Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Wiki iliyopita Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu (mstaafu), Jaji Joseph Sinde Warioba, alizungumzia uchaguzi wa serikali za mitaa na kusisitiza kuwa mwenendo wa uchaguzi unavyokwenda na kwa jinsi watu wanavyoonyesha dalili za kuishiwa uvumilivu, amani ya Tanzania imo hatarini.

Amezungumzia hali ya kutoridhika kwa baadhi ya vyama kuona kama uchaguzi wanaonewa, lakini pia akazungumzia vurugu zinazojitokeza katika uchaguzi, ambapo watu wanajeruhiana, wanauana na kujengeana chuki. Ametahadharisha kuwa mwenendo huu hauna afya kwa ustawi wa taifa la Tanzania.

Wiki hiyo hiyo, Ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Amani Simbayo, akauawa na wananchi waliozingira gari la TRA na kukataa mtu aliyekuwa anafuatiliwa asikamatwe kutokana na hofu ya uwapo wa mtandao wa ‘watekaji’ ambao mara kadhaa wameteka watu na ama kuwapoteza au kuwaumiza.

Sitanii, nahusishanisha matukio haya mawili, kwani katika siku za hivi karibuni Tanzania imeanza kushuhudia ongezeko la matukio ya wananchi kujichukulia sheria mikononi dhidi ya watu wanaowatilia shaka kuwa ni sehemu ya ‘watu wasiojulikana,’ kundi linalodhaniwa kuhusika na utekaji, mauaji au vitendo vingine vya kihalifu.

Tukio la wiki iliyopita, ambapo mfanyakazi wa TRA Simbayo alipigwa hadi kufariki dunia kwa majeraha akidhaniwa kuwa ni mtekaji, linaibua mjadala mpana kuhusu athari za hali hii kwa usalama wa raia, imani kwa vyombo vya dola na utulivu wa kijamii.

Nafahamu matukio kama haya yanatokana na ukosefu wa taarifa sahihi. Kwamba wananchi wengi hawana ufahamu wa kutosha kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa na mamlaka za usalama kukabiliana na matukio ya kihalifu kama haya ya utekaji, hali inayochochea hofu na uvumi.

Sitanii, historia ya matukio ya utekaji na mauaji yaliyotokea huko nyuma, ambayo hayajapatiwa ufumbuzi au taarifa za uchunguzi kuwekwa wazi, imewafanya wananchi kuwa na shaka kubwa na kuwa tayari kuchukua hatua haraka wanapohisi tishio. Hii inarejesha mkono ule uliokuwapo miaka michache iliyopita wa “wananchi wenye hasira kali.”

Sitanii, kutotoa taarifa za uchunguzi wa matukio hadharani na kwa nguvu au kishindo kilekile cha utekaji, kunazaa hisia miongoni mwa baadhi ya wananchi kwamba vyombo vya usalama haviwezi au havijafanya kazi ya kutosha kushughulikia changamoto za usalama, hali inayosababisha watu kujihami wenyewe.

Hatari kuu iliyopo ni kuwa watu wasio na hatia wataanza kupoteza maisha, kama tukio la mfanyakazi wa TRA ni mfano wa jinsi uvumi na hisia za haraka zinavyoweza kusababisha vifo vya watu wasiohusika na matukio ya uhalifu.

Hali hii isipodhibitiwa itavuruga utawala wa sheria kwa wananchi kujichukulia sheria mikononi, hali inayovunja misingi ya kikatiba na kudhoofisha mamlaka ya vyombo vya sheria. Tukumbuke zipo silaha nyingi za jadi zinauzwa bila kizuizi. Wananchi wakihamishia mikononi mwao jukumu la kujilinda, madhara yanakwenda kuwa makubwa mno, hali inayoweza kuzaa machafuko.

Sitanii, polisi mnao wajibu wa kudhibiti hali hii, kwani tulipofikia sasa kunaweza kuwapo kuzorota kwa uhusiano kati ya wananchi na serikali. Wananchi wanapoanza kupoteza imani kwa vyombo vya dola, uhusiano kati yao unaweza kudhoofika, na hii inahatarisha mshikamano wa kitaifa.

Naamini kama nchi hatujachelewa. Polisi waanze kufanya kazi ya kuzuia matukio haya ya utekaji. Ikitokea tukio la aina hii limetokea, uchunguzi ufanyike haraka kama tunavyoona kwa nchi za wenzetu, kisha taarifa ya matokeo ya uchunguzi itangazwe hadharani haraka. Hii itaongeza imani kwa wananchi kuwa Jeshi la Polisi limo kazini.

Suala la elimu kwa umma halikwepeki. Serikali na vyombo vya habari vinapaswa kutoa elimu kwa umma juu ya umuhimu wa kuzingatia utawala wa sheria na kuepuka kujichukulia sheria mikononi. Kama ilivyokuwa zamani, polisi sasa waanze kuwaelimisha tena Watanzania taratibu za kisheria, ikiwamo jinsi ya kukamatwa, matakwa ya lazima kutoka kwa mkamataji na mkamatwaji.

Elimu hii iende sambamba na kujitathmini. Ripoti ya Tume ya Haki Jinai ilisema bayana kuwa kuna vyombo vingi vinavyofanya ukamataji, hali inayowachanganya wananchi. Ukamataji ubaki kwa Jeshi la Polisi pekee. Ikiwa TRA wanaamini kuwa mhusika anayo kesi ya kujibu, wafanye mawasiliano na polisi kufanya ukamataji badala ya kwenda wenyewe, hali inayowafanya wananchi wasiwatofautishe na watekaji.

Kama nilivyosema, ziwepo juhudi za makusudi kuharakisha uchunguzi wa matukio. Mamlaka za usalama zinapaswa kushughulikia kwa haraka na uwazi kesi za kihalifu ili kuondoa uvumi na kurudisha imani ya wananchi.

Wakati hayo yakiendelea, kwa pamoja tuimarishe usalama wa jamii. Tunapaswa kuweka mikakati ya usalama wa kijamii kwa kushirikisha wananchi katika mipango ya ulinzi shirikishi, inaweza kusaidia kupunguza hofu na kutoa nafasi ya kushirikiana na vyombo vya usalama.

Sitanii, kwa watakaobainika kutenda makosa kweli, basi itolewe adhabu kali kwa washiriki wa matendo haya maovu na jamii ifahamu kuwa wahusika wamehukumiwa kama ilivyofanyika kwa haraka kwa “Vijana wa Afande” wabakaji. Serikali inapaswa kusimamia sheria kwa kuhakikisha kuwa wote wanaojihusisha na vurugu na mauaji ya kiholela wanakabiliwa na hatua kali za kisheria.

Hali ya wananchi kujihami kwa hofu dhidi ya kile wanachoamini kuwa ni “watu wasiojulikana” ni tishio kubwa kwa utawala wa sheria na usalama wa kijamii nchini Tanzania.

Tukio la kuuawa kwa mfanyakazi wa TRA linapaswa kuwa somo kwa vyombo vya dola kuchukua hatua za haraka na madhubuti ili kurejesha imani ya wananchi, kupunguza hofu na kuhakikisha kuwa haki inatendeka kwa mujibu wa sheria.

Bila hatua hizi, na bila kusikiliza mwangwi wa sauti ya Jaji Warioba katika uchaguzi wa sasa na ujao, Tanzania itakuwa inajihatarisha kuingia katika mzunguko wa machafuko na vurugu zisizo na mwisho.

Tunayo nafasi ya kuyazuia haya. Sheria ichukue mkondo wake, tusimamie haki bila uonevu, jamii itasimama yenyewe. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404 827