UJENZI wa hospitali ya Halmashauri ya Madaba Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma upo katika hatua za umaliziaji.
Mkuu wa Wilaya ya Songea Mheshimiwa Pololet Mgema amesema serikali imetoa shilingi bilioni 2.9 kutekeleza mradi huu ambao utawezesha kutoa huduma zote muhimu za matibabu.
Amesema hadi sasa zimetumika shilingi bilioni 2.2 kujenga majengo mbalimbali katika hospitali hiyo na kwamba serikali tayari imeleta shilingi milioni 700 ili kujenga wodi tatu ambazo ni za wanawake,watoto na wanaume pamoja na nyumba ya maiti.
“Wananchi walikuwa wanasafiri zaidi ya kilometa 120 kutoka Madaba hadi Songea kufuata huduma za matibabu katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa ,lakini sasa huduma zote muhimu zitatolewa hapa Madaba “,alisema Mgema.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Madaba Sajidu Idrisa Mohamed amesema tayari vifaa muhimu vya hospitali kama X-ray iliyogharimu shilingi milioni 350 imeshafungwa katika hospitali hiyo na kwamba kinachoendelea hivi sasa ni kufunga milango na kazi ndogo ndogo za ukamilishaji ili huduma za afya zianze kutolewa.
Halmashauri ya Madaba ni miongoni mwa Halmashauri tatu zinazounda Wilaya ya Songea.