“Upendo huvumilia, Upendo hufadhili, Upendo hauhusudu, Upendo haujivuni, Upendo haukosi kuwa na adabu, Upendo hauhesabu mabaya, Upendo haufurahii udhalimu, Upendo hautakabari, Upendo hustahimili yote.’’ – (1Kor 13:113).
Februari 14, dunia nzima inasherehekea Sikukuu ya Wapendanao, ijulikanayo kama ‘Valentine’s Day’. Ningependa leo tufahamu sote asili ya sikukuu hii. Mwanzilishi wa sikukuu ni padri wa Kanisa Katoliki ambaye Kanisa Katoliki linamheshimu kama mtakatifu.
Mtakatifu Valentino alikuwa ni Padri wa Roma (Italia), ambaye aliishi kwa kuishuhudia imani ya Kikristo kati ya mwaka 197 na 273. Kanisa linamtambua kuwa ni shahidi wa imani kwa kuwa alitoa uhai wake kwa kuilinda, kuitetea na kuitangaza imani ya Kikristo.
Lakini pia Mtakatifu Valentino anajulikana duniani kote kuwa ni mtakatifu wa wapendanao. Kwa hiyo utakatifu wake katika historia ya kanisa na umaarufu wake duniani kote ni mambo mawili yanayojikita katika jambo moja la msingi kwa maisha ya mtu wa dini yoyote na mahali popote, jambo hilo ni imani.
Valentino aliongoka katika ujana wake na kubatizwa mwaka 197 na baadaye akawa padri kwa kuishi imani ya Ukristo mpaka mwaka 273 alipouawa kwa ajili ya kutetea imani ya Kikristo.
Imani hiyo ya Kikristo aliishi si tu kwa maneno bali pia kwa vitendo, kwani wakati ule kuwa Mkristo lilikuwa ni jambo gumu sana.
Ugumu huo ulitokana na ukweli kwamba watawala wa Kirumi wa nyakati hizo walikuwa bado hawajaipokea imani ya Kikristo.
Valentino aliishi imani yake ya Kikristo nyakati za Mfalme Claudio, ambaye mara kadha alimtesa na kumfunga gerezani na baadaye aliuawa kwa amri ya Mfalme Aureliano, huyu alikuwa ni mfalme katili sana na watu walimwita jina la ‘Nero wa Pili’.
Mtakatifu Valentino anatambuliwa na wengi duniani pote kwa sababu ya upendo wake kwa watu. Tabia yake ya kupenda watu ilijikita katika imani yake kwa Neno la Yesu. “Amri yangu ndiyo hii: Mpendane kama nilivyowapenda ninyi. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.” (Yoh. 15:12-13).
Mtakatifu Valentino alitumia muda wake mwingi kuwasaidia watu wa ndoa na vijana wachumba – kwa kuwafundisha juu ya upendo. Aliwafundisha kuwa upendo ni fadhila kuu ya Kikristo na kiutu, kwa hiyo alisisitiza kuwa upendo ni kielelezo cha imani na utu.
Watu wa ndoa aliwafundisha kuwa upendo wao hujionyesha katika mambo makuu mawili; uaminifu na umoja. Uaminifu wa viapo vya ndoa katika kupendana na kuheshimiana siku zote na kwa hali zote. Umoja katika kutambua kuwa ndoa ni kati ya mume mmoja na mke mmoja.
Mtakatifu Valentino aliishi nyakati ambazo ndoa za mume mmoja na wake wengi zilikuwa ni kama jambo la kawaida. Wanawake walinyimwa upendo ndani ya ndoa zao na wakawa wanyonge mbele ya waume zao.
Yeye alikemea jambo hilo bila kujali mtu yeyote; watawala kwa mfano, walikuwa pia na tabia hiyo ya kukosa uaminifu kwa ndoa zao. Polepole watu wengi walianza kujirekebisha na upendo ukaanza kurudi ndani ya ndoa. Hata hivyo Mfalme Claudio alimchukia Valentino na kumfunga gerezani.