Historia ya matibabu ya saratani ya aina yoyote hapo kabla, watu ambao wamewahi kuwa na aina nyingine za saratani hapo awali, na wakati wa matibabu wakapewa tiba ya mionzi, dawa kali za saratani, wapo katika hatari kubwa ya kupata ugonjwa huu wa leukemia.

Kupigwa na kiasi kikubwa cha mionzi: 

Watu ambao wamewahi kupigwa mionzi, wana hatari kubwa ya kupata aina yoyote ya saratani ikiwamo saratani hii ya damu.

Kuwa na magonjwa mengine ya damu: 

Saratani ya aina hii inahusika zaidi kwenye seli za damu na damu yenyewe, hivyo ina uhusiano mkubwa na magonjwa ya damu ambayo mtu aliugua kabla.

Kutumia au kupigwa na baadhi ya kemikali: 

Watu ambao wamewahi kukumbana na kemikali kama vile benzene au zile zinazotumika kwenye viwanda kuyeyushia na kutengeneza magurudumu au vifaa vikubwa vya plastiki, nao pia wamo kwenye uwezekano kupata saratani ya damu.

Kuwa na historia ya ugonjwa huu katika familia: 

Ni watu ambao  wazazi wao pia wana uwezekano mkubwa wa kupata ugonjwa huu wa leukemia. Hata hivyo, hii haina maana kwamba leukemia inaambukizwa isipokuwa kuna uhusiano wa kifamilia tu katika kusababisha ugonjwa huu.

Uvutaji wa sigara: 

Uvutaji wa sigara umethibitika kuwa ni kitendo hatarishi sana cha leukemia inayoenea kwa kasi (acute myeloid leukaemia), sumu iliyopo kwenye moshi wa sigara – nikotini – huingia kwenye njia za damu na kuenea katika sehemu mbali mbali za mwili.

Hata hivyo ifahamike kuwa wapo watu wengi ambao wamewahi kukumbana na vihatarishi nilivyovieleza hapo juu bila kupata ugonjwa huu wa leukemia, kadhalika wapo waliopata leukemia bila kukumbana na kihatarishi hata kimoja kati ya hivi. 

Dalili za ugonjwa wa leukaemia

Kama ilivyo kwa magonjwa mengine hususani ya saratani, leukaemia pia ina dalili nyingi, lakini zifuatazo ndizo dalili kuu:

• Uchovu na matatizo ya kupumua ambayo hutokana na na uchache wa seli nyekundu za damu. 

• Maambukizi  na magonjwa ya mara kwa mara ambayo yanatokana na uchache wa seli nyeupe za damu.

• Kuvuja damu ambako kunasababishwa na uchache wa ile aina ya tatu ya seli za damu inayoitwa platelets ambayo kazi yake kubwa ni kuzuia damu isiendelee kutoka pale panapoashiria kuwa na hali ya uvujaji damu. 

Uvujaji huu wa damu unaweza kutokea kupitia pua, fizi za kwenye meno ambazo huwa zinatoa damu kirahisi, majeraha madogo madogo sana yaliyopo kwenye ngozi ambayo wakati mwingine hutokea kwa mikwaruzo au kujikuna sana.

Seli za leukemia katika ubongo zinaweza kusababisha maumivu makali ya kichwa, kutapika, au kupunguza uwezo wa kuona vizuri na zile za bone marrow zinaweza kusababisha maumivu ya mifupa na maungio katika mwili.

Uchunguzi na vipimo vya ‘leukemia’

Vipimo vya damu vya kawaida kama vile kupimwa damu ka ujumla (the complete blood cell count) ni kidhihirisho cha awali kabisa kwamba mgonjwa ana leukemia. 

Kupitia kipimo hicho, seli nyeupe za damu zinaweza kuonekana zimepungua, au zipo kwenye idadi ya kawaida au zimeongezeka; lakini idadi ya seli nyekundu za damu na zile seli za vigandishi damu yaani platelets mara zote kipimo hiki huonesha zimepungua sana. 

Muhimu zaidi, zile sampuli za seli nyeupe za damu zilizochanga baada ya kuzalishwa (blasts), zinaweza kuonekana kupitia kifaa cha uchunguzi kinachoitwa hadubini (microscope) kwa lugha ya kisayansi. 

Kwa kuwa sampuli hizo huwa hazionekani kabisa kwenye damu, tathmini ya uwepo wake ni muhimu sana ili kuweza kuchunguza ugonjwa huu wa leukemia.

Kipimo cha supu ya mifupa (bone marrow biopsy) hufanyika pia kwa ajili ya kuchunguza uwezo wa seli za saratani. 

Wakati mwingine kipimo hiki hufanyika ili kutambua kwa nini seli za damu hazipo kawaida. Sampuli za bone marrow kwa kawaida huwa zinachukuliwa katika mfupa wa paja. Mgonjwa huwa analala kwa ubavu mmoja, huku goti la mguu wa juu akiwa amelikunja. 

Baada ya kuzifuta vizuri tishu za ngozi, daktari anadunga sindano kwenye mfupa na kufyonza kiasi kidogo cha bone marrow. Kwa tafsiri nyingine hiki ndicho kipimo hasa kikuu cha kuchunguza ugonjwa huu wa leukemia.