Mei, 2013, aliyekuwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Jakaya Kikwete aliwaaga wapiganaji wa Tanzania waliokwenda DRC kulinda amani dhidi ya waasi wa kundi la M23 Mashariki wa nchi hiyo.

Rais Kikwete alimkabidhi bendera kiongozi wa bataliani ya wapiganaji wa JWTZ waliokwenda kujiunga na Jeshi la Umoja wa Mataifa la kulinda amani nchini humo katika hafla iliyofanyika Msangani, Kibaha mkoani Pwani.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, wa wakati huo, Shamsi Vuai Nahodha na Mkuu wa Majeshi wa wakati huo Jenerali Davis Mwamunyange ni miongoni mwa walioshuhudia hafla hiyo.

Tanzania iliungana na naungana na Afrika Kusini na Malawi kufanya kuwapo kwa kikosi cha askari 3,100. Tanzania ikipeleka askari 850.

Vikosi vya awali vya Tanzania viliongozwa na Brigedia Jenerali Mwakibolwa na kuwasili Goma ambao ndio Mji Mkuu wa Jimbo la Kivu ya Kaskazini unaokaliwa na waasi wa M23 tangu Aprili 2012.

Septemba 2013, Gazeti la JAMHURI, liliandika ‘JWTZ yasafisha M23’ katika toleo hilo tuliandika kuwa JWTZ kwa kushirikiana na majeshi washirika ya kimataifa, limewafurusha askari wote wa kundi la M23 kutoka katika ardhi ya Mji wa Goma.

Ukiacha hali hiyo ya waasi wa M23 waliokuwa wanasumbua kwa kuranda na kufyatua risasi hovyo usiku na mchana, habari za uhakika kutoka ndani ya Jeshi hili linaloongozwa na JWTZ, zilieleza kuwa waasi walibembeleza kipigo walichokipata Agosti 21, kisirejewe.

Mazungumzo yanayoendelea Uganda kati ya Serikali ya Rais Joseph Kabila na waasi wa M23, ni wazi yatahitimishwa kwa kumaliza vita. Kinachoendelea ni malalamiko kwenye mazungumzo hayo tu kuwa askari wa Tanzania wanawachapa kupita kiasi,” alisema mmoja wa washiriki wa vikao vinavyoendelea jijini Kampala.

Wamepata mshituko, hawakutarajia. Walikuwa hawaijui Tanzania na ndiyo maana Umoja wa Mataifa umeona ni bora kikosi hiki kiongozwe na Tanzania kutokana na uzoefu wa Anjouan, Lebanon, Darfur na maeneo mengine ambapo majeshi ya Tanzania yanalinda amani. Mara zote, majeshi yetu yamefanya kazi ya kupigiwa mfano,” kilisema chanzo kingine.

Habari za uhakika kutoka ndani ya JWTZ zilisema pamoja na mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea Uganda, Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, alitoa makombora ya masafa marefu yanayoweza kusafiri hadi kilomita 1,000 kutoka eneo yaliporushiwa, yakasaidie kufurusha waasi misituni.

Ametoa makombora haya yako standby (tayari tayari). Ikiwa mazungumzo yatavunjika, basi yatatumiwa kuwafyekelea mbali huko huko msituni waliko.

 “Tunapata wakati mgumu kweli. Askari wetu wanafika mahala wanasema waruhusiwe wakasafishe hadi hao waliokimbilia misituni, sisi tunawaambia tulieni tu. Tusubiri mazungumzo ya Uganda yaishe, ila kwa kila hali lazima M23 wasalimishe silaha. Wasiposalimisha, hakuna msalie Mtume, hapo tutawachapa vilivyo hao wachache watakaokuwa wamesalia,” kilisema chanzo chetu.

Nchi za Afrika Kusini, Malawi na Msumbiji zinaunda Jeshi la Umoja wa Mataifa linaloongozwa na Tanzania kwa wakati huo.