Leo ni Mei Mosi, Siku ya Wafanyakazi Duniani. Siwezi kukwepa taratibu za itifaki kwa kutoa salamu za pongezi kwa wafanyakazi wote kwa kuadhimisha siku hii muhimu kwetu sote leo.

Salamu maalumu napenda kuzitoa kwa wanahistoria kwa kazi kubwa wanayofanya ya kutafiti na kuandika historia yetu kwa manufaa ya vizazi vyote, vya sasa na vya baadaye. Lakini salamu mahususi kabisa nazitoa kwa wataalamu waliojumuika mjini Windhoek, Namibia, Apirili 24- 25 Aprili kujadili mikakati ya kukusanya taarifa juu ya historia ya vyama vya ukombozi vya Bara la Afrika.

 

Mkutano uliandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni (UNESCO) na kujumuisha wataalamu, wanazuoni, wanahistoria, na wadau wa historia kutoka sehemu mbalimbali kwa madhumuni ya kubaini mapengo ya taarifa za kihistoria ambazo zimeshakusanywa na kupanga mipango mipya ya kukusanya taarifa za kuziba mapengo hayo.

Vita ya ukombozi wa Bara la Afrika imepiganwa katika maeneo mbalimbali ya bara hili kuanzia miaka ya mwanzo ya 1960 hadi miaka ya 1980. Tanzania inatambulika kama nchi mojawapo ya Afrika iliyotoa mchango mkubwa katika kuunga mkono vyama vya ukombozi vya Bara la Afrika na hata vya maeneo mengine ambako harakati za mapambano dhidi ya ukoloni ziliendelea. Ni suala lililojitokeza mara kadhaa katika majadiliano ya mkutano.

 

Madhumuni ya mkutano yalikuwa mengi, lakini mojawapo ni kutambua kuwa sehemu ya historia hii ya ukombozi wa Bara la Afrika haijaandikwa na iko kwenye kumbukumbu za watu mbalimbali. Umeonekana umuhimu wa kuzikusanya hizi taarifa.

Ninayo kumbukumbu ya Mama Maria Nyerere ya jitihada zake binafsi za kuunga mkono harakati za ukombozi kwenye miaka ya 1970 alipochangisha na kukusanya misaada kununulia mbeleko zilizopelekwa kwenye kambi za wakimbizi za wapiganaji wa FRELIMO kusaidia kina mama walezi kubebea yatima waliokuwa kwenye kambi hizo.

Hakuwa peke yake. Matukio kama haya yalitokea maeneo mengi nchini. Kilichojitokeza wakati huo ni kuwapo kwa hamasa kubwa ya wananchi ya kuunga mkono harakati za mapambano.

Inakusudiwa kuwa kuboresha taarifa kama hizi kutaongeza ufahamu miongoni mwa raia wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) juu ya kuwepo kwa historia moja inayotuunganisha. Ufahamu huu utasaidia kupunguza aina ya matukio yaliyotokea Afrika Kusini miaka ya hivi karibuni ya kushambuliwa kwa raia wa nchi za Afrika wanaoishi nchini humo. Ufahamu wa historia utaimarisha misingi ya udugu na umoja.

Mfano mdogo lakini mzuri wa jinsi gani ufahamu wa taarifa unaweza kuchangia kulinda usalama wa watu ni simulizi ya mwanasoka mashuhuri wa Rwanda ambaye alinusurika kuuawa wakati wa vita ya kimbari ilivyopamba moto nchini mwake mwaka 1994. Maisha yake yalisalimika kwa sababu tu mmoja wa wauaji aliyekuwa shabiki wa timu aliyochezea mchezaji huyo alimtambua na kuamua kumuacha salama.

Lakini kama ambavyo vita ya ukombozi haikuwa rahisi, vita ya kueneza historia hii muhimu nayo inabeba changamoto kubwa. Vijana wa siku hizi hawathamini au hawatambui umuhimu wa historia. Wanataka kusikia kuna mbinu gani mpya za kuboresha kipato chao; wanataka kujiongezea maarifa ya kutajirika, siyo kufahamu Mama Maria alichangia khanga ngapi kwa yatima wa FRELIMO.

Tatizo lingine lililojitokeza ni kuwa vijana wa siku hizi hawapendi kusoma, na kwa bahati mbaya Facebook na Twitter hawana muda wa kutoa taarifa za historia ya ukombozi wa Bara la Afrika. Mchapishaji wa vitabu na mshiriki wa mkutano, Walter Bgoya, alisema kuwa hata wale wanaopendelea kusoma vitabu hawataki kusoma vitabu vikubwa sana. Baadhi yao wanasema vitabu vikubwa vinawatia uvivu kusoma.

Kwa hiyo changamoto ya mwanzo kabisa itakuwa jinsi ya kubuni mikakati itakayowasilisha taarifa zilizoboreshwa za historia ya vyama vya ukombozi na kuzifikisha kwa vijana kupitia njia ambazo wao wanazitumia kupata taarifa. Badala ya kushindana na Facebook na Twitter, mkutano umeona umuhimu wa kutumia mikondo inayotumiwa na vijana kuwapatia taarifa za kihistoria zitakazokusanywa.

Pamoja na kutambua tatizo hili, ipo pia mikakati ya kuchapisha vitabu kwa rika la watoto, vijana, na watu wazima.

Mkutano umejadili na kutukumbusha kuwa sisi ni wamoja, ya kwamba tunayo historia iliyotukuka inayotuunganisha, na upo wajibu usiokwepeka wa kuirithisha historia hiyo kwa kizazi cha sasa ili kiweze kuitumia kama msingi wa kujenga umoja wa kikanda, na umoja wa watu wa Bara la Afrika.

Umoja uliokuwapo enzi hizo ulikuwa wa dhati, na ndiyo uliwezesha nchi za Afrika, kwa jitihada zake za pamoja na kuongezea misaada kutoka nchi rafiki, kupambana na mataifa makubwa yenye nguvu yaliyotetea uwepo wa tawala za kibaguzi za Rhodesia, Ureno, na Afrika Kusini.

Kusahau historia hii kunadhoofisha umoja wetu na kuathiri pia malengo yetu ya kujenga umoja imara miongoni mwa Waafrika.

Mkutano wa Windhoek unaweza kufananishwa na ukuta mmoja wa nyumba ya umoja inayojengwa na Bara la Afrika. Cha msingi ni kuwa malengo ya mkutano yanachangia kufikiwa kwa visheni na matarajio ya Ajenda 2063 ya Umoja wa Afrika juu ya Afrika Tunayoitaka.

Miongoni mwa masuala mengine yaliyotajwa kwenye Afrika Tunayoitaka ni uwepo wa Waafrika – barani Afrika na wale wa diaspora (nje ya bara) ambao ni wamoja, na wenye ufahamu thabiti wa historia yao. Muhimu pia, ni watu wanaotambua kuwa Afrika inapaswa kuungana ili kufanikisha kuleta maendeleo kwa watu wake.

Historia ya mapambano ya vyama vya ukombozi vya Bara la Afrika na mafanikio yaliyopatikana na mapambano hayo ni moja ya matukio muhimu kabisa katika historia ya Bara la Afrika. Ni jambo muhimu sana kuwa UNESCO inafanya jitihada za kuikamilisha historia hiyo ili iweze kuwa nyenzo kwa vijana wa sasa kuendelea kulinda na kuimarisha uhuru uliopiganiwa na vijana waliowatangulia.

 

.tamatiā€¦