Naomba nianze kwa kutoa taarifa. Jana, baada ya kusoma sehemu ya hotuba yangu ya ukaribisho kwa kugha ya Kiswahili; Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC walifurahi na kuvutiwa sana.

Hivyo basi, tulipokwenda tu kwenye mkutano wetu wa ndani, wote kwa pamoja na kwa kauli moja, walifanya uamuzi wa kukifanya Kiswahili kuwa Lugha Rasmi ya Nne ya SADC. Hii ndiyo sababu nimeamua kuhutubia kwa Kiswahili.

Napenda kutumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza waheshimiwa wakuu wa nchi wenzangu kwa uamuzi huu mkubwa na wa kihistoria, ambao pia unaendana na kumuenzi Baba wa Taifa letu, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Kama mnavyofahamu, wakati wa uongozi wa Mwalimu Nyerere, Tanzania ilifanya kazi kubwa ya kusaidia harakati za ukombozi, hususan wa nchi za Kusini mwa Afrika.  Nchi yetu ilitenga maeneo mengi kwa ajili ya kuanzisha kambi za wapigania uhuru kutoka ANC, FRELIMO, MPLA SWAPO, ZANU-PF, (Nachingwea, Mgagawa, Kongwa, Kaole, Dakawa na Mazimbu), nimefurahi hivi majuzi tu Mheshimiwa Rais Ramaphosa alikwenda kutembelea Mazimbu hivi karibuni. Lakini hata Mheshimiwa Rais Mnangagwa wa Zimbabwe alipokuja alikwenda Bagamoyo (Kaole) ambako alipata mafunzo ya kupigania uhuru.

Tanzania pia, wakati wa uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, ilisaidia kuzuia jaribio la mapinduzi nchini Shelisheli lililopangwa kufanywa na utawala wa makaburu wa Afrika Kusini. Baada ya kuzimwa kwa jaribio hilo, Mtanzania, marehemu Brigredia Jenerali Hassan Ngwilizi, aliongoza nchi hiyo kwa muda. Hii ni mifano michache tu ya mchango uliotolewa na Tanzania chini ya uongozi wa Baba wa Taifa.

Na katika harakati zote hizo, lugha ambayo ilitumika sana ni Kiswahili. Hivyo basi, uamuzi wa kukifanya Kiswahili kuwa Lugha Rasmi ya SADC ni sahihi na muafaka katika kuenzi kazi zilizofanywa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.

 Narudia tena kuwashukuru na kuwapongeza waheshimiwa wakuu wa nchi na serikali kwa uamuzi huu mkubwa na wa kihistoria. Kwa hakika, mmeingia kwenye vitabu vya historia. Vizazi na vizazi vitawakumbuka.

Kama mnavyofahamu, lugha ni chombo muhimu katika kuimarisha mahusiano baina ya watu lakini pia katika kukuza na kuimarisha ushirikiano na utengamano kati na baina ya mataifa. Mwanasosholojia na mtaalamu wa lugha, Dk. Joshua Fishman aliwahi kusema, napenda nimnukuu “…a common indigenous language in the modern nation states is a powerful factor of unity…it promotes a feeling of single community. Additionally, it makes possible the expansion of ideas, economic targets and cultural identity”, mwisho wa kunukuu.

Kiswahili ni lugha ya Kiafrika; na sisi ni Waafrika. Hivyo basi, nina imani kuwa uamuzi huu wa kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya SADC utasaidia kuimarisha uhusiano miongoni mwa wananchi wetu na pia kukuza na kuimarisha ushirikiano na utengamano kati ya mataifa yetu.

Na napenda nitumie fursa hii, kuzisihi nchi wanachama ambazo Kiswahili hakitumiki, kuiga mfano wa Afrika Kusini, ambayo kuanzia mwakani, wataanza kufundisha Kiswahili kwenye shule zao. Sisi Tanzania tutakuwa tayari kuwaunga mkono, ikiwemo kwa kutoa walimu na nyenzo mbalimbali za kufundishia.

Tupo hapa kwa ajili ya kuhitimisha mkutano wetu. Kwa takriban siku mbili, tumekutana kujadili masuala mbalimbali yenye lengo la kuiletea maendeleo jumuiya yetu. Napenda nitumie fursa hii kutamka kuwa, mkutano wetu umekuwa wa mafanikio makubwa sana.

Nasema hivyo, kwa sababu, kwanza, umefanyika kwenye mazingira ya utulivu, upendo, na maeleweno makubwa. Ni kweli, mara chache chache, kulikuwa na kutofautiana kwenye baadhi ya hoja, lakini tulijadiliana kwa urafiki mkubwa na hatimaye kuweza kufikia makubaliano.

Pili, Mkutano wetu ulikuwa wa mafanikio kwa sababu ya ajenda zenyewe tulizozijadili na maazimio tuliyoyafikia. Tumejadili ajenda nyingi na kufikia maamuzi makubwa, ambayo binafsi naamini, endapo yatatekelezwa, yataleta manufaa mengi kwenye Nchi Wanachama pamoja na Jumuiya yetu kwa ujumla.  Naomba, kwa haraka haraka, mniruhusu nitoe muhtasari wa baadhi ya masuala tuliyoyajadili na kuyafanyia maamuzi. 

Kama mnavyofahamu, mkutano wetu umefanyika chini ya kaulimbiu isemayo: “Mazingira Wezeshi ya Biashara kwa ajili ya Kuwezesha Maendeleo Jumuishi na Endelevu ya Viwanda, Kukuza Biashara na Kuongeza Fursa za Ajira (A Conducive Environment for Inclusive and Sustainable Industrial Development, Increased Intra-Regional Trade and Job Creation)”.

Kaulimbiu hii ni mwendelezo wa kaulimbiu za Mikutano ya Wakuu wa Nchi iliyofanyika Zimbabwe mwaka 2014; Botswana mwaka 2015, Eswatini mwaka 2016, Afrika Kusini mwaka 2017 na Namibia mwaka 2018; ambapo zote ziliweka mkazo kwenye utekelezaji wa Mkakati na Mpango Mwongozo wa Maendeleo ya Viwanda wa SADC wa Mwaka 2015 – 2063 (the SADC Industrialization Strategy and Roadmap 2015 – 2063).

Kaulimbiu ya mwaka huu imeweka msisitizo katika kuboresha mazingira ya biashara, ikiwemo kuondoa vikwazo vya mipakani, ukiritimba kwenye maamuzi, rushwa, n.k.; ili kukuza sekta ya viwanda na kustawisha biashara kwenye Ukanda wetu.  Ninayo furaha kuarifu kuwa Wakuu wa Nchi wamepitisha kaulimbi hiyo na kuilekeza Sekretarieti kusimamia utekelezaji wake na kisha kuwasilisha Ripoti kwenye Mkutano ujao wa SADC. Sambamba na hilo, kwa lengo la kukuza sekta ya viwanda kwenye Jumuiya yetu, Mkutano umezihimiza Nchi Wanachama kuendelea kutekeleza Mkakati na Mwongozo wa Maendeleo ya Viwanda wa SADC 2015 – 2063. Na kama mlivyoshuhudia, hivi punde, nchi zetu zimesaini Itifaki kuhusu Viwanda.

Waheshimiwa viongozi, mabibi na mabwana; wakati wa mkutano wetu pia tumepokea Ripoti za Mwaka za Mwenyekiti wa SADC anayemaliza muda wake na Ripoti ya Mwaka ya Mwenyekiti anayemaliza muda wake wa Taasisi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (SADC Organ). Wakuu wa Nchi wamewapongeza wenyeviti hao, Mheshimiwa Rais Geingob na Mheshimiwa Rais Lungu, kwa kazi nzuri walizofanya katika wenye mwaka uliopita.

Wakuu wa Nchi pia wamekubaliana kuendelea kufuatilia suala la usalama nchini DRC; lakini pia wameitaka Falme ya Lesotho kuharakisha utungwaji wa sheria itakayoanzisha Mamlaka ya Kitaifa ya kusimamia Mabadiliko (National Reform Authority). Zaidi ya hapo, Wakuu wa Nchi wameiagiza Sekretarieti kuharakisha Uanzishaji wa Chombo cha SADC cha Kukabiliana na Majanga (SADC Disaster Preparedness and Response Mechanism) kitakachozisaidia nchi wanachama kukabiliana na majanga, kama vile mafuriko, ukame, njaa, vimbunga, magonjwa ya mlipuko, n.k.

Waheshimiwa viongozi, mabibi na mabwana; sambamba na hayo, wakuu wa nchi walipitia hali ya uchumi kwenye ukanda wetu. Na kama ambavyo nilieleza jana, kwa sababu ya majanga mbalimbali yaliyozikumba baadhi ya nchi wanachama pamoja na matatizo mbalimbali ya kiuchumi duniani, uchumi wa ukanda wetu ulishindwa kukua kama ilivyotarajiwa, kwa asilimia 7.0; badala yake ulikua kwa asilimia 3.1.

 Hivyo basi, nchi wanachama zimetakiwa kuendelea kuwekeza kwenye miundombinu na kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji na biashara; kwa kuwa ni mojawapo ya vikwazo vikubwa vya ukuaji wa uchumi barani Afrika, ikiwemo kwenye Ukanda wa SADC. Zaidi ya hapo, tumekubaliana kuendelea kuboresha sera zetu za uchumi na fedha ili kuboresha mazingira ya ukuaji wa uchumi kwenye ukanda wetu.

Waheshimiwa viongozi, mabibi na mabwana; masuala mengine tuliyojadili ni pamoja na suala la upatikanaji mapato (resources mobilization), ombi la Burundi kujiunga na SADC pamoja na suala la vikwazo kwa Zimbabwe.