Hospitali kubwa zaidi ya rufaa ya umma nchini Kenya imetangaza kuwa itazika mamia ya miili ambayo haijachukuliwa na jamaa wao iliyopo katika chumba chake cha kuhifadhi maiti ikiwa wanafamilia hawataichukua.
“Wananchi wanaombwa kutambua na kuchukua miili hiyo ndani ya siku saba, vinginevyo, hospitali itatafuta mamlaka kutoka kwa mahakama kuizika,” Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) ilisema Jumanne katika notisi iliyochapishwa katika gazeti la kibinafsi la The Star.
Miili hiyo 541 ni pamoja na watoto 475 na watu wazima 66.
Hospitali ilichapisha majina ya marehemu, lakini miili michache bado haijatambuliwa na jamaa wao.
KNH na hospitali zingine za umma na vyumba vya kuhifadhia maiti nchini Kenya mara kwa mara hutoa notisi kwa jamaa kuchukua miili ambayo haijachukuliwa.
Miili ambayo husalia bila kuchukuliwa baada ya kipindi kilichowekwa mara nyingi huzikwa kwenye makaburi ya halaiki.
Kwa kawaida miili hiyo ni ya wagonjwa wanaofia hospitalini bila familia zao kujua.
Baadhi ya familia pia huchagua kutochukua miili ya wapendwa wao katika vyumba vya kuhifadhia maiti wakiwa hawana uwezo wa kulipa gharama zao za hospitali au chumba cha kuhifadhi maiti.