DAR ES SALAAM

Na Pawa Lufunga 

Afrika ina historia ndefu inayohusishwa na maisha magumu kutokana na ukosefu wa siasa safi, ajira na matumizi mabaya ya rasilimali zilizopo.

Maisha ya Mwafrika kijamii, kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi ndiyo yanayoonekana duni kuliko maeneo mengine ulimwenguni.

Wakati Afrika ikitimiza miaka 50 ya uhuru, bado inatajwa kila mahali kama bara lenye umaskini, ukosefu wa haki, kuanguka kwa tawala za kisheria, vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu, teknolojia duni, tawala mbaya, usimamizi mbaya wa rasilimali, ubinafsi na maovu mengine.

Licha ya mabadiliko ya sayansi na uvumbuzi ulimwenguni, Afrika bado inabaki dampo la bidhaa feki.

Hali hii huzika fikra za Mwafrika katika kubuni na kuuza teknolojia yake nje, badala yake kila kinachogunduliwa Afrika huonekana hakina ubora, hivyo kumuacha Mwafrika awe mtumiaji wa vinavyotengenezwa na wengine.

Ipo mifano inayoonyesha jinsi Afrika inavyoendelea kuwa chini ya mataifa ya nje kiuchumi, kiteknolojia na kijamii.

Teknolojia

Uvumbuzi na matumizi ya magari na pikipiki yamekuwapo na yameendelea kuletwa Afrika kwa miongo kadhaa kutoka ughaibuni.

Cha kushangaza hadi karne hii ya 21, hakuna jamii ya Afrika inayotengeneza vitu hivyo zaidi ya kufurahia kuyaagiza kutoka Ulaya, Asia na kwingine.

Tumeshindwa hata kuiga teknolojia hii pamoja na ya kutengeneza simu, kompyuta na vitu vingine vingi licha ya kuwa na maprofesa wengi katika nyanja hizo.

Ni nini kinachofanya hali iwe hivi? Ni swali ambalo Waafrika tunapaswa kujiuliza.

Diplomasia

Katika ulimwengu wa diplomasia, Afrika bado inakabiliwa na visa vya tawala za kidikteta, ufisadi, watawala wabinafsi na wasiowajibika kuliko bara jingine lolote.

Mifano inayoonekana na kuthibitisha ukweli huu ni uchaguzi; kwamba katika uchaguzi maeneo mengi ya Afrika kumekuwa na ripoti za uvunjifu wa haki, mauaji na matendo yasiyofaa kwa wanaoomba kupigiwa kura –  wakosoaji wa watawala.

Kumekuwapo ripoti za wizi wa kura na vyombo vinavyosimamia uchaguzi visivyotenda haki kwa kuwa si huru.

Maisha ya wanaharakati kadhaa wasio na hatia na wazalendo ama yamekuwa hatarini au yamepotea.

Kwa nini uchaguzi unaofanywa na wapiga kura chini ya 1,000 tu ugharimu maisha ya watu? Ni nani anayefaidika na hili? 

Ni maswali yanayochemsha vichwa vya wazalendo halisi pekee, wakisaka suluhu, wakati wabinafsi wachache wakifurahia fursa kutokana na wengine kuonewa.

Waafrika tumekumbwa na janga la kutokuwa na umoja. Afrika kuna vita ya wenyewe kwa wenyewe inayosababishwa na tofauti za kiitikadi na ukabila au maeneo.

Hadi leo kuna Waafirka wanaoishi nje ya mataifa yao kama wakimbizi kutokana na machafuko ya kisiasa, kidini, kikabila na hata kikanda. 

Mitazamo

Hata kifikra, wasomi wengi wa Afrika wamekuwa na mitazamo tofauti juu ya utajiri wa bara hili, wakati wasomi wa mabara mengine wanaiona Afrika kama bara lenye baraka na rasilimali anuwai.

Wasomi wa Afrika wanaiona Afrika kama bara duni kwa asili, ambalo haliwezi kujengwa kushindana na mabara mengine kiuchumi, kisiasa, kijamii, kiutamaduni na hata kiakili.

Mmoja wa wasomi wa Afrika, Profesa Patrice Lumumba (PLO), amewahi kunukuliwa akisema machafuko ya Afrika ni matokeo ya mitazamo duni ya walio katika tawala, akisema hawana maono mazuri ya kufanikisha matarajio ya bara hili.

“Shida ya Afrika ni kwamba, walio madarakani hawana maarifa, lakini wale walio na maarifa hawana nguvu,” anasema PLO akiwahutubia wanazuoni wa kimataifa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mtazamo wa Lumumba juu ya shida za Afrika ni matokeo ya umaskini wa kifikra kwa viongozi wake ambao wanapingana na raia wa chini wenye maono mazuri ambayo yangeheshimiwa na viongozi, yangelibadilisha bara hili. 

Hata hivyo katika kukabiliana na masuala yote hayo, ajabu ni kwamba mawakala wakuu wa kutafuta suluhu na kuweka maazimio ni watu kutoka mabara mengine!

Kwa upande mwingine, viongozi wengi wa Afrika na wafuasi wao hawakubali nchi zao kutajwa kama nchi maskini, zisizo na maadili katika siasa za kistaarabu na dhuluma.

Badala yake huwashuku wanaolalamikia mambo hayo na kuwaona kama washirika wa wakoloni mamboleo na wasaliti. 

Ni nani aliye sahihi kati ya wanaounga mkono ukweli kwamba Afrika inakabiliwa na mienendo hiyo mibovu na wanaosema Afrika imetulia? Iko shwari kabisa ikifanya vizuri katika nyanja zote?

Jawabu la madhila haya

Mataifa mengi yaliyostawi yalipata hadhi hiyo baada ya umoja kamili uliowaweka pamoja na kuwa nchi moja yenye nguvu katika nyanja zote. 

Marekani, Urusi, Ujerumani, Uchina, Uingereza na mataifa mengi yenye nguvu kiuchumi, kiteknolojia na kisiasa yalibadilika kupitia njia hii.

Fursa za kisiasa, ubinafsi, kiu ya madaraka, mitazamo potofu juu ya kabila, dini, rangi, misimamo ya vyama vya kisiasa, hali ya uchumi wa mataifa ni sababu kubwa ya machafuko yanayoikumba Afrika kwa miongo kadhaa tangu uhuru.

Ni kutokana na kero hizi, ndoto ya wanadiplomasia wakubwa wa Afrika na waasisi wa uhuru inatoweka na hata kusahaulika.

Maono yao yalikuwa kuifanya Afrika kuwa dola kubwa moja; shirikisho; serikali yenye nguvu na nchi zote za Afrika zingetambulika kama majimbo ambayo kwa pamoja yangeitwa the United States of Africa.

Waasisi hao walioona mbele na mbali sana ni Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania, Kwame Nkrumah (Ghana), Namdi Azikiwe (Nigeria) na Mfalme Haile Selasie wa Ethiopia.

Maono na malengo ya waasisi hawa vimesalia kwenye makaratasi na hati dhaifu zisizoendelezwa za AU. 

Ni dhahiri kwamba warithi wao hawakuthamini mawazo hayo, labda kwa sababu ya masuala yale yale; ubinafsi, uchu wa madaraka na kadhalika.

Kilichosalia kwa sasa ni vikundi ‘dhaifu’ vya ushirikiano wa kijamii na kisiasa kama EAC, COMESA, SADC na ECOWAS.

Vikundi hivi havina nguvu za kuchochea uimarikaji wa Afrika kiuchumi, kisiasa, kiteknolojia na hata kijamii.

Viongozi wa Afrika wa leo

Wanadiplomasia na wanaharakati wenye ushawishi wanapaswa kuzitazama jumuiya hizi za kikanda kama sehemu ya kuanzia katika kuunda chombo chenye nguvu zaidi.

Chombo chenye nguvu kisiasa, kiuchumi na kijamii duniani. Yaani iwepo taasisi itakayosimama kama chombo cha Kiafrika katika ngazi zote za vikao vya kitaifa na kimataifa.

Kwa muundo wa jumuiya zilizopo, Afrika haitafika popote kwani hazina nguvu, ingawa ni hatua bora ya kuanzia katika kuwaenzi mababa wa Afrika waliotamani kuwapo kwa United States of Africa.

Chombo chenye nguvu cha Afrika chenye taasisi imara kama Mahakama ya Haki ya Afrika, Jeshi la Afrika, Baraza la Wawakilishi (Bunge la Afrika), Baraza la Mawaziri wa Afrika, Benki ya Afrika na idara nyingine muhimu.

Malalamiko yote ya Afrika yatatuliwe na Waafrika bila kusubiri shinikizo kutoka kwa watu wa nje kuingilia.

Kuwepo chombo cha Afrika chenye jukumu la kuratibu taratibu za uendeshwaji wa masuala ya utamaduni na burudani kama kuanzisha timu ya soka ya Afrika.

Haya yakizingatiwa, Afrika itatumia vipaji vya ndani kuinuka na hakika itafanya vizuri na itafika mbali.

Hii itasaidia kuimarisha umoja wa Waafrika na hisia za Uafrika na Afrika itasonga mbele baada ya kuondoa fikra za kulilia misaada, matamko na uamuzi wa kutatua changamoto zetu.

0689990248

[email protected].