Napata wakati mgumu. Napata shida jinsi ya kuanza makaha haya. Napata shida si kwa sababu nina maslahi binafsi, bali kwa sababu nakumbuka hadithi ya mwanafunzi aliyebeba upodo huku akijifunza kurusha mishale ya sumu. Hakuwa mahiri na hakujua jinsi ya kuvuta upinde. Kwa kicheko kikubwa, aliipaka sumu ncha ya mshale, upinde akauelekeza karibu na tumbo lake, kamba ya kurushia mshale ikatokea mbele yake. Bila kujua kijana huyu, akaweka mshale ukielekea tumboni kwake. Kisha akaanza kutanua kamba akivuta na kumwambia adui yake ‘Sali sala ya mwisho kwani utakoma ubishi kuingilia kambo yasiyokuhusu.’ Kwa adui kuona tukio lile, moyo wake ukapata ganzi. Akajiuliza kijana anamaanisha nini. Huku wakati kijana akiendelea na mbwembwe kwa kuwa alikwishavuta kamba kitambo, jasho taratibu lilianza kutoka katika vidole vilivyoshikilia kifundo. Kwa bahati mbaya mshale ukamporochoka. Ncha ya mshale ilikuwa imepakwa sumu ya nyoka aina ya swila (cobra). Sitaki kusimulia kilichotokea mara mshale ulipoanza safari.
Sina uhakika kama Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika hili la aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu, na Ofisa Utawala wa ubalozi huo, Grace Martin, waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya euro milioni 2 kama Kikwete alikuwa anajifunza kurusha mishale huku akiwa amebeba upodo au la.
Nimeshuhudia kesi kadhaa za aina hii mahakamani – si kwa kukurupuka bali kwa malengo maalum – Serikali ya Rais Jakaya Kikwete imezipeleka mahakamani. Sitaki kuamini na wala sitakaa niamini, iwapo kauli anayoitoa Rais Kikwete mara kwa mara kuwa wanasheria wetu bado hawana utaalamu wa kutosha kama ina ukweli. Kama anajua hawana utalaamu si turejeshe Wazungu tu wafanye kazi kwa muda hadi tutakapopata utaalamu?
Sitazungumzia kesi nyingine zilizopo mahakamani kwa hofu ya kusingiziwa kuwa nimeingilia uhuru wa mahakama, lakini hili ya Balozi Mahalu kwa kuwa imemalizika nia kila chembe ya uhuru kuitania.
Sitanii, wapo wanaoweza kushangaa kwa nini nimeanza makala yangu kwa kumwelekea Kikwete moja kwa moja. Niliandika siku nyingi kabla ya kuanzisha gazeti langu kuwa kesi hizi zilizofunguliwa kwa shinikizo la kufurahisha wafadhili kuonyesha kuwa serikali mpya inachapa kazi, zitaishia kuwa aibu kwa Serikali.
Wala nilikuwa sifanyi kazi ya Sheikh Yahya Hussein ya kutabiri nyota. Pamoja na kwamba wakati huo sikuwa nimeanza masomo ya sheria, nilikuwa nasoma sheria zilizopo, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) na kubaini kuwa tunapigwa changa la macho.
Niliyasema haya katika suala la Richmond na Dowans, bila soni watu wakaninyooshea kidole kuwa nimehongwa. Kwa bahati wakati nasoma sheria nimekutana na somo la Sheria ya Mikataba moyo wangu ukaburudika mno.
Nikaona kuwa yote tuliyokuwa tukifanyiwa kama nchi ni kuuziwa mbuzi kwenye gunia tu. Kesi kama ya Dowans iko wazi kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mikataba hata tukienda mahakama ya mbinguni, hadi hapo tutakapobadili sheria yetu, tutaendelea kushindwa tu.
Zitto Kabwe aliyasema haya, magwiji wa sheria waliyasema haya, kilichoibuka ni wote waliosimama kusema ukweli kubandikwa majina kuwa wamehongwa. Leo wakubwa waliojaza upepo wananchi aibu imewarudi, hawathubutu hata chembe kulizungumzia. Hata Rais Kikwete alidiriki kuwaambia Watanzania kuwa hili la Richmond halijui, lakini Edward Lowassa alipomwambia aeleze ni lipi alilofanya bila yeye kumwelekeza, tumemaliza mwaka sasa Kikwete ‘ame-mute’.
Tabia ile ile aliyoianzisha Kikwete kwa kumruka swahiba wake Lowassa ili yeye aendelee kuonekana msafi, ndiyo tunayoishuhudia sasa ikimuumbua. Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, Ilvine Mugeta, wakati anatoa hukumu katika kesi ya Balozi Mahalu, alisema kuwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakati huo, Jakaya Kikwete, alikwenda Italia na kukubali ununuzi wa nyumba hiyo ufanyike kwa mikataba miwili.
Sitanii, Mugeta hakuuma maneno bali aliweka kila kitu bayana kuwa kama ni uzembe si wa Mahalu bali ni wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, iliyokubali kufanya malipo kwa mikataba miwili na pengine kusaidia ukwepaji kodi kwa muuzaji wa nyumba.
Haiingii akilini kudhani kuwa Kikwete hakulifahamu hili. Haiingii akilini kudhani kuwa Kikwete hakufahamu kuwa Rais mstaafu Benjamin Mkapa alimwelekeza Balozi Mahalu kufanya ununuzi huu. Kwa taratibu za kidiplomasia (ambazo nimezisomea) baada ya Rais katika masuala ya nje ya nchi, namba mbili ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Sitaki kuamini pia kuwa Kikwete hana simu ya Mkapa, kwamba haya aliyokwenda kuyasema Mkapa mahakamani wangeweza kuulizana na Kikwete hata kabla ya kupeleka kesi mahakamani wakapeana majibu. Sina uhakika kama Mkapa ni mkaidi kwa kiwango hicho kwamba Kikwete kama hakuwa na taarifa sahihi angeweza kumpigia simu akakataa kumweleza lolote na kumwambia tukutane mahakamani.
Kwa wasiojua, kuna cheo katika mfumo wetu wa kisheria kinachotambulika kama Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP). Cheo hiki ndiyo serikali yenyewe. Kwa kutumia kifungu cha 89 na 90 cha Kanuni ya Adhabu Sura ya 16, DPP anaweza kuondoa kesi yoyote mahakamani kwa utaratibu wa Nolle Prosequi. Halazimiki kutoa sababu yoyote kwa kuondoa kesi chini ya utaratibu huu.
Hapa namaanisha nini? Kikwete kama hajawahi kusoma Katiba yetu na kuangalia kifungu cha 46 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1977) kinachompa kinga Rais aliyeko madarakani ya kushitakiwa kwa jambo lolote – liwe la jinai au madai alilofanya akiwa madarakani. Kwa kukisoma kifungu hiki iwapo angewasiliana na Mkapa akamwambia aliyokwenda kuyasema mahakamani, basi angemuuma sikio DPP na kumwambia ‘tunakwenda kushindwa ondoa kesi mwanangu’.
Nampongeza Mkapa kwa kukataa unafiki. Kama Mkapa angemtosa Mahalu na kukataa kwenda mahakamani kutoa ushahidi kwa sasa tungekuwa tunampelekea ndala na mswaki Profesa Mahalu Keko, Ukonga au Segerea. Katika hili, Mkapa amesimamia usemi kuwa heri kuishi siku mbili kama simba kwa kusimamia ukweli kuliko kuishi siku 100 kama nzi.
Tabia hii ya Kikwete kutaka kuwatosa wenzake na mikono yake ibaki ikionekana misafi, ndiyo iliyomsukuma Profesa Mahalu kuwaambia waandishi wa habari wasome Zaburi ya 17. Isome msomaji kisha utafakari uzito wa maneno haya. Alamsiki.
Zaburi 17:
1. Ee Bwana, usikie haki, ukisikilize kilio changu, Utege sikio lako kwa maombi yangu, Yasiyotoka katika midomo ya hila.
2. Hukumu yangu na itoke kwako, Macho yako na yatazame mambo ya adili.
3. Umenijaribu moyo wangu, umenijilia usiku, Umenihakikisha usione neno; Nimenuia kinywa changu kisikose,
4. Mintarafu matendo ya wanadamu; Kwa neno la midomo yako Nimejiepusha na njia za wenye jeuri.
5. Nyayo zangu zimeshikamana na njia zako, Hatua zangu hazikuondoshwa.
6. Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika, Utege sikio lako ulisikie neno langu.
7. Dhihirisha fadhili zako za ajabu Wewe uwaokoaye wanaokukimbilia; Kwa mkono wako wa kuume Uwaokoe nao wanaowaondokea.
8. Unilinde kama mboni ya jicho, Unifiche chini ya uvuli wa mbawa zako;
9. Wasinione wasio haki wanaonionea, Adui za roho yangu wanaonizunguka.
10. Wameukaza moyo wako, Kwa vinywa vyao hutoa majivuno.
11. Sasa wametuzunguka hatua zetu, Na kuyakaza macho yao watuangushe chini.
12. Kama mfano wa simba atakayekurarua, Kama mwana-simba aoteaye katika maoteo yake.
13. Ee Bwana, usimame, umkabili, umwinamishe, Kwa upanga wako uniokoe nafsi na mtu mbaya.
14. Ee Bwana, kwa mkono wako uniokoe na watu, Watu wa dunia hii ambao fungu lao li katika maisha haya. Matumbo yao wayajaza kwa hazina yako, Hushiba wana, huwaachia watoto wao akiba zao,
15. Bali mimi nikutazame uso wako katika haki, Niamkapo nishibishwe kwa sura yako.