adolf-hitlerKiongozi wa Chama cha Kisoshalisti kilichojulikana kama ‘NAZI’, Adolf Hitler (1889-1945) alikuwa mmoja wa madikteta dhalimu na wenye nguvu kuwahi kutokea katika karne ya 20. 

Baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia mbabe huyo aliamka kwa nguvu kupitia chama hicho cha Wafanyakazi wa Ujerumani na kuchukua udhibiti wa Serikali ya Ujerumani mwaka 1933.

Hitler aliamuru uanzishwaji wa kambi za mateso dhidi ya Wayahudi na makundi ya watu wengine, huku akiamini kuwa kufanya hivyo ilikuwa chachu na tishio tosha dhidi ya ukuu wa himaya ya Aryani, na hatimaye kusababisha vifo vya zaidi ya Wayahudi wapatao milioni Sita.

Mashambulizi ya Ujerumani dhidi ya nchi ya Poland mwaka 1939 ndiyo yaliyoanzisha Vita Kuu ya Pili ya Dunia ambapo mpaka kufikia mwaka 1941 Ujerumani iliteka sehemu kubwa ya ardhi ya Ulaya na Afrika Kaskazini. 

Ili kuepuka kukamatwa kwa kukwepa utumishi katika jeshi la Austria-Hungary, Adolf Hitler aliondoka kutoka Vienna na kuelekea Munich Mei 1913 lakini baadaye alilazimika kurejea.

Taarifa za kihistoria zinasema kuwa kiongozi huyo wa Nazi alijiunga na Jeshi la Bavaria na kuanza kufanya kazi za kujitolea, ambapo mwaka uliofuata alishiriki kikamilifu katika Vita ya Kwanza ya Dunia akiwa mstari wa mbele upande wa Magharibi ambako uzoefu wake katika vita na mapambano uliathiri mawazo, fikra na mitazamo yake yote baada ya hapo.

Baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia, Hitler alichukua udhibiti wa chama hicho cha Wafanyakazi wa Ujerumani kama kiongozi, hivyo alidhani kingemwezesha kushika dola ya Ujerumani punde si punde.

Aliposhindwa kwenye jaribio la mapinduzi la mwaka 1923, yeye na wenzake walikamatwa na kufungwa jela na baada ya kutokajela alijitahidi kukijenga chama hicho na kuanza mikakati ya kukamata dola kwa njia zilizo halali.

Hitler alikusudia kufanya mageuzi na kuendesha sera za kibaguzi, ambazo zingetoa nafasi ya kutosha kwa Wajerumani kuweza kuishi katika himaya kubwa duniani.

Kwanza alitabiri ingekuwa rahisi kuiteka Czechoslovakia, na kufuatiwa na Ufaransa ambayo ilikuwa kizingiti kigumu kwa wakati huo na hatimaye kumalizia na nchi ya Uingereza. 

Kwa mujibu wa mikakati ya Adolf Hitler, vita ya tatu ingefuata juu ya uvamizi dhidi ya Jumuiya ya Kisovieti ambayo kwake ulikuwa ni mtihani ambao alipanga afaulu kwa kufikiri vita ingepiganwa kwa haraka na kwa urahisi. 

Kwa fikra zake za kuipiga Urusi, hii ingempa utajiri wa malighafi za kutosha hususan mafuta ambayo yangemwezesha kuandaa mkakati wa maandalizi ya vita ya nne dhidi ya Marekani. 

Vita hiyo ingekuwa rahisi tu kwake endapo Ujerumani ingeweza kuwa na ndege ziwezazo kusafiri masafa marefu pamoja na meli za kivita na kwa upande mwingine ndege za kutosha na jeshi la maji kubwa na imara lingemwezesha kumkabili adui kokote aliko bila umbali kuwa kikwazo.

Mara baada ya Hitler kuingia madarakani mwaka 1933, maandalizi ya Ujerumani kijeshi yalianza kufanyika, hivyo mkazo na mkakati wa muda mfupi ulikuwa kutengeneza silaha kwa ajili ya vita dhidi ya mataifa ya Magharibi, na mkakati wa muda mrefu ulikuwa juu ya uzalishaji wa silaha nzito kwa ajili ya vita dhidi ya Marekani.

Mnamo mwaka 1938, Hitler aliachana na mpango wa uvamizi wa kijeshi dhidi ya Czechoslovakia na kuangalia zaidi makubaliano ya amani na kiongozi wa nchi hiyo, ambayo yalifanyika mjini Munich na hilo lilikuwa kosa lake baya na kubwa kuwahi kulifanya. 

Alipoamua kuigeukia Ufaransa na Uingereza, Hitler hakuweza kuishawishi Serikali ya Poland kujiunga na kuwa sehemu ya himaya ya Ujerumani kwa njia za amani ili kuhakikisha hali ya utulivu inakuwapo katika mashariki ya Ulaya, hivyo alichukua uamuzi wa kuivamia na kuiharibu Poland kabla ya kuanza kuzikabili nchi za Magharibi.

Uvamizi wa nchi ya Poland ulikusudiwa kufanyika ifikapo Septemba 1, 1939 lakini ili kufanikisha azma yake hiyo na ushindi wa haraka juu ya Poland kwa kuvunja kila aina ya kikwazo mbele yake, alikusudia kuiingiza Ujerumani katika makubaliano na Urusi ili mwisho wa siku iwe rahisi kwake kuzivamia nchi za Magharibi bila pingamizi lolote baada ya Poland.

Hali kadhalika, Hitler alikusudia kufanya uvamizi dhidi ya mataifa ya Magharibi katika msimu wa baridi mwishoni mwa mwaka 1939, lakini hali mbaya ya hewa ilikuwa ni kikwazo kikubwa ambacho kingeathiri jeshi lake la anga, kwa hiyo  aliamua kuahirisha mpango huo na kuhamishia uvamizi huo ifikapo mwanzoni mwa mwaka 1940 katika majira ya joto. 

Kutokana na ushauri alioupata kutoka kwa Kamanda Mkuu wa Vikosi vya Wanamaji, Admiral Erich Raeder, juu ya kuivamia na kuiteka Norway ili kuwezesha upatikanaji wa njia rahisi kwa jeshi lake la maji katika Bahari ya Atlantiki kuelekea Kaskazini, aliivamia Norway Aprili 1940.

Baada ya kupokea ushauri tena kutoka kwa Kamanda Mkuu, Erich Von Manstein, lengo la uvamizi kuanzia Kaskazini lilibadilishwa na kuamua kupanga mashambulizi kuelekea nchi zilizoko Kusini mwa Ulaya kwa lengo la kuzuia misaada ya kijeshi kutoka majeshi washirika (allied forces) kuelekea nchi za Ubelgiji na Uholanzi. 

Mkakati mpya wa Hitler kwa mara ya kwanza ulionekana kufanya kazi wakati jeshi la Ujerumani lilipofanikiwa kuvunja mstari wa ulinzi wa jeshi la Kifaransa na kufanikiwa ndani ya siku kumi kufika kwenye mkondo wa pwani nyuma ya vikosi vya majeshi washirika. 

Baada ya kuonekana wazi kuwa majeshi washirika yaliyokwama yanaweza kutoroka kipigo cha jeshi la Ujerumani, mwelekeo wa silaha na jeshi la Ujerumani ulibadilika tena, lakini jeshi hilo lilikwishachelewa kuweza kuzuia na kufanya mashambulizi dhidi ya askari wa maeshi washirika kwa sababu kikosi maalum cha jeshi la Uingereza na wanajeshi wa Ufaransa walifanikiwa kuokolewa na kutoroka. 

Pigo lililotokea mapema Juni 1940 lililosababisha anguko kwa mstari wa mwisho wa ulinzi wa jeshi la Ufaransa, lilikuwa ni ushindi kamili uliompa Hitler furaha na shangwe huku akijua anapata msaada wa kutosha kutoka kwa makamanda na majemedari wake wa kivita, ambao kila mara alikuwa akiwapandisha vyeo na kuwapa namna nyingine za rushwa kama sehemu ya kuwapa motisha ya kuendelea na mapambano.

Taarifa zinasema kuwa kwa sababu ilionekana kama vita hii ilikuwa imeisha baada ya Ujerumani kuiteka Ufaransa, Hitler alianza kupanga mipango mingine kwa ajili ya vita dhidi ya Marekani na Umoja wa Kisovieti. 

Julai 11, 1940 Hitler alitoa amri kuanza kwa ujenzi wa jeshi la maji ikiwamo ujenzi wa meli za kivita na ilipofika Julai 31, 1940 baada ya mkakati wa kutaka kuvamia Umoja wa Kisovieti katika msimu wa baridi wa 1940, kutokana na ushauri wa wanajeshi wake, Hitler aliamua kuishambulia Urusi katika majira ya joto mwishoni mwa mwaka 1941. 

Wakati Uingereza ikikataa kukubali kushindwa na kusalimu amri, Hitler alipanga kuchanganya hatua tatu ambazo zingehakikisha Uingereza inasalimu amri: kwanza kabisa, jeshi la anga la Ujerumani lingefanya uvamizi na kuharibu uwezo wa Uingereza kujitetea; pili Uingereza ingevamiwa ardhini iwapo kama isingejisalimisha, na tatu ushindi ambao ungepatikana dhidi ya Urusi ungeondoa uwezekano wa Uingereza kupata msaada wowote ule kutoka Urusi, hivyo kuangamia zaidi na kumaliza hatari yoyote dhidi ya Japan, ambayo ingehamasika kusafiri katika Bahari ya Pasifiki na kuivamia Marekani upande wa Magharibi.

Kwa upande mwingine Hitler alitaka Japan kujiunga katika vita na Uingereza na kuahidi kujiunga na Japan katika vita dhidi ya Marekani kama Tokyo ingeona umuhimu juu ya hilo, na hii ingekuwa njia nyingine kwa Ujerumani kupata kuimarisha jeshi la maji dhidi ya Marekani.

Kwenye kampeni dhidi ya eneo la Balkan, kiongozi huyo mbabe wa enzi hizo alikusudia kupata alichoamini kuwa ngome ya upande wa Kusini iliyokuwa katika hali tete, lakini hata hivyo aliona operesheni kubwa ya jeshi la anga katika eneo la Balkani ingekuwa ya gharama ya juu sana kutokana na ugumu wa eneo lenyewe na hivyo kutokusudia kufanya operesheni kama hiyo tena.

Ikumbukwe kuwa uvamizi wa Ujerumani dhidi ya Umoja wa Kisovieti ulianza Juni 22, 1941 ambapo hapo mwanzo uvamizi huo ulionekana kwenda kama ilivyopangwa, lakini ghafla kila kitu kilianza kwenda vibaya – vipigo vya kwanza ambavyo vilikusudia kuangusha Umoja wa Kisovieti ndani ya wiki chache havikuleta matokeo yaliyokusudiwa na hayakuweza kuwa na athari katika nchi hiyo, hivyo baada ya hapo, swali daima lilikuwa kwa Ujerumani ni sekta ipi nyeti na muhimu ishambuliwe ili kuidhoofisha Urusi na sekta gani iachwe.

Katika hali hiyo, Hitler alijikuta mara kwa mara akitofautiana na majenerali wake walioko mstari wa mbele katika kuamua mustakabali wa vita na baada ya vita kuonekana ikiielemea na kuigeukia Ujerumani hali ya kutofautiana kati ya makamanda wa Hitler ilizidi kuongezeka. 

Wakati jeshi la Ujerumani likiendelea kurudi nyuma, Hitler alikuwa daima na wasiwasi kuhusu hasara waliyokuwa wakiendelea kuipata ya watu, hali kadhalika ya uharibifu wa vifaa vyake vya kijeshi kwa hiyo baadhi ya majemedari kama Erwin Rommel na Walther Model, mara kwa mara walikuwa wanapingana na amri ya Hitler kwa kurudi nyuma wakati majenerali wengine walikuwa wakirudishwa  nyumbani kukusanya kiinua mgongo chao cha kila mwezi na kustaafu kwa kutofautiana na amri za kiongozi wao ingawa wengine walikuwa wakiendelea na kazi zao.

Hitler alifikiri kwamba kushindwa kwa Ujerumani katika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia kulitokana na anguko lililotokea katika ardhi ya nyumbani mbele na kwa hivyo kudhani kuwa uanzishwaji wa sera za kidikteta na mauaji ya kukusudiwa ya Wayahudi, ulikuwa uhakika wa ushindi wa vita dhidi ya majeshi washirika, na safari hii Hitler alipoona hana jinsi na majeshi washirika yameshaingia mjini Berlin huku yakiongozwa na Jeshi Jekundu la Urusi, Hitler alijaa hofu ya kisasi ambacho Warusi wangetoa dhidi ya Wajerumani, hivyo aliamua kumuoa mke wake na wote kwa pamoja kuamua kujiua muda mfupi kabla ya jeshi la Urusi kuwasili.