Wiki iliyopita, Rais John Magufuli alipokea ndege aina ya Bombardier Q400 yenye uwezo wa kubeba abiria 70, ikitokea nchini Canada.
Katika hafla hiyo, Rais Magufuli akawataka Watanzania kujivunia ndege hiyo ya tatu ikiwa ni miongoni mwa ndege sita alizoahi kuzinunua.
Pia Rais Magufuli alizindua ukuta wenye urefu wa kilomita 24.5 uliojengwa kuzunguka eneo lenye madini ya Tanzanite lililopo Mirerani mkoani Manyara.
Kwenye hafla zote hizo, Rais Magufuli na viongozi wengine wa Serikali walizungumzia mambo tofauti yanayohusu mikakati yenye kuchagiza kasi ya maendeleo na kustawisha maisha ya watu.
Sisi wa JAMHURI tunampongeza Rais Magufuli kwa kufanikisha miradi hiyo iliyo kati ya mikubwa inayotekelezwa na Serikali yake.
Ununuzi wa ndege, pamoja na changamoto zilizojitokeza ni hatua nzuri itakayosaidia kuboresha usafiri wa anga, kutoa ajira na kurahisisha ama kuongeza shughuli za utalii nchini.
Kwa muda mrefu sasa, Tanzania imeshuhudia mashirika ya ndege katika nchi mbalimbali zikiwamo zilizo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, yakiimarika na kuchangia kukuza uchumi wao.
Nchi kama Kenya na Rwanda zimejiimarisha katika sekta ya anga. Kwa upande wa Tanzania, Shirika la ndege limekuwa likidorora siku kwa siku na hatimaye kuliondoa katika ushindani katika sekta ya anga.
Hivyo Rais Magufuli anaposimamia na kutekeleza miradi inayoonesha mafanikio yatakayoifikisha nchi katika ushindani wa sekta ya usafiri wa anga, ikiwamo ununuzi wa ndege kama iliyoingia nchini wiki iliyopita, halipaswi kuwa jambo la kubezwa.
Kwa upande mwingine tunatambua na kupongeza ujenzi wa ukuta kule Mirerani, ikiwa ni sehemu ya udhibiti wa utoroshwaji na hujuma kwa madini ya Tanzanite.
Tanzanite ni moja ya rasilimali ambazo kwa muda mrefu, Watanzania wamepaza sauti dhidi ya utoroshwaji wake, na hujuma nyingine zinazosababisha nchi isinufaike, yakanufaika mataifa mengine.
Ingawa kukamilika na kuwapo kwa ukuta huo ni sehemu ya mahitaji mengi katika usimamizi na ulinzi wa rasilimali hiyo, bado Rais Magufuli anastahili pongezi kwa kulifanikisha jambo hilo.
JAMHURI tunatambua kuwa zaidi ya ndege ya Bombardier Q400 na ujenzi wa ukuta wa Mirerani, ipo miradi mingine mikubwa inayotekelezwa na Serikali yake.
Lakini kwa haya yaliyofanyika wiki iliyopita na ambayo ni kielelezo cha utekelezaji wa ahadi zake, Rais Magufuli ‘anajifunua’ kwa kuwa mtekelezaji wa vitendo kwa ahadi anazozitoa, na hivyo anastahili pongezi.