Serikali imeandaa kampeni ya kitaifa ya kuhakikisha kuwa wanaume wanapima kwa hiari maambukizi ya Virusi ya UKIMWI.

Hayo yamesema na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alipokuwa katika harambee ya uchangishaji wa fedha za Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI Nchini (ATF).

Serikali imefikia hatua hiyo kufuatia hali ya wanaume wengi kutojitokeza kupimwa UKIMWI kwa hiari kama ilivyo kwa wanawake.

Kampeni hiyo itaanza mwezi Machi 2018 na itadumu kwa miezi miwili ikiwa na lengo la kuhakikisha kila mwanaume anapima na kufahamu hali ya afya yake.

Waziri Mhagama alisema kwamba, tatizo la maambukizi ya UKIMWI ni kubwa sana, hivyo ni vyema wakapima ili kuweza kuweka mikakati ya kukabiliana na ugonjwa huo.

Waziri Mhagama aliyasema hayo baada ya utafiti wa viashiria vya VVU/UKIMWI nchini mwaka 2016/17 kuonyesha idadi ndogo ya wanaume wanaoishi na VVU ndio wanafahamu hali zao za maambukizi tofauti na wanawake.

“Wanaume ni lazima tuambiane ukweli, kupima VVU/UKIMWI ni lazima sio kuwaacha wanawake peke yao katika kupima. Lakini hii haimaanishi wanawake waache kupima kwa sababu hata wao bado kuna asilimia kubwa hawajui hali zao za maambukizi” alisema Waziri Mhagama.

Kuhusu mfuko huo, Waziri Mhagama alisema kwamba, kila mmoja katika Mkoa na Wilaya anayoishi anatakiwa kuchangia lengo likiwa ni kuondokana na utegemezi wa wahisani katika mapambano dhidi ya UKIMWI.