Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, amefanya jambo lenye manufaa makubwa kwa wanafunzi wa kike jimboni mwake na kwa taifa.
Amesimamia ujenzi wa mabweni ya wasichana katika Shule ya Sekondari Mboga, iliyopo Kata ya Msoga mkoani Pwani. Amesukumwa na azima yake ya kuona mtoto wa kike anasoma kwa bidii katika mazingira mazuri ili afikie ndoto alizojiwekea.
Tumeambiwa kuwa mabweni hayo yatahifadhi wanafunzi zaidi ya 200. Mafanikio hayo yatawasaidia wanafunzi wanaoteseka kwa kusafiri umbali mrefu kwenda kusaka elimu.
Ridhiwani anasema wanafunzi wa kike wamekuwa wakikutana na changamoto nyingi, ikiwamo ya kutiwa mimba, hivyo kukatisha masomo. Anaamini kwa mabweni hayo hata ufaulu utaongezeka.
Jambo la kufurahisha ni kusikia kuwa mabweni hayo yamejengwa kwa fedha za halmashauri na msaada wa wadau wa elimu wilayani Chalinze. Kwa wavulana, ujenzi wa mabweni yao umeshaanza. Muhimu ilikuwa kuanza na ya wasichana, kwa sababu wao ndio walio kwenye hatari kubwa ya kuharibiwa maisha.
Nampongeza Ridhiwani kwa dhati kabisa, nikitambua kuwa kazi anayoifanya ina manufaa makubwa, si kwa Chalinze pekee, bali kwa taifa zima. Historia ya nchi yetu inabebwa na watu wa aina hii ya Chalinze ambao mbunge wao ameamua kuwasaidia. Watoto wa maskini wamekuwa na manufaa makubwa kwa nchi.
Nimesafiri katika barabara kuu zote nchini mwetu. Sidhani kama kuna wilaya ambayo sijatia mguu. Kote huko kitu tunachoweza kukiona mara moja ni shida wanazopata wanafunzi wakati wa kwenda na kutoka shuleni. Wanateseka kweli kweli.
Mwaka jana niliwapa lifti wanafunzi saba mkoani Singida. Ilikuwa jioni. Nikastaajabu waliponieleza kuwa muda ule kama wangekosa lifti, wangerejea kulala madarasani. Wapi wanapata chakula? Mungu tu anajua. Wanatembea kilometa 17 kwenda na kutoka shuleni.
Hali ni hiyo hiyo katika maeneo mengi nchini mwetu. Wanafunzi wanaamka saa 9 alfajiri! Wanatembea umbali mrefu wakiwa wanakabiliwa na mazingira magumu. Hawa hawawezi kusoma na kufaulu.
Mara kadhaa wameomba lifti kutoka kwa madereva, hasa wa malori. Si madereva wote wenye uungwana au huruma. Wanawaona watoto wa kike kama viumbe dhaifu, walio tayari kuingia mtegoni kutokana na udhaifu wao.
Mtoto wa kike ambaye anatoka nyumbani bila kuwa na shilingi kwenye mkoba wake, anapokumbana na dereva jahili akampa Sh 2,000 si rahisi kuzikataa, pia kuyakataa maelekezo au amri atakayopewa. Wapo madereva wa malori wanaowapa simu, tena zile za bei ndogo – hata kama ni za Sh 20,000 – kwa lengo la kuwasiliana. Watoto wengi wa kike wameingia kwenye mitego si kwa kupenda, bali kutokana na shida zinazowakabili.
Matokeo ya haya yamekuwa mabaya. Wapo waliokatizwa masomo kwa kutiwa mimba. Wapo waliohadaiwa na kuyakimbia masomo kwa ahadi ya kupewa maisha mazuri mijini. Wapo walioambukizwa maradhi kwa sababu hata matumizi ya kinga watoto wengi wa kike huwa hawana hiari.
Pamoja na madereva wa malori, wapo madereva wa bodaboda. Hawa tunawaona hata mijini tunakoishi. Hawawaoni kina mama watu wazima, bali watoto wadogo – wanafunzi! Wapo waliowaahidi usafiri kila wanapokwenda au kutoka shuleni kwa ujira wa ngono. Madhara yamekuwa yale yale kama wanayopata kutoka kwa madereva wa malori.
Watoto wa kile hawako salama. Wale wanaoona shida kuhangaikia usafiri kila mara wamepanga katika nyumba binafsi karibu na shule.
Huko walikopanga mambo ni mabaya. Wengi wamekuwa hawapati mahitaji muhimu; hali inayowafanya waangukie mikononi mwa wakwale. Hao huwapa huduma ndogo ndogo lakini za lazima. Uhusiano hukoma pindi binti akitiwa mimba, akiugua au akichokwa! Wengi wameingia kwenye madanguro.
Hayaishii hapo. Wapo ambao kwa sababu ya utoto au kutojua, huamua kuishi kinyumba na wavulana wanafunzi. Hawa huwa mke na mume. Mara nyingi wavulana wanaofanya hivyo ni wale wanaotoka kwenye familia ambazo walau zina uwezo kidogo. Wengine ni wavulana ambao hutumia muda fulani kwenda kusaka fedha kwa namna yoyote wanayoweza.
Ujumla wa yote haya ni janga kwa watoto wa kike katika taifa letu. Wao ndio wanaokatishwa masomo kwa wingi kila mwaka. Wao ndio wanaotiwa mimba na kujikuta wakipata shida kulea watoto.
Tunaona umaskini ukiongezeka katika familia. Mzazi maskini aliyetarajia mtoto wake asome ili walau amsaidie siku za usoni [kosa letu Waafrika], anajikuta akilazimika kulea wajukuu ilhali yeye mwenyewe ni hohe hahe. Umaskini unakuwa juu ya umaskini.
Bahati mbaya wale wanaoshiriki kuleta matokeo haya mabaya (watia mimba) hawapati adhabu zinazolingana na za kukatisha masomo watoto wa kike.
Kwa kuyatambua haya na mengine ya aina yake, nashawishika kutoa mwito kwa viongozi aina ya Ridhiwani kujitokeza kwa wingi kuona namna bora ya kuwaokoa watoto wa kike. Hili la kujenga mabweni halina budi kupewa kipaumbele kwa majimbo yote.
Zipo changamoto zinazotokana na shule za mabweni. Changamoto kuu bila shaka ni chakula na huduma nyingine za kijamii kwa wanafunzi. Hili ni changamoto kwa sababu tumeamua liwe changamoto. Sasa tulikatae. Tanzania yenye ardhi nzuri ya kilimo haiwezi kuwa nchi ya kukosa chakula cha kuwalisha watoto mabwenini.
Tunayo mabonde mazuri yanayostawi kila aina ya mazao ya chakula, matunda, mbogamboga na kadhalika. Tuna Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambalo moja ya kazi zake kubwa ni uzalishaji. Tunalo Jeshi la Magereza ambalo likitumiwa vizuri linaweza kuwa na mashamba yenye ukubwa wa kukidhi mahitaji ya nchi. Tunachokosa kwenye hili suala la chakula ni utashi tu. Tukiamua, chakula hakiwezi kuwa “changamoto” nchini mwetu.
Adha wanazopata watoto ni nyingi na kubwa kweli kweli. Wanateseka ilhali uwezo wa kuwaondolea mateso hayo tunao.
Kama la mabweni haliwezekani, basi tuangalie uwezekano wa kujenga shule nyingi za sekondari katika mitaa, vijiji na kata zetu. Tuhakikishe shule zinakuwa karibu na wanafunzi. Tuamue kisera kuwa umbali fulani ndio uwe wa mwanafunzi kutoka nyumbani na kufika shuleni. Tuwe na umbali “elekezi”.
Haya yatawezekana tu endapo suala la elimu kwa watoto wetu tutalichukulia na kulikubali kuwa ni letu wazazi, walezi na wadau wengine. Dhana ya kwamba kazi ya kusomesha watoto ni ya serikali ni mbaya, na kwa kweli ndiyo inayotufanya tufeli. Dhima ya kwanza ya kusomesha ni ya mzazi.
Hakuna namna yoyote ambayo wazazi na walezi wanaweza kukaa kando halafu tutarajie matokeo chanya kwenye elimu. Sidhani kama mpango wa elimu bure ulilenga kutufanya “tususe” kuchangia elimu.
Viongozi aina ya Ridhiwani wala hawataweza wao wenyewe kufanikisha suala hili la uboreshaji elimu. Na kwa mantiki hiyo, ndiyo tutaona umuhimu wa kuketi pamoja tukiwa taifa moja kwa ajili ya kupanga na kuamua mustakabali wa elimu katika nchi yetu.
Hili lihusu miundombinu ya shule na vyuo, lihusu mitaala inayoendana na ulimwengu wa leo na ujao ambao unakwenda kwa kasi kubwa sana. Lihusu aina ya elimu tunayotaka watoto wetu maelfu kwa maelfu waipate. Tujadili tuone kama ni jambo la heri kweli kutenga fedha nyingi kwa ajili ya mikopo ya vyuo vikuu badala ya VETA.
Haya na mengine yanayohusu elimu katika nchi yetu si mambo ya kuamuliwa na mtu au kikundi cha watu. Hili ni jambo la kuamuliwa na nchi nzima.
Nihitimishe kwa kumpongeza Ridhiwani na wabunge wengine waliotambua umuhimu wa kusaidia kujenga mabweni kwa lengo kuu la kuwakomboa watoto wetu wa kike. Mungu awabariki sana.