Juma liliopita nimeongozana na ugeni kutoka baadhi ya nchi za Kusini mwa Afrika – Namibia, Zimbabwe, Msumbiji, na Zambia –sehemu ya wajumbe wa bodi ya Southern African Research and Documentation Centre (SARDC), kituo cha utafiti kilichopo Harare kinachofanya kazi kwa karibu sana na Sekretariati ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kwenye ziara yao nchini. Mimi ni mjumbe wa bodi ya SARDC.
SARDC iliundwa mwaka 1985 wakati harakati za ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika zimepamba moto na moja ya majukumu yake yalikuwa kufichua njama za utawala wa kibaguzi wa Afrika Kusini wa kuhujumu ukanda huo wa Afrika, hasa zile nchi zilizokuwa zikiunga mkono harakati za ukombozi.
Leo hii SARDC ni kituo kinachoendesha utafiti na kuchapisha matokeo ya tafiti za kitaaluma juu ya ukanda huu pamoja na miongozo ya kisera inayolenga kuimarisha umoja na ushirikiano wa kikanda katika masuala ya matumizi ya maji, miundombinu, nishati, mazingira, na jinsia.
Mwenyekiti wetu Profesa Peter H. Katjavivi pia ni Spika wa Bunge la Namibia. Amefafanua vyema sababu ya ziara ya SARDC nchini na uamuzi wa kufanya kikao cha bodi kijijini Butiama.
Kwanza ni kumuenzi Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakati huu wa kumbukizi ya miaka 20 tangu afariki dunia. Mwalimu alikuwa mdhamini wa kwanza wa SARDC.
Lakini, na pengine muhimu zaidi, ni kuenzi mchango mkubwa wa Mwalimu Nyerere na nchi ya Tanzania kwenye jitihada za kuleta uhuru wa nchi nyingi za Kusini mwa Afrika.
Mwalimu alikuwa Mwenyekiti wa Nchi za Mstari wa Mbele pamoja na muasisi wa jumuiya ya SADC na Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) iliyounda Kamati ya Ukombozi ambayo makao yake yalikuwa jijini Dar es Salaam.
Nafasi zote hizi ziliipa Tanzania nafasi muhimu katika kuchangia na kuongoza mapambano dhidi ya tawala za kibaguzi zilizoshikilia makoloni ya Ureno barani Afrika, na dhidi ya tawala za kibaguzi zilizokandamiza wananchi wa Afrika Kusini, Msumbiji, na Namibia.
Profesa Katjavivi anakumbuka safari iliyomtoa Namibia mwaka 1962 na, akisafiri kwa usiri mkubwa na mwenzake kutoka Afrika Kusini, jinsi walivyofanikiwa hatimaye kufika kwenye nchi huru ya Kiafrika iliyokuwa jirani wakati huo: Tanganyika. Alifikia Mbeya na baadaye akafanya kazi Tanganyika na Tanzania kama Katibu wa Mwakilishi wa SWAPO, chama kimojawapo kilichoongoza mapambano ya silaha na kufanikisha kuipa Namibia uhuru wake Februari 9, 1990.
Historia ya ukombozi wa Bara la Afrika si historia ya nchi moja tu kwa sababu ni historia ambayo ina muingiliano mkubwa kati ya watu wa nchi ambazo zilishiriki kwenye ukombozi huo. Ni historia ambayo inashirikisha pia watu na nchi nje ya Bara la Afrika.
Lakini ni historia ambayo haiheshimu mipaka kwa sababu, mathalani, nchini Tanzania na hasa kwa sababu ya nafasi ya Tanzania katika historia hiyo, tunayo maeneo mengi ambayo yamebeba historia ya Afrika Kusini, Namibia, Msumbiji, Angola na maeneo mengi ya bara letu.
Uamuzi mwingi muhimu wa harakati zile ulipitishwa Dar es Salaam. Viongozi wengi wa vyama vya ukombozi waliishi Tanzania, na hurudi kutafuta kumbukumbu za kihistoria za nyakati hizo. Si rahisi kuzipata hizo kumbukumbu.
Akiwa Dar es Salaam, Profesa Katjavivi aliomba kutembelea baadhi ya majengo yaliyokuwa na ofisi za vyama mbalimbali vya ukombozi. Tulianzia kwenye jengo lililokuwa na ofisi za African National Congress (ANC)na alipata fursa ya kutembelea zilipokuwa ofisi za chama cha ukombozi wa Angola, MPLA.
Pamoja na kwamba alishapewa taarifa kuwa jengo lililokuwa na ofisi ya chama chake cha SWAPO ilikuwa limeshabomolewa, tulitembelea eneo lile. Ni kwenye Mtaa wa Kaluta, katikati ya Jiji la Dar es Salaam. Sasa hivi ni sehemu ya maegesho ya magari ya jengo kubwa ambalo lipo kwenye Mtaa wa Samora.
Hatuthubutu kuuliza ni maswali gani ambayo kiongozi mwandamizi wa SWAPO aliyefika Tanganyika kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 21 tu, lakini mwenye kumbukumbu makini kabisa juu ya kipindi ambacho aliishi nchini atakuwa nayo juu ya uamuzi wa kubomoa sehemu ya historia ya nchi yake.
Mahala ambako angeondoka na historia ya ofisi ambamo alifanya kazi amefanikiwa kuondoka na picha za uzio wa mabati ya maegesho ya magari ambayo mama lishe wanayatumia kuhudumia wateja wao.
Tunapozungumzia suala la ukombozi, historia ya Namibia si historia ya nchi hiyo pekee, ni historia yetu sote. Ni rahisi sana kwa rika la sasa kusahau –na kusahau huku kunarahisishwa na kupunguzwa kwa vielelezo vya kihistoria kama ofisi ya zamani ya SWAPO – uhusiano wa muda mrefu na wa kihistoria uliopo baina ya watu wa ukanda huu wa Afrika.
Na muhimu sana kulinda historia ya SWAPO na Namibia kama ambavyo ni muhimu kulinda historia ya Mkwawa na Kinjeketile.
Kwa bahati mbaya sana hoja ya kutunza majengo ya kihistoria inazidiwa nguvu na vigezo vya faida. Historia haiingizi pesa benki. Jengo jipya linafanya hivyo.