Wiki iliyopita, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi Simon Sirro, amepiga marufuku uuzaji wa silaha za jadi hadharani. 

Silaha za jadi zilizozuiwa kuuzwa hadharani ni pamoja na mapanga, pinde, mikuki, manati, majambia na visu. Kwa muda sasa vifaa hivi vimekuwa vikiuzwa barabarani na wamachinga hasa katika maeneo ya mataa kwa Jiji la Dar es Salaam.

Sirro amesema Januari 12, mwaka huu, Jeshi la Polisi limemkamata Mgoli Sakalani (39) kwa kosa la kuuza silaha za jadi. Amesema Sakalani na wengine watakaokamatwa wakiuza silaha hizo watafikishwa mahakamani. Ameeleza sababu ya kuzuia silaha hizi kuwa ni matumizi mabaya yanayofanywa na wauzaji hasa nyakati za usiku kwani silaha hizo wanazitumia kupora watu mbalimbali.

Sisi wa JAMHURI tunapenda kuchukua fursa hii kulipongeza Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kwa kuona hatari hii na kuchukua hatua mapema. Tunaamini tishio la amani kwa silaha hizi kuuzwa hadharani halipo Dar es Salaam pekee, bali nchi nzima. Vitu vyote vyenye ncha kali visiruhusiwe kuuzwa hadharani vikiwamo visu.

Kwa nchi zilizoendelea kama Uingereza, ni takwa la kisheria kuwa mtu asibebe kitu chochote chenye ncha kali chenye urefu wa zaidi ya inchi moja na nusu. Walifikia hatua hiyo baada ya kubaini kuwa vijana walikuwa wakitumia visu kuchomana. Haya tumeyashuhudia Morogoro wakati mfugaji alipomchoma mkuki kinywani ndugu Agustino Pius, mkazi wa Kijiji cha Dodoma Isanga, Tarafa ya Masanze, wilayani Kilosa.

Ni kutokana na hali hii tunaamini wakati umefika sasa kwa nchi yetu kuzuia watu kumiliki silaha za jadi holela. Ikibiti tupige hatua mbele na kuanzisha usajili wa silaha za jadi kama mapanga na visu sawa na zinavyosajiliwa bunduki. Sisi tunaamini si kila Mtanzania anahitaji panga au kisu, kwani kwa sasa watu wengi wanapikia gesi hivyo hawatumii mapanga kukatia kuni.

Kitendo cha kuuza mapanga hadharani kinaweza kuwa kishawishi cha hatari ambacho mbele ya safari wachochezi wanaweza kuhamasisha wananchi kupambana wao kwa wao na yakatumika. Tunasema hata maduka yatakayopewa leseni za kuuza silaha hizi, ni bora yawe na uratibu wa kusajili nani ananunua panga au kisu na orodha hii itunzwe kwa nia ya kuimarisha usalama.

Kwa mara nyingine tunapenda kulipongeza Jeshi la Polisi kwa kuimarisha usalama katika eneo hili kutokana na kudhibiti uuzaji holela wa silaha za jadi, na pia kurejesha utaratibu wa kufungua vituo vidogo vya polisi kwa muda wa saa 24, hali tunayoamini itaimarisha usalama wa nchi yetu.