Wiki iliyopita katika makala hii inayomhusu mwasisi wa Siku ya Wapendanao, Mtakatifu Valentino, iliishia pale ambapo katika kila barua aliyokuwa anaandika aliweka maneno
“Ndimi Valentino wako.”
Maneno hayo yakawa ni kielelezo cha upendo wa Mtakatifu Valentino kwa watu wote kuwa yeye aliishi na kufa kwa ajili ya kuwapenda watu wote kama Kristo alivyosema: “Amri yangu ndiyo hii: Mpendane kama nilivyowapenda ninyi. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.” (Yoh. 15:12-13)
Mtakatifu Valentino ametuachia urithi mkubwa wa imani, anatufundisha kuwa fadhila ya upendo ni kielelezo cha imani. Mtu yeyote mwenye imani humpenda Mungu na huwapenda wenzake.
Kipimo cha imani na kipimo cha utu ni upendo. Dunia inahitaji sana upendo ili mambo mengine mazuri yawezekane. Mtakatifu Valentino alitambua kuwa watu wa familia wanapopendana jamii yote itapendana na kuishi kwa amani.
Anatufundisha kuwa upendo huanzia nyumbani, yaani kati ya wanafamilia. Ndiyo maana aliwataka watu wa ndoa wapendane katika misingi ya imani na wafunge ndoa takatifu. Leo hii watu wengi duniani pote wanaikumbuka tarehe 14 Februari kuwa ni Siku ya Wapendanao. Je, wanatambua kwa nini Valentino alitoa uhai wake siku hiyo?
Tunatakiwa tupendane kwa upendo wenye msingi katika imani kama alivyofundisha Mtakatifu Valentino. Siku ya Mtakatifu Valentino ni Siku ya Wapendanao katika misingi ya imani na utu.
Kwa bahati mbaya watu wengi katika maisha ya leo tunapendana katika misingi ya tamaa za kimwili na kimapato. Leo hii kuna watu wengi wa ndoa ambao wana nyumba ndogo lakini nao wanasema eti leo ni siku yao ya wapendanao.
Ni upendo gani huo wenye nyumba kubwa na ndogo? Je, Valentino hakufa kwa kupinga jambo hilo? Vijana wengi leo wanaishi uchumba sugu bila kufunga ndoa, lakini wao wanasema eti leo ni siku yao ya wapendanao.
Upendo gani huo pasipo msingi wa imani? Je, Valentino hakutoa uhai wake ili kuwafundisha na kuwapigania vijana wafunge ndoa takatifu? Ni ajabu kuwa siku ya Mtakatifu Valentino uovu mwingi dhidi ya upendo ndiyo hufanyika.
Ni vema siku hii iwe kwa ajili ya kujikumbusha maana halisi ya upendo. Wakati ule Mtakatifu Valentino alikwazika sana kuona watu wanaishi pamoja bila kufunga ndoa, alikwazika kuona vijana na watu wa ndoa wanakosa uaminifu katika ndoa zao.
Alisikitika kuona hata vijana wanakosa haki za kuuishi upendo wa ndoa, lakini akija leo hii, Mtakatifu Valentino atashindwa hata kushangaa kuona jinsi upendo ulivyogeuzwa kuwa ni starehe ya kimwili badala ya kuwa ni fadhila ya kimungu.
Mbaya zaidi, atakutana na watu wa jinsia moja (ushoga na usagaji), wanaodai wanapendana na wana haki ya kufunga ndoa. Mtakatifu Valentino anatukumbusha tena kuwa upendo ni fadhila ya kimungu na si starehe ya kimwili. Tafakari njema.