugu zangu. Wafanyabiashara wote ndani ya nchi hii, nataka sana mfanye biashara kweli kweli, hasa kwa wafanyabiashara wazalendo. Nawaomba wala msiwe na wasiwasi kabisa, hata mkitaka kuwekeza kwenye gesi, fursa ipo, kwangu hakuna kikwazo kabisa!
‘The room is there’ (nafasi ipo) kwa sababu hakuna nchi yoyote duniani ambayo iliendelea bila kuwasaidia watu wake wa chini. Ukiwasaidia, ukawajenga wazalendo, wengine hao wa nje watakuja kuwekeza kwa njia ya ubia, hivyo kusaidia kuimarisha soko la uchumi wa taifa letu.
Huwezi ukawa kiongozi wa nchi halafu ukasema hawa (wazalendo) hawawezi au hawana uwezo wa kuwekeza. Kwa sababu gani? Hao wa nje wanaoweza kuwekeza vitega uchumi vyao hapa kwetu wana kundi gani la damu? Mbona kundi lao la damu ni sawa na la kwetu tu? Nawaomba ndugu zangu mjiamini, lakini mtangulize uzalendo kwanza kwa nchi yenu!
Tuje kwenye sekta ya utalii. Mara zote, kila tunapozungumzia utalii, tunaelezea idadi ya watalii milioni 1.1 wanaoingia kila mwaka, halafu tunasema mwakani tunatarajia watalii milioni mbili.
Hatujiulizi hao watalii milioni 1.1 walioingia waliingiza shilingi ngapi? Hatujiulizi kama fedha zao hizo walilipa hapa nchini na ni kiasi gani kililipwa na zilitumikaje kwa maana ilivyo ni kwamba watalii wengi wa nje wanalipa huko huko kwa ‘credit card’ zao, halafu wanakuja kwetu mikono mitupu, sisi tunabakia kushangaa sura zao.
Tunahesabu idadi ya watalii walioingia nchini mwetu bila fedha. Si ni bora mara 100 wangefika watalii watano tu wa kutulipa fedha hapa tukajua wamelipa kiasi gani cha fedha kuliko idadi hiyo ya watalii milioni ambao hatujui walilipa shilingi ngapi na walimlipa nani ili kuja nchini mwetu kufanya utalii?
Kwa nini Misri inapokea watalii wengi zaidi yetu wanaokwenda kwa ajili ya kushangaa mapiramidi na kuota jua la jangwani, wakati hapa kwetu kuna jua linalolingana na wao? Tuna vivutio vingi pamoja na fukwe nyingi za bahari?
Ndugu zangu wafanyabiashara, najaribu kuzungumza yote haya kwa kuwakumbusha ili tufahamu changamoto nyingi zinazotukabili ambazo ninyi kama sekta binafsi, mkiamua, kwa pamoja tunaweza kuiokoa nchi hii ambayo imebahatika kujaaliwa kila kitu na kila aina ya rasilimali asili, badala ya miongoni mwenu kuanza kukwepa kodi.
Nafahamu, katika mchezo huo wa kukwepa kodi, baadhi ya wafanyabiashara wadogo hutakiwa kukusanya fedha na kumpatia mtu mmoja fulani ili huyo ndiye akawakombolee mizigo yao bandarini.
Mchezo wa aina hii kwa mfanyabiashara wa kweli anaweza akaufanya kwa muda tu, lakini hauwezi kuwa wa kudumu kama kweli anaipenda na kuithamini biashara yake. Wanadhani Serikali haifahamu, kumbe tunaujua mchezo wote huu!
Ndiyo maana natumia muda mwingi kuwaomba tushirikiane. Wale ambao kwa bahati mbaya walikwepa kodi, wakakimbia na makontena yao, natoa muda wa siku saba wawe wamelipa kodi yetu ya Serikali. Wakilipa kodi yetu, hakuna atakayewashitaki kwa sababu tunachohitaji sisi ni fedha zetu, vinginevyo watajipa shida ya bure tu kwa sababu kontena si sindano ya kuficha isionekane.
Kama kuna mfanyabiashara yeyote kati yenu au nje ya hapa atakayetaka kuwekeza mahali popote, lakini akacheleweshwa na mtu yeyote aliyeko chini ya mamlaka ya uteuzi wangu kwa sababu yoyote ile, nitakuomba Mwenyekiti nitafute, njoo kwangu, huyo hatakuwa na nafasi ndani ya Serikali yangu.
Nafahamu kwamba Minja (Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Wadogo nchini) na wafanyabiashara wenzake wadogo, walikuwa na matatizo na hizi mashine za kukusanyia kodi za TRA. Siku moja hivi nikakaa na Kamishina Mkuu wa TRA, nikamuuliza mashine hizi zinazoleta mgogoro ni zenu na mnazinunua bei gani? Kwani ni lazima muwauzie wafanyabiashara?
Nikamuuliza; kama mashine halali na ni zenu, kwa nini hamuwapi bure ili waisaidie Serikali kukusanya kodi vizuri na kwa ufanisi? Nilimwambia kwa nini mnapoteza muda wote huo kwa mabishano wakati mashine zote walizonazo TRA, thamani yake haizidi hata Sh. bilioni 12?
‘Simple logic’ tu ambayo haihitaji hata elimu ya Chuo Kikuu. Wakati TRA inaendeleza mgogoro ule na wafanyabiashara wadogo hawa kuhusu mashine hizi, kilikuwa ni kipindi cha kampeni, nikalazimika kukutana na kina Minja kuwaambia wayamalize wasije wakanisababishia kukosa kura zao, na sijui kama kweli nilipata hizo kura zao!
Ndugu zangu, napenda tuambiane ukweli, kampeni zimekwisha, sasa ni wakati wa kufanya kazi. Mimi ninawapenda wote, maana katika siasa zetu hizi anaweza akatokea mtu akaanza kusema oh huyu alikuwa upande ule, huyu alikuwa upande huu… hapana, huyo hatufai, sisi sote ni Watanzania, no matter ni chama gani, no matter ni kabila gani, baada ya uchaguzi kumalizika, sote tunabakia kuwa taifa moja.
Ningependa tushirikiane wote, katika miaka mitano yangu hii ya uongozi wangu kabla ya Uchaguzi Mkuu mwingine, tujenge nchi yetu kwa pamoja kama Mungu atakavyotujalia, katika kukabiliana na changamoto hizi zinazolikabili taifa letu, tusahau yaliyopita, tugange yajayo, tusonge mbele!
Kila mtu na mahali pake pa kazi, asimame imara kwa sababu naamini ndani ya Tanzania tunao watu wazuri wenye taaluma zao, waadilifu na wawajibikaji, wengine hao Mheshimiwa Mwenyekiti (Reginald Mengi), wamo ndani ya chama chako cha wafanyabiashara wa sekta binafsi nchini.
Kama kuna vi-kodi vidogo vidogo mnadhani vinawakwamisha katika shughuli zenu za biashara au vinawachelewesha kwa namna moja au nyingine, viwekeni wazi kwetu kupitia Baraza lenu la Taifa la Biashara tuviondoe.
Sisi kama Serikali, kwa maoni yangu, ni bora tukusanye kodi kidogo kidogo kutoka kwa watu wengi zaidi kuliko kukusanya kodi kubwa kutoka kwa watu wachache, ambao hao hao wachache nao wanakwepa kulipa kodi na wala hutuipati.
Niwaombe sana ninyi wafanyabiashara, kwa sababu tunamtanguliza Mungu mbele, basi tuwatangulize Watanzania mbele pia. Kamwe msitumie nafasi zenu za kuwa matajiri kuwanyima haki wengine wa chini.
Saa nyingine inashangaza unapoona eneo la wazi kwa ajili ya matumizi ya umma, matumizi ya watu wote, mtu analing’ang’ania eneo hilo hilo kwa sababu tu ya uwezo wake wa kifedha wa kuweza kuwarubuni watu wa serikalini, unataka ulinunue kwa ajili ya kuendesha biashara zako.
Halafu, watu wa Manzese na maeneo mengine waliozoea kutumia eneo lao hilo kwa kwenda kufurahia michezo yao, kwenda kuogelea, wanakosa haki yao ya kutumia eneo hilo… kwa kuwa tu una fedha, unaweza hata ukakimbilia mahakamani, ukashinda kesi kwa kuhalalishiwa eneo hilo kwa sababu tu ya utajiri wako, sawa tu!
Lakini ndugu zangu nataka niwaambie, Serikali ipo, na Serikali yenyewe hiyo ni ya Rais Magufuli. Kama mnataka eneo kubwa kwa ajili kuendeleza biashara zenu, mbona maeneo hayo yako mengi tu hapa nchini? Kachukue huko ambako hakuna maslahi ya umma wala migogoro!
Mkishaenda kuchukua huko na kuwekeza mitaji yenu, watu lazima watawafuateni huko huko, hivyo kupunguza misongamano ya watu katika jiji letu. Lakini kusema utang’ang’ania hapo hapo tu kwa sababu ya utajiri wako, nasema haitawezekana katika utawala wangu huu.
Kwa bahati nzuri sana mimi nimekaa katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, nayaelewa maeneo yote ambayo hayapaswi kuguswa.
Nasema tena na tena, tumwogope Mungu, lakini pia tuwaogope Watanzania.
Ndiyo, unaweza ukaamua kujenga kwa nguvu kwa sababu ya jeuri yako ya fedha, lakini kwa jiji kama hili la Dar es Salaam lenye wakazi zaidi ya milioni tano, ukiamua kujenga kwa sababu ya jeuri ya fedha zako, nao hao watu milioni tano wakiamua kutoka nje na kuanza kubomoa jengo lako, utafanyaje? Hutakuwa na uwezo wa kuwazuia watu hawa!
Nawaombeni sana, mkiona kitu kinaweza kuvunja sheria, hata kama sheria hiyo una uwezo wa kuipindisha. Kwa bahati nzuri sana, Sheria Namba Nne ya mwaka 1999, Sheria Namba Tano ya Vijiji ya mwaka 1999 pamoja na Sheria ya Mipango Miji na matumizi ya ardhi ya mwaka 2007, zinaeleza vizuri upana wa eneo, kila mtu anajua hivyo na Mahakama zetu zinajua pia, lakini kwenye Mahakama zetu hizi mtu anaweza akashinda kesi yoyote, inategemea alivyojipanga kushinda kesi.
Kwa hapa kwetu, mtu hata kama unataka kununua Ikulu inawezekana tu, lakini nawahakikishia kwa sasa haiwezekani, labda kwingine huko (kicheko). Ndiyo! Mtu akitaka kununua Ikulu, kwanza atauliza Hati ya Ikulu iko wapi. Na kwa bahati mbaya, maeneo yote ya Serikali hayana Hati! Hivi sasa ndiyo tumeanza mpango wa kuandaa Hati kwa ajili ya maeneo ya Serikali, hivyo ni rahisi leo mtu kughushi hati ya kumiliki ardhi ya Ikulu na akashinda kesi yake.
Na kwa bahati nzuri sana mtu ukitaka kughushi hati ya eneo la ardhi inawezekana tu kwa sababu anachemsha majani ya chai na kuchukua karatasi nyeupe na kuichovya ndani ya maji hayo yanayochemka, ukitoa tu inaonekana hati hiyo ilitolewa mwaka 1931.
Ndugu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Sekta Binafsi na wadau wengine mbalimbali wa biashara hapa nchini, nataka kusema kwamba Serikali ya Awamu ya Tano ipo pamoja na ninyi, itasaidia na kushirikiana nanyi mahali popote mtakapokwama ili mfanyebiashara zenu vizuri, kwa uhuru na kwa faida zaidi.
Mfanyabiashara yeyote yuko ‘after maximization of profit’. Kupata profit ya kutosha. Lakini, katika kupata faida yenu hiyo, niwaombe sana nanyi kukumbuka kumlipa Kaizari chake, yale mapato yote ya revenue yanayotakiwa kupatikana, yapatikane. Kwa njia hii, tutaweza kuongoza nchi yetu vizuri, nawaombeni sana!
Nafahamu Mwanyika yuko hapa. Kwenye madini kule kuna ndege zinatua kila siku. Sina uhakika vile vyote vinavyobebwa na ndege hizo tunavijua, lakini kwa kuwa nafahamu wewe ni Mbena, sijui ni Mhehe na mna tabia ya kujinyonga kila mambo yanapoharibika, basi simamia haya mambo vizuri.
Kwa kweli ndugu zangu mimi ninawapenda sana ninyi wafanyabiashara wa nchi hii, mtapata sapoti kubwa sana kutoka kwenye Serikali yangu kwa asilimia 100 wala hamtakwama.
Kama kuna mahali popote mtakwamishwa, tutachukua hatua, tena hatua za papo hapo. Kama mtakwamishwa kwa misingi yoyote ya ajabu ajabu ya rushwa, Ndugu Mwenyekiti msisite kunitafuta, ikibidi mtafuteni Katibu Mkuu Kiongozi.
Tunataka wawekezaji wa ndani na nje wawekeze vya kutosha katika nchi hii ili Serikali yetu ipate mapato ya kutosha kwa kwenda mbele. Lakini niwaombe na ninyi muwe wazalendo wa kweli kwa nchi yenu. Mtangulize maslahi ya Tanzania kwanza, kwa sababu hatuwezi tukawa tunachezewa wakati wote, enough is enough!
Wafanyabiashara wa Tanzania tumedharauliwa vya kutosha, ifike mahali sasa kwa pamoja tuushike wenyewe uchumi wa Tanzania. Tunazo rasilimali za kutosha kuanzia kule Moa kwa kina Shamte hadi Msimbati kule Mtwara kuna jumla ya kilomita 1,422.3 kwenye ukanda wote wa bahari, hakuna hata kiwanda kimoja kikubwa cha samaki.
Tulipokamata meli ile ya uvuvi haramu, walisema walikuwa na tani 70 za samaki, lakini ukweli ni kwamba walikuwa na tani karibu 300. Samaki wakubwa waliokutwa mle ndani ya meli, mmoja alikuwa na uzito wa kilo 310. Ukienda kule kwenye rada na kuangalia kule baharini na kuona idadi ya meli zinazovua samaki katika ukanda wetu huu kwa njia haramu, unaweza kutoa machozi.
Meli nyingine hizo zina hata viwanda ndani yake, zinavua na kufanya kazi humo humo bahari ya ku-process bidhaa zinazotokana na mazao ya samaki. Katika hali hii kuna ubaya gani miongoni mwenu ninyi wafanyabiashara mlioko hapa, mmoja wenu akamiliki meli kubwa ya kwake ya uvuvi kama hizo?
Mtu huyo akawa anavua samaki kwenye maji marefu kule baharini na kuleta hapa ndani, akawa anawa-process mwenyewe kwenye viwanda vyake, anasafirisha hawa samaki aina ya tuna kupeleka hata Ulaya, watu wetu wa hapa wakapata ajira, Serikali ikapata mapato yake na mabaki ya samaki yakatumika kutengeneza hata chakula cha kuku, huku naye akijipatia fedha zake na maisha yakaendelea!
Nasema hivyo kwa sababu kama mtu anatoka Ulaya au Mashariki ya Mbali anakuja hadi huku kufanya kazi hiyo ya uvuvi, maana yake anapata faida kubwa. Huyu hafanyi kazi ya hasara. Kama hivyo ndivyo, kwa nini basi kazi hiyo ya faida kubwa kiasi hicho isifanywe na mmoja wenu kutoka miongoni mwenu hapa?
Ndiyo maana nasema hapa kwamba changamoto kubwa ipo kwenu ninyi hapa. Inawezekana. Ifike mahali sasa wa kukaa pamoja ninyi watu wa sekta binafsi, hata kama ni kwa kugawana maeneo, mnaweza kufanya kweli.
Najua, pamoja na kumtanguliza Mungu mbele, tunaweza kufanikiwa sana kwa njia hii!
Ndugu Mwenyekiti, nimalize hotuba yangu hii kwa kuwashukuru tena sana. Kwa kukutana nanyi, nimepata nafasi hii nzuri. Nataka niwahakikishie kwamba nitajitahidi kuwa pamoja nanyi kila inapobidi. Leo nimejifunza mengi kutoka kwenu, nitaendelea kujifunza zaidi kwa sababu tunayo mambo mengi zaidi ya kujifunza.
Ndiyo maana hata aliyetoa mfano hapa, amesema hata njiti za kuchokonolea meno tunaagiza kutoka nje wakati nchi hii inao msitu mkubwa wa Mgololo, kuna miti mingi kule, mbao zinasafirishwa nje, wanakwenda kutengeneza vijiti vya meno wanatuletea, halafu tunanunua huku tukishangilia.
Fenicha za maofisini vivyo hivyo. Tunazo mbao za kutosha za kila aina, mfano za mitiki na kadhalika, lakini kila siku tunashuhudia magogo yakipita bandarini kwetu hapa yakisafirishwa kwenda nje.
Yote hayo yanafanyika katika nchi hii, lakini tunalo Baraza la Taifa la Biashara ambao wajumbe wake mko hapa, halijakaa chini hata siku moja kutafakari hatua ya kuanzisha viwanda vya fenicha na vijiti vya kuchokonoa meno!
Tayari nimekwishatoa maelekezo kuanzia sasa fenicha zote za Serikali zisiagizwe nje tena, naomba niulize; ni nani kati yenu hadi sasa amejiandaa kuchukua nafasi hiyo ya kutengeneza fenicha za hapa kwetu kwa kutumia malighafi zetu, zenye ubora unaotakiwa na Serikali ili Serikali iwe inanunua au kuagiza kutoka kwake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki kuwachosha, sitaki niwapotezee muda wenu. Sisi kama Serikali tutaendelea kujifunza kutoka kwenu, nawashukuruni sana na ninawaomba mzitafakari changamoto chache hizi zinalolikabili Taifa letu.
Mungu awabariki sana, asanteni!