Ndugu Wananchi,
Leo ni siku ya ambayo Tanzania Bara inatimiza miaka 17 tangu tumejikomboa na ukoloni. Kwa kawaida siku kama ya leo huwa tunafanya Gwaride Rasmi ambalo huwa lina linakaguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano.
Lakini leo hatufanyi hivyo. Hatufanyi sherehe nchini, na wala hatuna hilo Gwaride Rasmi hapa Dar es Salaam, na sababu zake zinajulikana. Tunayo matatizo makubwa. Na hatudhani kwamba katika hali hiyo ya matatizo makubwa ni jambo jema tuwe na sherehe nchini na magwaride ya wanajeshi Dar es Salaam. Kwa kweli hata sina hakika kwamba ni jambo zuri kuwa hivi sisi wengine leo hatufanyi kazi; ni siku ya livu, hatuna kazi. Wenzetu wako kazini; wenzetu wako mpakani, wanafanya kazi na wanalala ndani ya mahandaki. Nasema sina hakika kwamba hata kule kuacha kufanya kazi leo ni jambo jema.
Lakini nilidhani, kwa sababu ya matatizo haya tuliyonayo, ingawa kwa kawaida katika siku kama ya leo huwa sihutubii Taifa, pengine si vibaya nikazungumza kidogo. Nilidhani, pamoja na matatizo yetu haya tuliyonayo sasa hivi, ni vizuri nikaitumia siku hii ya leo kukumbusha maana ya siku ya leo; nieleze maana ya jeuri ya ukoloni, maana ya fidhuli ya ukoloni.
Jeuri ya ukoloni ni jeuri ambayo inazidi jeuri nyingine yoyote duniani. Ni jeuri ambayo, walio nayo jeuri ile, wanakataa usawa wa watu wote. Maana huwezi ukaamua kwamba utawatawala watu wengine wakipenda wasipende, bila kukana usawa wa binadamu. Lazima waseme kwamba watu sio sawa na wewe. Watawala hawa wa kikoloni, na watawala wa namna yoyote hii ya kijahili, lazima waseme kwamba wao si watu, ni miungu wana wajibu wa kuwatawala watu wakipenda wasipende. Ama wataamua kwamba wao watawala (hawa wa nguvu) wao ndio watu, na wale wanaotawaliwa sio watu, ni wanyama tu.
Mimi nilikuwa bado mwanafunzi shuleni niliposoma filosofia ya mheshimiwa mmoja kiongozi wa Wajerumani, anaitwa Hitler. Hitler alikuwa anawachukia sana Wayahudi, na katika maisha yake aliua Wayahudi wengi sana. Alikuwa hasa na shabaha ya kuwafuta kabisa duniani, waishe. Alikuwa anawakusanya na anawapeleka katika matanuri makubwa; halafu nafunga milango nafungulia gesi, na Wayahudi wanakufa humo ndani. Na Hitler aliua Wayahudi milioni sita.
Na mmoja katika madhambi ya Wayahudi, walikuwa na madhambi mengi lakini moja wapo ya madhambi ya Wayahudi, Hitler anasema, ni kwamba walikuwa wanahubiri usawa wa binadamu. Wanasema binadamu ni sawa; na Hitler hakubali kwamba binadamu ni sawa. Anasema, kwa mfano Wayahudi hawa magazeti yao yanasema kwamba watu weusi na watu weupe ni sawa.
Na mifano yao ni nini? Mfano ni kwamba inawezekana yako mashindano, ya mbio ama ya ngumi. Halafu mtu mweusi anaweza akakimbia akamzidi mtu mweupe. Basi magazeti haya ya Wayahudi yanasema kwamba, watu weusi hawa ni sawa na watu weupe, au wanazidi; maana unaona wanaweza kuwazidi mbio au wanaweza kupiga ngumi.
Hitler anasema ujinga gani huu! Binadamu na manyama hawawezi akashindana katika mbio au ngumi, na hawa weusi wamewashinda hawa kwa sababu wao ni wanyama; wanaweza sana mbio zaidi. Badala ya kusema hivyo hawa wanapotosha Taifa letu la wateule, kusema kwamba watu weusi na watu weupe ni sawa. Ama anasema kwamba magazeti haya ya Kiyahudi yanatoa ushahidi mwingine wa ovyo wa usawa. Wanasema weusi fulani wamekwenda katika Vyuo Vikuu na huko wamesoma na wamehitimu, wamepata shahada sawa sawa na watu weupe, au hata wamezidi. Kwa hiyo Wayahudi hawa wanasema watu weusi ni sawa na weupe. Anasema badala ya kusema kwamba watu weupe ni watu wa ajabu kweli, wanaweza kufundisha nusu manyani hawa wakafanya mambo ya kibanadamu, wanapotosha Taifa letu teule kusema kwamba nusu nyani hawa sawasawa na binadamu!
Hiyo ndiyo jeuri ya watu kama kina Hitler, kutoamini usawa wa binadamu. Na Hitler hakutaka kuishia hapo. Alikuwa anaamini watu weupe hao wako weupe walio bora zaidi kuliko weupe wengine. Wenzao hawa wa Afrika ya Kusini, hawa akina Voster, hawakupigana vita vile vya Hitler; walikataa kwa sababu imani yao ni ile ile. Walikuwa jela wakati wote wa vita vile vya kupinga Hitler; wao walikataa kabisa kumpiga Hitler sababu ya imani yao ni ile ile. Na hawa wanaamini kabisa, kwa Msahafu, kwamba ndiyo Mwenyezi Mungu alivyofanya; ameumba watu weupe kuwa bora zaidi kuliko watu weusi, na kwa hiyo lazima watu weusi watawaliwe na watu weupe.
Nasema jeuri ya ukoloni au ya utumwa, au ya ujahili ni hiyo ama ya kujifanya miungu , ama ya kufanya binadamu wengine kuwa ni wanyama. Na jeuri ya namna hiyo, ninasema, inazidi jeuri nyingine yoyote duniani. Na inapotokea akili ya binadamu iliyokomaa inakataa; inakataa kabisa kukubali! Kwa hiyo lazima mpambane nayo jeuri hiyo popote inapotokea. Sasa ilitokea kwetu. Rafiki zetu Waingereza hawa, ingawa wao hakupenda kutawaliwa na akina Hilter , wao walidhani wana haki kutawala sana duniani. Watu wachache Waingereza wajidai wanakwenda kutawala Wahindi. Wahindi ni wengi sana. Lakini jeuri hii ya kwamba wao ni bora zaidi kuliko watu wengine ikawafanya Waingereza hawa wathubutu hata kwenda kuwatawala Wahindi na sisi pia; na wote tukawa chini ya himaya hiyo ya Kiingereza. Lakini hawakukubali: na mahali popote walipokuwa wanawatawala, watu hawakukubali. Wakafanya jitihada mpaka akajitawala. Akili ya binadamu aliyekomaa inakataa, na lazima uipinge mpaka ujitawale.
Sasa tumeipinga na tukajitawala. Hivi leo tunaadhimisha huko kukataa kwetu kutawaliwa na watu wengine ambao wanajidai kwamba labda wao ni bora zaidi kuliko binadamu wenzao. Basi tumepata uhuru wetu. Na baada ya kupata uhuru wetu tumetangaza; tumesema nini shabaha yetu tukiwa nchi huru. Na shabaha zetu tumesema ni mbili.
Moja ni kutumia uhuru wetu katika jitihada ya kuwaendeleza wananchi; kuvunja yale makovu yaliyofanywa na ukoloni, kujenga heshima ya wananchi wetu, kuleta maendeleo. Na tukasema maana ya maendeleo kwetu ni kila litakalosaidia kuleta heshima ya Mtanzania. Kila kitendo kitakachoweza kumrudishia ubinadamu wake Mwafrika, ubinadamu uliokuwa umevurugwa- vurugwa na matope ya ukoloni, sisi tutakiheshimu kukifanya kwamba ni kitendo cha maendeleo. Hivyo ndiyo jitihada yetu ya kwanza. Lakini shabaha yetu ya pili ilikuwa ni kusaidia wenzetu nao katika Afrika ambao hawajajikomboa, hawajafikia hatua hii ambayo sisi tumeifikia, na wao wajikomboe.’
Kwa hiyo tumekuwa tunazo shabaha hizi mbili, ya maendeleo ya nchi yetu, kuendeleza uhuru wetu na maana ya uhuru, na kuwasaidia wenzetu ao katika Afrika ajipatie uhuru wao. Hatuna uwezo mkubwa sisi, uwezo wetu ni mdogo; na uwezo wa kuwasaidia ndugu zetu wajikomboe nao ni mdogo.
Lakini dunia inajua, na Afrika inajua kwamba pamoja na udogo wa uwezo wetu, tumefanya jitihada za dhati kuzitekeleza shahada hizo mbili; kuleta maendeleo kwa wananchi wetu, na kuwasaidia wenzetu kujikomboa. Nasema dunia inajua, na Afrika inajua, kwamba pamoja na udogo wetu na unyonge wetu, lakini shabaha hizo tumejitahidi kuzitekeleza kwa dhati.
Na uhusiano wetu na nchi za nje unategemea sana msimamo wao katika shabaha zetu hizo mbili. Hatukupata kugombana na nchi yoyote kwa sababu hautusadii kuleta maendeleo katika nchi yetu; hata mara moja. Kuleta maendeleo maendeleo katika nchi yetu, tumesema, ni jukumu letu, na hatuwezi kugombana na mtu mwingine kwa sababu eti hatusaidii; hata kidogo. Hatujapata kugombana na nchi yoyote kwa sababu haitusadii sisi au hawasaidii wenzetu katika jitihada ya kuleta ukombozi katika Bara la Afrika; hata kidogo. Kwa sababu tumesema jukumu la ukombozi wetu, ni letu sisi Waafrika wenyewe.
Lakini tumegombana. Tumegombana na nchi ambazo tumeamini zinatuingilia sisi katika kuleta maendeleo yetu katika nchi yetu. Hatukugombana na nchi kwa sababu haitusaidii; lakini tumegombana na nchi ambazo tumeamini kwamba zinatungilia katika maendeleo yetu. Zinatuwekea vipingamizi, zinatuvurugia mipango yetu, ama ya kuleta maendeleo katika nchi yetu, ama kuwasaidia wenzetu katika ukombozi wao. Tumegombana nazo, nyingine nchi kubwa kubwa tumegombana nazo. Tuliwahi kuvunja uhusiano na Waingereza, tuliwahi kugombana na Wajerumani, tulitaka kugombana na Marekani kwa sababu ya msimamo wao katika shabaha zetu mbili hizo; moja, maendeleo ya nchi yetu wenywe hapa, na pili, ukombozi wa Bara la Afrika. Lakini hata mara moja hatukuwahi kugombana na na nchi za Kiafrika; hata mara moja.