WIKI iliyopita vyombo vya habari nchini vilichapisha habari kuwa Mahakama ya Wilaya Bunda imemtia hatiani na kuamuru afungwe jela miaka mitatu mfanyabiashara mwenye asili ya Kichina, Mark Wang Wei aliyejitoa wazi kumhonga Sh 500,000 Mkuu wa Wilaya hiyo, Joshua Mirumbe.

Wei kupitia kampuni yake ya Panda International Co. Limited, alikuwa akishawishi apewe kandarasi ya kusambaza pembejeo za kilimo wilayani humo. Mirumbe alipigiwa simu na Wei akitaka kwenda kumuona ofisini kwake. Mirumbe akashtuka anamtafuta kwa nia ipi akawaarifu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).


TAKUKURU walijipanga vilivyo na kumdaka Wei mara tu alipokabidhi bahasha yenye kitita cha Sh 500,000. Wei alipofika mahakamani hata hakubishi zaidi ya kukiri mbele ya Hakimu, Safina Semfukwe kuwa ni kweli alitoa kitita kumhonga Mirumbe kwa nia ya kupata kandarasi hiyo.


Hakimu Semfukwe hakuchelewa na kwa mujibu ya sheria akamhukumu Wei kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya Sh 700,000. Wei aliamua kulipa faini akaachiliwa huru. Kwa maana hiyo hakutumikia kifungo cha miaka mitatu jela badala yake amelipa faini.


Sisi tunapenda kuchukua fursa hii kumpongeza Mkuu wa Wilaya Mirumbe kwa kukataa udhalilishaji huu wa wageni. Wageni wamefika mahala wanaambizana kuwa viongozi wa Tanzania wanahongwa kila kitu ikiwamo suti, pipi, fedha na vyakula. Ndiyo maana kwa jeuri kabisa alikwenda na kutoa bahasha ya Sh 500,000.


Tunampongeza pia Hakimu Semfukwe kwani wengine wangeogopa kumhukumu raia wa kigeni, na hasa raia mwenyewe akiwa mwenye ukwasi na aliyetayari kuhonga kwa nia ya kupindisha haki. Hata hivyo, tunasema tukio hili litufungue macho. Ni wazi wageni wengi wanafanya mchezo huu, na huenda Wei amekanyaga pabaya.


Wakati tukiwataka viongozi wetu kujitathimini, tunasema Bunge lenye jukumu la kurekebisha sheria, linapaswa kufanya hivyo haraka kwa sheria ya TAKUKURU hasa mtu anapokiri kwa hiyari kuwa ametoa rushwa. Badala ya kutoa fursa ya faini, iwe ni kifungo tu kukomesha mafedhuri wenye kutembeza rushwa. Rushwa inashusha heshima ya nchi tubadili mbinu za kupambana nayo.