Na Muhidin Amri, JamhuriMedia, Ruvuma
Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Hospitali ya Wilaya Tunduru mkoani Ruvuma,imeanza kampeni ya kuwapima maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu watoto wadogo kupitia haja kubwa kutokana na watoto hao kutokuwa na uwezo wa kutoa sampuli za makohozi na kwa ajili ya vipimo kama ilivyo kwa watu wazima.
Hayo yasemwa na mratibu wa ugonjwa wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongle, wakati wa kampeni za uelimishaji na uchunguzi wa kifua kikuu kwa wanawake wenye watoto walio chini ya umri wa miaka mitano zilizofanyika kata ya Nanyoka wilayani humo.
Dkt Kihongole amesema,kutokana na ukubwa wa tatizo la kifua kikuu wilayani humo,wameanza kutoa elimu ya Tb kwa akina mama kwa kuwa watoto wadogo ni kundi linalo sahaulika na wanafikishwa kwenye vituo vya kutolea huduma za matibabu baada ya kuzidiwa.
Amesema,uchunguzi wa TB kupitia mfumo wa haja kubwa kwa watoto wadogo umeonyesha mafanikio makubwa,kwa kuwa watoto uwa wanashindwa kutoa makohozi kwa haraka ili kufanyiwa uchunguzi wa kitaalam.
“Kama mtoto amembukizwa ugonjwa huo ni dhahiri umetoka kwa wazazi au jamii inayowazunguka,hivyo kupitia elimu hii na uchunguzi kwa watoto tuna matumaini ya kuwapata hata watu wazima walioambukizwa ugonjwa huo ambao wako majumbani” alisema Kihongole.
Aidha alisema,jumla ya watu 53 wamebainika kuwa na maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu baada ya kufanyiwa uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa huo kwa njia ya makohozi.
Alieleza kuwa,watu hao wamekutwa na TB kupitia kampeni zilizofanyika katika maeneo mbalimbali kati ya mwezi Oktoba na Novemba mwaka huu za kuwaibua watu walioambukizwa ugonjwa huo ili waweze kuanzishiwa matibabu.
Dkt Kihongole ambaye ni mratibu wa tiba asili na tiba mbadala,ameitaka jamii kuhakikisha inajitokeza kwenye kampeni hizo ili kujua hali ya afya zao na watakaobainika watapata matibabu bure kwenye zahanati,vituo vya afya na Hospitali zote hapa nchini.
Beatrice Kiloha mkazi wa mtaa wa National wilayani humo,ameiomba serikali kufikisha elimu ya kifua kikuu kwa wananchi wengi zaidi kwani itasaidia jamii kupata uelewa kuhusu ugonjwa huo,dalili zake na namna ya kujikinga.
Alisema,katika jamii zetu wapo wagonjwa wa kifua kikuu ambao hawajaanza matibabu,lakini kutokana na kukosa elimu hasa madhara ya ugonjwa huo wanaendelea kuishi nao majumbani jambo ambalo ni hatari.
Fatma Rajabu,amefurahishwa na hatua ya Hospitali ya wilaya Tunduru kutoa elimu ya kifua kikuu,hata hivyo ameshauri elimu hiyo ifike kwa madereva wa mabasi ya mikoani kwani baadhi yao wanazuia abiria kufungua madirisha ya magari.
Fatma alisema,ugonjwa wa kifua kikuu unaambikizwa kwa haraka kupitia mfumo wa hewa hivyo ni rahisi mtu mwenye ugonjwa huo kuambukiza wengine anapopiga chafya au kukohoa bila kuchukua tahadhari kama madirisha ya gari yatafungwa kwa bila kuruhusu kuingia hewa.
…………………………………………………
Baadhi ya akina mama wa kata ya Nanyoka wilayani Tunduru,wakimsikiliza mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya hiyo Dkt Mkasange Kihongole(hayupo pichani)wakati wa kampeni ya uchunguzi wa ugonjwa huo kwa watoto kupitia haja kubwa.
Mratibu wa ugonjwa wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Dkt Mkasange Kihongole akitoa elimu ya kifua kikuu kwa akina mama wenye watoto wadogo kabla ya kuanza kwa kampeni ya uchunguzi wa ugonjwa huo kwa watoto kupitia haja kubwa