Ni vema na haki kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa mema mengi anayotutendea na kipekee kumshukuru kwa zawadi ya uhai, maana ni kwa neema yake sisi tunapumua.
Vilevile ninamshukuru Mungu sana kwa taifa letu kusherehekea vizuri na kwa amani Uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara) uliopatika Desemba 9, 1961 wakati Bendera ya Waingereza ilipoteremshwa na kuipandisha Bendera ya Tanganyika.
Hata hivyo, Tanganyika iliungana na Zanzibar Aprili 26, 1964 na kuanzisha Jamhuri ya Muungano ya Tanzania (sasa miaka 55 ya muungano).
Historia inaonyesha kuwa Waingereza walitawala Tanganyika baada ya Vita ya Kwanza ya Dunia kumalizika Novemba 11, 1918. Kabla ya hapo eneo la Tanganyika lilikuwa chini ya utawala wa Wajerumani kama sehemu ya eneo la Afrika Mashariki lililojulikana kama German East Africa (Deutsch Ostafrica).
Baada ya Vita Kuu ya Dunia kumalizika mataifa yaliunda umoja uliojulikana kama ‘The League of Nations’ na chombo hiki kilitarajiwa kuleta umoja na kudumisha amani duniani. Kwa upande mwingine, sehemu iliyokuwa ikitawaliwa na Wajerumani iligawanywa, hivyo kuanzisha nchi tatu za Afrika Mashariki na kuwekewa mipaka ipasavyo.
Pamoja na Waingereza kuitawala Kenya kama koloni lao, pia walikabidhiwa madaraka ya kuisimamia Tanganyika kwa niaba ya umoja huo na mwaka 1922 (mwaka aliozalia Baba wa Taifa marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere) eneo ambalo Waingereza walikabidhiwa kulisimamia kwa niaba ya ‘The League of Nations’, wakaliita ‘Tanganyika’.
Mwaka 1939 ilizuka tena Vita ya Pili ya Dunia wakati Waingereza wakiwa bado wasimamizi wa Tanganyika. Vita ilikwisha mwaka 1945 na mataifa yakaanzisha Umoja wa Mataifa (United Nations-UN), Makao Makuu yakawa katika Jiji la New York, Marekani (USA).
Mabadiliko kutoka ‘The League of Nations’ kuwa Umoja wa Mataifa (UN) yalilenga zaidi kuwepo na nguvu ya pamoja katika kuhakikisha amani na usalama duniani. Wakati huo, Tanganyika iliendelea kuwa chini ya uangalizi wa Wingereza na kupewa hadhi ya ‘United Nations Trusteeship’ na jina kuwa ‘Tanganyika Territory’.
Wakati huo Kenya na Uganda zilibaki kuwa makoloni ya Waingereza. Pamoja na Tanganyika Territory kuwa chini ya uangalizi (trusteeship), bado Waingereza walitutawala kama koloni lao maana haikuwa rahisi kuiona tofauti kati ya uangalizi kwa mfumo wa ‘United Nations Trusteeship’ na mamlaka kamili ya kumiliki na kutawala (colonial administration).
Kiuhalisia Wajerumani walikalia ardhi ya Tanganyika kwa kipindi cha miaka 27, na Waingereza kipindi cha miaka 42; jumla miaka 69 taifa likiwa chini ya wakoloni.
Wakati Desemba 9, 2019 Tanzania ilisherehekea miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika katika Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza, tuna kila sababu ya kujivunia Uhuru wetu. Tunapolinganisha mafanikio yetu kwa miaka 58 na yaliyopatikana kwa miaka 69 ya ukoloni, kuna tofauti kubwa. Maendeleo makubwa yamepatikana ndani ya miaka 58 ya kujitawala. Baba wa Taifa, marehemu Mwalimu Julius Nyerere mwanzoni mwa uhuru alikuwa na kaulimbiu kama: Uhuru na Amani, Uhuru na Umoja, Uhuru na Kujitegemea, Uhuru na Kazi. Vilevile, alituasa kuwa hatutakuwa na uhuru kamili iwapo nchi jirani zitaendelea kutawaliwa na wakoloni. Kwa hali hiyo alimaanisha kuongeza nguvu katika harakati za ukombozi barani Afrika.
Ili kufanikisha hili, kwanza alikubaliana na marehemu Abeid Amani Karume kuunganisha Tanganyika na Zanzibar, hivyo kuzaliwa Tanzania. Baada ya mafanikio hayo muhimu na kwa namna ya pekee, jitihada zilifanyika tukaunganisha nguvu na kuanzisha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lenye nguvu kamili.
Isitoshe baada ya kupata Uhuru, Mwalimu Nyerere aliona wananchi wengi wanaishi mbalimbali (wametawanyika) kiasi cha kukosa huduma za kijamii. Hivyo alianzisha mfumo wa vijiji vya ujamaa na kukawepo na kaulimbiu: “Ujamaa ni Utu” na baadaye kukawepo Sera ya Ardhi ya Vijiji pia Sheria ya Ardhi ya Vijiji. Madhumuni hayo yote yakiwa ni kuviwezesha vijiji kujiletea maendeleo endelevu. Hivyo tukasema: “Uhuru na Maendeleo” na kwa kupitia huduma za kijamii kama elimu (kisomo cha watu wazima kikawekewa mkazo, na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima kuanzishwa). Vilevile, huduma za afya, maji, miundombinu zikawekewa mkazo ili kuharakisha maendeleo ya jamii nzima.
Baada ya kufanikiwa kuanzisha vijiji, ikafuata azima ya kuhakikisha taifa linapata chakula cha kutosha. Hivyo kilimo na ufugaji vikapewa msukumo wa kutosha na kukawepo msemo wa: “Siasa ni Kilimo” tokomeza njaa.
Taifa likajenga maghala makubwa ya kuhifadhi nafaka (Silos) na mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na Magharibi ikawa vinara kwa kuzalisha nafaka kwa wingi.
Kadhalika, hayati Mwalimu Nyerere alikazania umoja wa kitaifa na kudumisha amani nchini. Kiswahili kikapewa mkazo ili kuunganisha makabila zaidi ya 120 kuwa kitu kimoja na kwa maendeleo ya taifa.
Juhudi hazikuishia hapo, bali pia Nyerere alifuta utawala wa kijadi kupitia machifu. Vilevile alianzisha shule za sekondari za kitaifa ambazo zilichukua wanafunzi kutoka mikoa yote (mfano, Kibaha Sekondari).
Hali hiyo iliwezesha wanafunzi kutoka mikoa mbalimbali kukaa pamoja, hivyo kusababisha kujenga umoja wa kitaifa na kuishi kwa upendo bila kujali walikotoka.
Mafanikio kwa Awamu ya Kwanza, ilileta uhuru si tu kwa nchi yetu, bali kwa Bara zima la Afrika; ikatujengea umoja wa kitaifa na kuimarisha nguvu za vijiji pamoja na kufuta ujinga kupitia elimu ya watu wazima.
Vilevile viwanda vingi, kikiwemo Kiwanda cha Urafiki vilianzishwa; pia kujenga Reli ya TAZARA pamoja na bomba la mafuta kwenda Zambia (TAZAMA pipeline).
Awamu za serikali zilizofuata tangu ya pili (baada ya Mwaalimu Nyerere akung’atuka madarakani mwaka 1985) na sasa tuko Awamu ya Tano; viongozi wake kwa pamoja wamechangia sana maendeleo ya taifa letu ndani ya kipindi cha miaka 34 iliyopita.
Huduma za kijamii zimekuwa zikiimarika. Mathalani, hali ya upatikanaji wa dawa na vifaatiba imekuwa nzuri; shule nyingi zimejengwa na karibu watoto wanaostahili kwenda shule wanafanya hivyo.
Sasa watoto wanasoma katika shule za serikali bila kudaiwa karo; miundombinu imeboreshwa na inaendelea kuboreshwa zaidi, hasa wakati huu wa Serikali ya Awamu ya Tano; hali ya upatikanaji maji safi inazidi kuboreshwa na huduma za umeme sasa mpaka vijijini.
Ni mengi ambayo tumeyafanya katika kipindi cha miaka 58 ya Uhuru na sasa tutarajie makubwa zaidi kupitia Sera ya Uchumi wa Viwanda na Uwekezaji ya serikali iliyopo madarakani.
Tanzania kufikia kipato cha kati ifikapo mwaka 2025 ni jambo linalowezekana, tumwombe Mwenyezi Mungu atujalie amani na uzima tele na kupitia afya njema na nguvu kazi tuliyonayo na kila mtu akifanya kazi kwa bidii tukiongozwa na kaulimbiu: “Hapa Kazi Tu” tutaweza kufanikisha malengo yetu. Mwenyezi Mungu ibariki Tanzania na watu wake.