Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazosifika kwa kuwa na umoja na amani, tofauti na nchi nyingi katika Bara la Afrika na dunia kwa ujumla.
Nchi yetu imekuwa na amani kiasi cha Watanzania kuchoshwa na amani hii inayoliliwa na wenzetu hadi kuanza kutamani kuivuruga na kuishi maisha ya kukimbia na kukimbizana.
Ni vyema kila mmoja wetu akatambua ya kuwa vurugu na mapigano si kitu cha kuombwa katika nchi yoyote duniani, hasa ambayo wananchi wake hawana historia ya kuishi maisha hayo.
Naamini ya kuwa kila mmoja wetu ni shahidi kufuatia nchi yetu hii kuwa sehemu ya kimbilio kwa majirani zetu yanapotokea mapigano kule makwao. Tumeshukudia ni kwa kiasi gani majirani zetu wanavyopata shida na kukimbia nchi zao, familia zao na maisha yao ya kila siku na halafu kuanza maisha mapya wasiokuwa na uhakika nayo.
Si jambo la kuiombea wala kuiombea nchi yangu Tanzania kufika huko.
Ni jukumu letu sote kuhakikisha tunalinda umoja wetu na amani yetu tuliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu kwa nguvu zetu sote.
Sote ni mashahidi kwa kilichokuwa kinaendelea nchini katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita wakati nchi ilipoingia katika mtikisiko wa Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (UKUTA) ambao ulitetema, ukatetemesha vyombo vyote vya dola, ukatetemesha viongozi wetu huku kila mmoja wetu akitetema bila kujua hatima ya mtetemo huo.
Ukuta ukatamalaki, tukayaona majeshi yetu yakifanya mazoezi hadharani tofauti na tulivyozoea, wenye ukuta wao nao wakatoa msimamo wa kusimika Ukuta bila kujali nini kitakachojiri.
Tanzania, nchi yangu, ikakumbwa na ugonjwa wa mtetemo wa Ukuta uliokuwa umeshika hatima ya nchi yetu pendwa.
Viongozi wakaishi maisha ya matamko, kila iitwayo leo kila kiongozi katika jamii yetu akatetema na kutoa tamko, wananchi wakapata woga, wasioitaki mema nchi yetu wakaanza kushangilia anguko la nchi yetu pendwa.
Kupitia mitandao ya kijamii huko ndiko ilikokuwa njia pekee ya uhamasishaji wa Ukuta, Watanzania wenzangu wakaanza kufunzwa jinsi ya kupambana na vyombo vya dola, wakafunzwa kuiangamiza amani yao, wakafunzwa ujasiri uchwara na kusababisha vurugu zisizo na ukomo!
Sitapenda kujadili yale yote niliyoyashuhudia kupitia mitandao hiyo, maana hayana nia njema na ustawi wa nchi yangu, bali ni vyema tukajiuliza nani aliyeturoga kiasi cha kufikia hapa tulipofika?
Ni lazima tujiulize; kweli tumerogwa? Ina maana tumeichoka amani tuliyonayo kwa kiasi hiki? Au ni ulimbukeni tu wa kupenda kuiga mambo yasiyoigwa katika dunia ya sasa inayolilia amani?
Sikubalini na msemo wa ‘mtoto akililia wembe mpe umkate…’
Kila mmoja wetu anatakiwa kutambua ya kuwa amani ya nchi yetu iko mikononi mwa kila mmoja wetu, na ni jukumu letu kuhakikisha tunaendelea kuwa salama huku tukiilinda amani hii bila kuendekeza mafunzo ya hovyo tunayofunzwa na wasioitakia mema nchi yetu.
Ni lazima tuziulize nafsi zetu; nini hasa nia zetu katika kuyafanya haya tunayoyafanya sasa? Tujiulize, tunaitendea haki nchi yetu kama tunavyopashwa katika zama hizi? Tujiulize, kwa kina tuko radhi kujiingiza katika mambo ya hovyo kwa faida ya nani?
Pamoja na kuziuliza nafsi zetu, ni muda mwafaka sasa kwa viongozi wetu kujitafakari upya na kuangali hatima ya nchi yetu katika kizazi hiki cha dot.com. Kufahamu mahitaji ya wananchi na nchi kwa ujumla, si kutoa miongozo ya kukariri na kuibuka na matamko tata yanayoibua sintofahamu na manung’uniko yasiyoisha.
Mungu Ibariki Tanzania.