Serikali imeaanza mipango ya kuipandisha Hospitali Kuu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Lugalo, kuwa Hospitali ya Rufaa, Bunge limeelezwa.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, amesema uamuzi huo wa Serikali umelenga kupanua utoaji huduma kwa wananchi.
Hospitali Kuu ya Lugalo imekuwa tegemeo na kimbilio la makabwela wengi hasa wakati wa mgomo wa madaktari katika hospitali za umma.
Pinda ametangaza uamuzi huo alipokuwa akijibu swali la papo kwa papo kutoka kwa Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mwangungu (CCM).
Katika swali lake, pamoja na mambo mengine, Mwangungu alitaka kujua mikakati ya Serikali katika kuhakikisha kuwa huduma za afya zinaimarishwa nchini.
Waziri Mkuu amesema Serikali imekuwa ikijitahidi kadri ya uwezo wake kuboresga huduma, na akatoa mfano wa ufunguzi wa kitengo cha huduma ya matibabu ya moyo katika Hospitali ya Taifa Muhimbi (MNH) ambao unatarajiwa kufanywa hivi karibuni.
Pia amesema kitengo cha meno katika hospitali hiyo kubwa kuliko zote nchini, kimeboreshwa kwa vifaa na huduma za kisasa.
Kwa upande wa Taasisi ya Saratani Ocean Road , amesema juhudi zinaendelea ili kuifanya iendelee kutoa huduma za kiwango cha juu, ikiwa ni pamoja na kuboresha majengo, vifaa na malazi.
Pinda amerejea wito wa Serikali kwa madaktari, wauguzi, wafamasia na wafanyakazi wengine wa afya kutambua dhamana kubwa waliyonayo kwa afya na uhai wa Watanzania.
Jina la Tanzania halijachafuka
Waziri Mkuu amepinga madai ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, aliyesema matukio ya watu kutekwa, kuteswa na hata kuuawa, yamechafua taswira ya Tanzania mbele ya jumuiya ya kimataifa.
Mbowe alijenga hoja ya madai yake kutokana na tukio la hivi karibuni la kutekwa na kupigwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania , Dk. Steven Ulimboka.
“Sikubaliani na Mbowe eti jina la nchi yetu limechafuka sana . Kuchafuka kwa lipi?” Alihoji.
Amesema bado hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa Dk. Ulimboka ametekwa na kupigwa na vyombo vya dola.
“Hadi sasa hakuna mwenye ushahidi, ni vizuri tukasubiri uchunguzi,” amesema.
Amesema kwa muda wote wa matatizo ya madaktari Serikali imeshirikiana na Dk. Ulimboka kupata suluhu, na kwamba haiwezekani mtu ambaye Serikali ilimtarajia kufanikisha suluhu hiyo, atekwe na kupigwa na vyombo vya Serikali.
“Haiingii akili, tufanye kazi vizuri, sisi hao hao tumteke na kumpiga, haiingii akilini,” amesema.
Bei ya vyakula wakati wa Mwezi Mtukufu
Waziri Mkuu ametoa wito kwa wafanyabiashara kuacha kupandisha bei za vyakula wakati wa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Rai ya Pinda imetokana na swali la Mbunge wa Ole, Rajab Mbarouk Mohammed (CUF) aliyetaka kujua namna Serikali itakavyoshiriki kudhibiti mfumko wa bei za vyakula kwa wakati huo.
Pinda amesema, “Tuache kutaka utajiri kwa njia zisizo halali, tusitumie mwanya huo (wa mfungo) kujitajirisha. Serikali tutachukua hatua stahiki.”