Wiki mbili zilizopita Mpita Njia (MN) akiwa kwenye gari linalofanya kazi ya kusafirisha abiria (Heace)  kati ya Muganza na Buselesele Wilayani Chato, Mkoani Geita,  aliwasikia abiria  watatu wakiteta juu ya uteketezaji wa nyavu na ukamataji wa wavuvi haramu unaoendelea katika ziwa victoria.

MN alivutiwa na mazungumzo ya abiria hao kwani walionekana kuwa na mitazamo tofauti  katika mzungumzo yao.

Katika mazungumzo hayo MN alisikia mmoja wa abiria hao akihoji uhalali wa serikali kuchoma nyavu haramu na kushindwa kupambana na kiini cha tatizo ambacho ni viwanda vinavotengeza nyavu hizo.

Hata hivyo watatu  hao walikubaliana na hali ngumu ya kiuchumi waliyo nayo lakini wakadokeza neno lilimfanya MN aongeze umakini wa kuwasikiliza.

Walidokeza kuwa siku si nyingi ziwa Victoria litakuwa na samaki wakubwa sana hasa sangara.

Walisema  mbali na sangara hao  kuuzika kwa bei nzuri siku za usoni, mifuko ya samaki hao ya kutunza hewa ambayo kuwasaidia kuogelea wanapokuwa majini (Mabondo) itakuwa na thamani kubwa mno.

MN aliwasikiliza abiria hao wakisema biashara ya Mabondo ambayo imekuwa akifanywa na wachina kwa kushirikiana na Waganda kuwa na faida kubwa mno kwani kilo moja ya bondo huuzwa hadi laki nne na hela hiyo haikatwi kodi.

MN alihitaji kupata undani wa biashara hiyo, ambavyo walimudokeza kuwa kipindi cha nyuma  Mabondo yalikuwa yanatupwa kutokana na watu wengi kutokujua thamani yake,lakini kwa sasa ndiyo yanachangia hata kuongezeka kwa uvuvi haramu.

MN baada ya kupata dondoo hizo ameona ni vyema atume pongezi kwa uongozi wa awamu ya tano kwa juhudi zinazo fanyika ili kuzuia uvuvi haramu.

Lakini anawakumbusha kuwa kuna biashara ya mamilioni yatokanayo na kuuza mabondo ya sangara  inayofanyika ziwani hapo bila ya kutozwa kodi.

MN ameambiwa kuwa sangara wa kilo 80 bondo lake linaweza kuwa na kilo zaidi ya 25 ambavyo likikaushwa na kupelekwa China linaweza kuuzwa hadi milioni 10.