Mwanasiasa aliyetikisa taifa katika Uchaguzi Mkuu Mwaka 2015, Edward Ngoyai Lowassa, mwaka huu wa 2018 ameuanza kwa kishindo, baada ya ghafla kumtembelea Rais John Magufuli, Ikulu jijini Dar es Salaam hali iliyozaa fukutoa kwa upinzani na kicheko ndani ya CCM.
Hatua ya Lowassa kwenda Ikulu Januari 9, mwaka huu, imezua mjadala mzito miongoni mwa baadhi ya wafuasi wa vyama vya upinzani, huku wengine wakipendekeza afukuzwe, ila yeye amejibu kwa ufupi tu; “Nilichokitenda kina faida kwa taifa hili.”
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Januari 9, amesema hakuwa na taarifa za Lowassa kumtembelea Rais Magufuli Ikulu na akaongeza kuwa maoni aliyotoa ya kuipongeza Serikali ya Rais Magufuli ni yake binafsi na si ya chama chao, ila siku moja baadaye, Mbowe akazungumza na Gazeti la Mwananchi, akawataka wafuasi wa chama chao kutulia akisema; “Kuna watu wana nia ya kuwachonganisha wapinzani na hawatafanikiwa.”
Rais Magufuli kwa upande wake amemtaja Lowassa kama mwanasiasa mahili, huku akimsifia kwa kufanya siasa za kistaarabu na akikiri kuwa katika kampeni za uchaguzi za mwaka 2015 Lowassa hakupata kumtukana hata siku moja.
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu aliyeko kwenye matibabu nchini Ubeligiji, amesema Lowassa asingeweza kuisifia Serikali ya Rais Magufuli wakati waliompiga risasi yeye (Lissu) hawajapatikana na hakuna uchunguzi wowote uliofanyika, magazeti yanafungiwa, kesi za uchochezi zimezidi kipimo, waandishi wa habari na wanasiasa wanapotezwa.
Wimbi hilo la aina yake, limekisukuma Chadema kuitisha Kamati Kuu ya dharura iliyokuwa ikutane Jumamosi, Januari 13, lakini ikaahirishwa kutokana na Mkurugenzi wa Sheria na Katiba wa Chama hicho, Peter Kibatala kufiwa na mama yake mzazi ikabidi viongozi waende Morogoro kushiriki maziko.
John Mrema, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, Jumapili mchana ameliambia JAMHURI; “Kikao kinaendelea hadi sasa hivi [katika Hoteli ya Bahari Beach Dar es Salaam], hakujawa na taarifa ya kutoa.” Afisa Habari wa chama hicho, Tumaini Makene amesema: “Kikao ni closed session (si mkutano wa wazi), taarifa zikiwa tayari nitawajulisheni.” Hadi tunakwenda mitamoni tulikuwa hatujafahamu kikao hicho cha Kamati Kuu kimeamua nini.
 
Lowassa azungumza
JAMHURI limemtafuta Lowassa kupata maoni yake baada ya vijana na baadhi ya viongozi wa Chadema kumshambulia kwa maneno makali kuwa ndiyo maana wakati wa kampeni mwaka 2015 hakumgusa Rais Magufuli katika hoja ya uuzaji wa nyumba na mengine mengi huku wengine wakisema anajiandaa kurejea CCM.
Lowassa amesema: “Hivi kweli inaingia akilini nitumie saa nzima kupongeza kweli? Maishani nimejiwekea utaratibu wa kutojibizana na wanaonitafuta, ila faida ya nilichofanya ni kubwa kwa taifa hili na kila mtu ataiona mbele ya safari. Amani yetu tunapaswa kuilinda na inapatikana kwa njia ya mazungumzo.”
JAMHURI lilipomdodosa kutaka kufahamu ni suala lipi hasa jingine alilozungumza na Rais Magufuli, ameongeza: “Kuna mambo tumezungumza na pande zote tukakubaliana kuwa ni siri, hivyo si vyema kuvunja makubaliano na naendelea kuheshimu hilo.”
Lowassa amesema wanaodhani anajiandaa kurejea CCM wanapoteza muda, ila akasisitiza kuwa nchi inahitaji kujenga upinzani unaofanya siasa zisizo za kiharakati kwani kwa kufanya hivyo wananchi wataviamini vyama vya upinzani na kuvikabidhi madaraka makubwa zaidi.
JAMHURI lilipomhoji Lowassa iwapo amemweleza Rais Magufuli hoja za wananchi kukerwa na kufungia magazeti, kuzia Bunge Live, kuzuia mikutano ya kisiasa, kutaka uchunguzi wa Lissu kupigwa risasi na mwandishi wa Mwananchi Azory Gwanda kupotea uharakishwe, akasema: “Nimekwambia kuna mambo tumekubaliana yabaki siri, na naendelea kuheshimu hilo.”
 
Julius Mtatiro anena
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) Julius Mtatiro, amesema si kosa kwa Lowassa kukutana na Rais Magufuli, isipokuwa hoja alizozitoa kuisifia Serikali ya awamu ya tano ikiwamo kutengeneza ajira nyingi nchini, zinapaswa kukosolewa.
Amesema Tanzania inashuhudia kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira unaoongezeka kila mwaka, hivyo haikumpasa Lowassa kutoliona hilo na badala yake kumsifia Rais Magufuli.
Amedai takwimu zinaonesha hali ya uchumi isivyokuwa nzuri nchini, hivyo kukwamisha jitihada za Watanzania kuondokana na umasikini.
 
Amesema kutokana na hali hiyo, kauli ya Lowassa kumsifu Rais Magufuli ni kama amejisafishia njia ya kutowania urais mwaka 2020, kwa sababu hatakuwa na jambo jipya la kuahidi kwa vile ameshatamka kuwa Serikali iliyoko madarakani inafanya kazi nzuri.
Hata hivyo, Mtatiro amesema Lowassa ana haki na uhuru wa kufanya mambo binafsi ikiwa ni pamoja na kufanya ziara kama alivyokwenda Ikulu pasipo kuingiliwa na mtu yeyote.
“Ziara ya Lowassa kwenda Ikulu ilikuwa ya binafsi isiyohusiana na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), licha ya ukweli kwamba mwanasiasa huyo alikuwa mgombea urais aliyeungwa mkono na umoja huo katika Uchaguzi Mkuu wa 2015,” amesema.
 
Fatma Karume
Wakili Msomi wa kampuni ya IMMMA Advocate, Fatma Karume amesema kikao cha Lowassa na Rais Magufuli kimemwezesha Waziri Mkuu huyo mstaafu kutumia haki yake ya kikatiba kutoa mawazo kwa mujibu wa Katiba.
Amesema Lowassa kwenda Ikulu si kosa kwani ametumia uhuru wake kama Mtanzania wa kawaida, mwenye uhuru wa kufanya chochote, ilimaradi asivunje sheria za nchi.
Ametaja tatizo lililopo ndani ya vyama vya siasa kuwa ni kujadili watu badala ya issues (masuala), na kwamba itakuwa vigumu kufahamu wawili hao walizungumza nini kwani walikuwa wao tu katika mazingumzo hayo.
Anaamini njia pekee ya kufahamu kilichozungumzwa ni kwa viongozi hao kukubaliana kukiweka hadharani walichozungumza badala ya watu kujadili hoja ya Lowassa kwenda Ikulu tu.
Karume amesema anaamini katika uhuru wa kutoa mawazo, hivyo kwake Lowassa aliyetoa upinzani mkali kwa Rais Magufuli mwaka 2015 katika Uchaguzi Mkuu kwenda kwake Ikulu si hoja hata chembe, ila ameonya:
“Unapokuwa mwanasiasa mwenye hadhi kama ya Lowassa, unapaswa kuwa makini na yale unayoyaongea, vinginevyo unaweza ukajikuta unatoa mtaji wa kisiasa kwa wapinzani wako.” 
 
Profesa Baregu
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu, amemtaka Lowassa ajitokeze hadharani na kueleza kwa umma ajenda iliyompeleka Ikulu ili kuondoa minong’ono iliyotawala, badala ya ukimya unaozua maswali miongoni mwa Watanzania na kushindwa kuelewa dhamira yake.
Amesema Lowassa alikuwa na fursa ya kumshauri Rais Magufuli kuhusu hali mbaya ya usalama inavyoendelea nchini yakiwemo mauaji yanayyotokea katika maeneo mbalimbali yakiwahusisha “watu wasiofahamika” kama mauaji ya Kibiti, kupigwa risasi kwa mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, miili ya watu inayookotwa katika fukwe za Bahari ya Hindi na kutekwa na kupotea kwa watu.
Amesema hoja nyingine ambayo Lowassa angepaswa kumweleza Rais Magufuli ni hali ya uchumi inayoonekana kudorora huku baadhi ya benki zikifungwa na pia kumshauri Rais Magufuli juu ya hali ya kisiasa nchini ambayo inaonekana dhahiri kuna uminywaji wa demokrasia na uvujwaji wa katiba ya nchi.
Profesa Baregu amesema Lowassa alipaswa kukumbuka mizengwe ya kura za urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 hivyo isingefaa kuonana na Rais Magufuli pasipo kuhusisha hoja hiyo.
 
Profesa Safari
Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Tanzania Bara), Profesa Abdallah Safari, amesema hapakuwa na sababu za Lowassa kupongeza utendaji kazi wa Serikali ya Rais Magufuli kwa vile, pamoja na mambo mengine vyama vya upinzani vinapitia kipindi kigumu cha kuminywa demokrasia tangu Rais Magufuli aingie madarakani.
“Unakwenda kumpongeza Rais Magufuli kwa lipi, anayezuia vyama vya upinzani kufanya shughuli zake ambazo ziko wazi kwa mujibu wa Katiba,” amehoji Profesa Safari.
Profesa Safari ameunga mkono hoja ya Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT), Profesa Mwesiga Baregu anayemtaka Lowassa ajitokeze hadharani na kuueleza umma kuhusu ajenda iliyompeleka Ikulu, ili kuondoa minong’ono iliyotawala miongoni mwa Watanzania.
Profesa Safari ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya Chadema, amesema bado kuna nafasi (ikiwa itahitajika) kwa Kamati hiyo kumhoji Lowassa ili kuelewa sababu za kumpongeza Rais Magufuli badala ya kuhoji kuhusu vyama vya upinzani kuzuiwa kufanya shughuli zake na hali ya usalama inavyodorora nchini kwa sasa.
Amegusa hoja kwamba watu wanapotea katika mazingira ya kutatanisha, wengine kutojulikana walipo na kushambuliwa kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, masuala ambayo Lowassa alipaswa kumweleza Rais Magufuli.
Kwa upande wake Mbowe amesema Chadema hawana mpango wa kuhukumiana kutokana na kauli hiyo ya Lowassa watazungumza ndani ya vikao vya chama na kuwekana sawa kisha maisha yataendelea.
Lowassa alimtembelea Rais Magufuli Ikulu Januari 9, mwaka huu na baada ya hapo zilisambazwa video kwenye mitandao ya kijamii zilizoonyesha Lowassa akimpongeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya katika sekta ya elimu, miundombinu, ajira na nidhamu ya utumishi wa umma hali iliyowakera wafuasi wa upinzani.