Kwanza naomba nitumie fursa hii kuungana na wazazi, ndugu, jamaa na Watanzania wote kwa msiba mkubwa wa kuondokewa na watoto wetu – wanafunzi wa Shule ya Lucky Vicent ya jijini Arusha – katika ajali iliyotokea Karatu.
Taarifa ya awali iliyotolewa na Ikulu ilithibitisha kuwa wanafunzi 32 na walimu wawili walikuwa wameaga dunia katika ajali hiyo. Huu ni msiba mkubwa, si kwa wazazi na uongozi wa shule hiyo tu, bali kwa Watanzania wote.
Bila shaka ajali hii itakuwa kichocheo kipya kwa mamlaka zinazohusika kusimamia ubora wa vyombo vya usafiri na uhakiki za madereva. Huu ukaguzi wa kadi pekee hautoshi. Watoto 34 kufa katika ajali moja ni jambo baya mno. Mungu awalaze mahali pema peponi, AMINA.
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imetangaza majina karibu 10,000 ya watumishi wa umma wenye vyeti vya kughushi.
Wakati akikabidhiwa orodha hiyo, Rais John Magufuli akapigilia msumari wa moto kwa kuamuru wote waliotajwa, ama wajiondoe wenyewe kazini, au wasubiri mkono wa sheria.
Kwa tamko hilo, kumeripotiwa kuwapo uhaba mkubwa watumishi wa umma katika idara na sekta mbalimbali nchini kote.
Kama ilivyotarajiwa, wapo waliounga mkono mpango huu kwa asilimia 100, lakini wapo walioukosoa.
Mara zote nimesema nchi inapokuwa kwenye ‘vita’, wanahabari, kama walivyo raia wema wengine wa nchi hii, hawana budi kuungana katika mapambano.
Suala la vyeti ni sehemu ndogo sana ya tatizo kubwa la kuporomoka kwa uadilifu katika nchi yetu. Serikali ya Rais Magufuli ilichofanya ni kutoa salamu kwa wananchi kujiepusha na maisha ya ujanjaujanja tuliyoishi kwa miaka mingi. Ni wajibu wa kila mwenye macho kuweza kuona, na mwenye masikio kuweza kusikia.
Endapo kuanzia Oktoba, 2015 hadi leo Mei, 2017 hakuna mwananchi aliyekwisha mwelewa Rais Magufuli na dhamira yake kwa nchi hii, basi huyo atakuwa na matatizo yake binafsi.
Zama hizi si za kuishi kwa ujanjaujanja. Tunapaswa kubadilika. Tena basi, inapotokea Serikali ikawa imetoa tamko au ilani fulani, ni vizuri wananchi wakalipokea na kuamini kuwa hilo tamko si la ‘nguvu ya soda’ wala la kuchangamsha baraza.
Kwa miongo mingi Watanzania wamelalamikia hali ya kuharibika kwa mambo katika nchi yetu. Wamelalamikia vitendo vya kughushi, wizi, ufisadi na uhalifu wa kila aina. Wamelalamikia kuporomoka kwa maadili. Tunapozungumza maadili hatuwezi kuyatenganisha na suala la kughushi vyeti au nyaraka mbalimbali. Kuporomoka kwa maadili ni pamoja na kuwapo genge kubwa mno la wachonga mihuri na vyeti feki.
Kwa miaka mingi, tumelalamika kuwa kuna watu walioshika nyadhifa kubwa kubwa ilhali wakiwa hawana sifa stahiki. Tumelalamika kuwa kundi kubwa la vijana waliosoma kwa taabu liko mitaani likiwa halina kazi. Haiwezekani matatizo na malalamiko yote haya tukawa tumeyasahau muda huu mfupi ambao Rais Magufuli ameutumia kuyashughulikia.
Tulipolia na kuomba Mungu atujaalie kumpata kiongozi mkuu wa nchi mwenye kuweza kuirejesha nchi hii kwenye mstari, tulikusudia kumpata kiongozi anayezungumza na kutenda.
Tunapoomba hawa 10,000 waonewe huruma, basi tuwaonee huruma na majambazi walioiba na kuua, ambao kwa sasa wamefungwa magerezani. Tuwaonee huruma na wengine wote waliofanya makosa mbalimbali. Hilo haliwezekani.
Wapo wanaosema ingekuwa vyema hawa 10,000 wakaachwa wang’atuke kwa mujibu wa sheria. Huruma ni jambo jema kwa kiongozi au uongozi wowote, lakini maslahi mapana zaidi ya nchi yanaufanya uongozi uwe na roho ngumu ili kujenga misingi ya uadilifu katika nchi.
Kuijenga nchi ni kama kujenga nyumba. Wengi, hasa wale wenzangu wa kudunduliza fedha, wanatambua kuwa ujenzi wa nyumba huanza ‘leo’. Hakuna nyumba inayojengwa kwa hisia, bali kwa kuamua kuanzia ‘sasa’ na ‘leo’.
Vivyo hivyo, kama nchi, sharti tuwe na mahali pa kuanzia. Tunaweza kuyumba kwa hatua zinazochukuliwa, lakini kuyumba huko ni kwa muda tu. Tunayumba kwa kuwakosa walimu. Tutayumba kwa kupungukiwa na wauguzi. Tutapata shida za hapa na pale kwa siku kadhaa kwa kukosa watumishi wengine kwenye sekta kadha wa kadha, lakini ukweli ni kuwa muda si mrefu tutarejea tena kwenye uimara wetu.
Bahati nzuri nchi hii haina uhaba wa wataalamu. Wapo wengi kweli kweli. Wale waliouona umati wa vijana zaidi ya 70,000 walioomba kazi zisizozidi 100 za Idara ya Uhamiaji, watakiri kuwa nchi hii haina uhaba wa watu wenye sifa za kuziba mapengo kazini.
Hatuwezi kuendelea kuwa nchi ya watu wanaoishi kwa kutengeneza vyeti feki wakiwa na mamia ya mihuri kuanzia ya mtendaji wa kitongoji hadi ofisi ya rais. Haiwezekani.
Nchi yetu ilishafika mahali ambako mtu anayeishi kwa uadilifu alionekana mjinga au aliyelaaniwa! Aliyeishi kwa uadilifu alionekana mzigo hata kwa ndugu zake. Wenye heshima wakawa ni wale waliotumia njia za mkato kujipatia ukwasi hata kama hawakuwa na sifa za kuwawezesha kuwa hivyo.
Tukafika mahali ambako Tanzania ikawa kupata hati ya kuzaliwa au hati ya kusafiria si jambo la kuhangaika, hasa kwa mwenye fedha. Udhaifu huo ukaifanya hati ya kusafiria ya Tanzania iwe moja ya hati za kuogopwa sehemu nyingi duniani. Watu wa mataifa yenye matapeli kama vile Nigeria wakamiminika kupata hati zetu na kuendesha vitendo vichafu duniani. Matokeo ya hali hiyo yamekuwa kuchafuliwa kwa jina zuri la nchi yetu.
Wageni wengi tumeona wakiingia na kuishi nchini kama Watanzania. Wamekuwa wakipata huduma zote na kuwafanya Watanzania wenye nchi wawe hohehahe katika nchi yao.
Bahati mbaya wananchi nao kwa kuona vitendo vya watumishi wa umma na dola, wakakata tamaa. Wakawa hawako tayari kuwaficha wahalifu bila kujali kama hatua hiyo ni hatari kwa usalama wao na usalama wa nchi.
Tunayasema haya si kwa sababu ya kushangilia yanayowapata wenzetu, la hasha! Tunayasema kwa sababu hata dini na mila zetu zinatutaka tuishi kwa uadilifu. Si hivyo tu, bali tunapaswa kuitambua dhamira njema ya Rais Magufuli katika suala zima la kuirejesha nchi kwenye mstari.
Tunapaswa kutambua na kuheshimu nia nzuri ya Rais Magufuli na wasaidizi wake, ya kuona Tanzania inakuwa nchi ya watu waliostaarabika na wanaojitambua. Hili la uadilifu halina mjadala kwa sababu ulimwengu huu wa teknolojia – tutake tusitake – ni lazima tubadilike.
Tunapotakiwa tuwe na TIN, nasi tukakubali kupigwa picha na kuweka alama za vidole, maana yake tunakubali kuingia kwenye maisha ya uadilifu. Tunaposajili simu za mkononi na baadaye kuchukuliwa alama za vidole na picha, maana yake ni kubwa zaidi ya hiyo simu au kadi ya simu tunayopata. Haya na mengine yanatufanya tusiwe na njia ya kukwepa pale mkono wa sheria unapotuhitaji. Maana yake nini? Maana yake ni kuwa maisha ya ujanjaujanja yanaelekea tamati.
Sisi tunaoyaona mambo haya sasa hatuna budi kuziandaa familia zetu ili zisije zikakumbana na mikasa ya aina hii.
Pamoja na hayo, utaratibu huu wa uhakiki wa vyeti kuwaacha wanasiasa ni bahati mbaya kweli kweli. Wanasiasa japo tunaambiwa si watumishi wa umma, bado ndiyo wenye kutoa uamuzi kwa masuala mbalimbali ya kijamii na kwa Taifa. Kwa kweli haileti mantiki kuona dereva akiwa na kiwango cha elimu kinachomzidi mkuu wa mkoa!
Kama Serikali ya Awamu ya Tano imeamua kupambana na UDANGANYIFU, ifanye hivyo bila kuwa na ‘DOUBLE STANDARDS’. Endapo kutajengwa tabaka “la wa kushughulikiwa”, na jingine “lisilo la wa kushughulikiwa”, mengi mema yanayofanywa na Serikali yatapuuzwa. Hakuna dhambi inayokuwa dhambi kwa mtu fulani na isiwe dhambi kwa mtu mwingine. Dhambi ni dhambi bila kujali imetendwa na nani. Wenye mamlaka walitafakari hili maana huku mitaani mtazamo wa wananchi ni kwamba kuna vimelea vya kulindana miongoni mwa wanasiasa.
Kwa yote hayo, bado naiona dhamira njema ya Rais Magufuli katika kuirejesha nchi kwenye mstari. Bila shaka tatizo analokumbana nalo ni kuwa karibu kila mahali kumeharibika, na kwa maana hiyo mzigo anaokabiliana nao ni mkubwa mno. Kama yupo ambaye hajamwelewa hadi sasa, basi huyo atakuwa na lake jambo. Tumuunge mkono.