Amani ni tunda la haki. Bila haki amani haipo. Bila haki manung’uniko na vilio hutamalaki.

Tunaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kusimamia suala la haki, na kwa namna ya pekee tunaipongeza Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kwa kuonyesha mwanga wa uwepo wa haki katika mfumo wetu wa sheria.

Mara kadhaa tumeandika matukio ya uonevu katika mifumo yetu ya haki. Mamia ya watu wanaumia mahabusu na magerezani kwa kubambikiwa kesi. 

Wabambikiaji ni baadhi ya watumishi wa vyombo vya dola kama Polisi, na viongozi wenye mamlaka madogo au makubwa.

Tunampongeza DPP kwa kuliona hilo, na kwa kweli anayofanya sasa kwa kuwafutia kesi watuhumiwa mbalimbali ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Tuna maombi kadhaa kwa hili linaloendelea: Mosi, ufutaji kesi usikomee kwa ‘vigogo’ tu ambao wana majina makubwa. Wengi wanaoteseka ni watu wasiokuwa na ‘koneksheni’ kwa wakubwa. Wapo mahabusu maskini wasiokuwa na utetezi wowote – hawa ndio wanaokaa miaka hadi 10 au zaidi bila kesi zao kusikilizwa au ushahidi kukamilika.

Tunamuomba DPP afanye kila analoweza awafikie hao makabwela ili nao wafaidi pepo hii iliyoletwa na Rais Samia.

Pili, ni hadhari kwa dola: Pamoja na nia njema ya kuwaondolea maumivu watu wanaoteseka bila kuwapo kwa ushahidi wa makosa yao, serikali isijisahau na kuanza kuachia watu ambao ni maadui kwa jamii na taifa letu kwa jumla.

Nchi yetu ndani ya muongo huu imeshuhudia viashiria na matukio halisi ya kigaidi. Kuna mauaji ya kigaidi yametokea Tanga, Morogoro, Geita, Lindi, Mtwara, Rufiji, Kibiti na kadhalika. Tunaamini watuhumiwa wa makosa mazito ya aina hiyo si walengwa wa huu msamaha.

Pia Watanzania wanatambua magenge ya matapeli wa viwanja, madini na kadhalika. Hawa nao tunaamini hawatakuwa katika hii ‘achia-achia’ inayoendelea. 

Tunayasema haya tukitambua kuwa nia njema ya serikali inaweza kutumiwa vibaya na ‘wabaya’ ndani ya mfumo kuwaachia watu ambao ni hatari.

Tunachosisitiza hapa ni kuwa haki ni pamoja na kuwapa haki ya kuwaadhibu kisheria wale wote ambao ni tishio kwa usalama, uchumi na ustawi wa jamii na nchi kwa jumla. 

Pia wananchi waelimishwe watambue kuwa sheria bado zipo, kwa hiyo wasifanye makosa kwa matarajio ya kufutiwa mashitaka baadaye.

Hongera DPP kwa kazi unayofanya, lakini tunashauri umakini uwepo ili baadaye tusijikute tunalazimika tena kupambana na matatizo yatakayosababishwa na msamaha huu. 

Haya tumeyaona kwenye msamaha wa Rais kwa wafungwa ambapo baadhi yao waliorudi uraiani wameendeleza uhalifu.