2 Rais Kikwete akiongea na Viongozi wa CCM Mkoa Dsm Leo jijiniNinaanza mada hii kwa kuyanukuu maneno ya Fulton J. Sheen aliyekuwa Askofu wa Kanisa Katoliki huko Marekani. Alinena; “Usiogope kukosolewa kama upo sahihi, na usikatae kukosolewa kama hupo sahihi.”
  Kwa sababu ninakwenda kuzungumzia mustakabali wa Taifa letu, inanilazimu kukosoa na kushauri, itanilazimu kusikitika na kulia pia pale itakapowezekana.
  Dhambi saba kwa mujibu wa Mahatma Gandhi, mwanamapinduzi wa India ni “Kupata utajiri bila kazi, anasa bila dhamiri, maarifa bila tabia, biashara bila maadili, sayansi bila utu, dini bila sadaka na siasa bila kanuni.”


  Nisimung’unye maneno, niseme wazi pasipo woga wa aina yoyote ile. Viongozi wa Taifa hili wanalitazama Taifa hili kwa nyuzi 90 badala ya kulitazama kwa nyuzi 360. Ninasema waziwazi viongozi wetu wamesababisha Taifa hili liendelee kuitwa maskini, tegemezi. Kwa zama hizi Mwalimu Julius Nyerere akifufuka hatatamani hata kuongea, nafikiri ataomba arudi mapema alikokuwa. Leo ni ndogo sana kuliko kesho ya Taifa hili, uamuzi wa leo unaweza kuangamiza na kuharibu maisha ya vizazi vya kesho.
  Asiyetazama hali hii ataitazama huko mbele lakini uhalisia wenyewe ni kwamba hali ya Taifa letu ni mbaya na tete. Baada ya kifo cha Mwalimu Nyerere Oktoba 14, 1999, mshairi mmoja aliandika hivi, “Lini tutamwona mwingine kama wewe?” Hata mimi leo ninajiuliza tutampata wapi mwingine kama Nyerere, mwenye kuchukia rushwa, mwajibikaji, mzalendo, muwazi, mwenye utulivu wa mawazo na uamuzi, mpenda watu na mnyenyekevu?


  Nchi sasa inayumba kwa kukosa viongozi, nchi inakufa kwa kuwa na baadhi ya viongozi bandia. Tumebaki na viongozi wenye uzoefu wa kuiba rasilimali za Taifa letu. Tumebaki na viongozi wenye uzoefu wa kughushi rasilimali za Taifa letu. Tumebaki na viongozi wenye uzoefu wa kusaini mikataba wasiyoifahamu. Tumebaki na viongozi wasiosikiliza maoni ya wananchi wao. Tumebaki na viongozi wenye kusubiri posho; ama hakika hii ni aibu na fedheha kubwa.
 Akihubiri katika mkesha wa Krismasi mwaka 2014, Askofu wa Jimbo Katoliki la Iringa, Tarcisius Ngalekumtwa, anasema “Leo tuna viongozi wanaojilimbikizia mali kuliko hata wanavyoweza kuzitumia, mtu unakuwa na mamilioni ya shilingi ambayo unaweza ukafa hata hujayatumia. Huu si uongozi, hata simba hajilikimbizii nyama ya ziada kuliko anayoihitaji.”


 Leo Taifa letu la Tanzania lina zaidi ya miaka 54 ya uhuru. Je, ni nini ambacho tunaweza kujivunia sisi kama Watanzania? Kuishi ndio kubadilika lakini sioni kama Taifa la Tanzania tumebadilika, bado tu wategemezi wa mataifa mengine, kweli hii ni aibu na fedheha kwa Taifa kama la Tanzania lenye rasilimali lukuki.
 Ndugu zetu Wafipa wana msemo unaosema, “Macho hayawezi kumponya mgonjwa.” Hatuwezi kuwa kama tunavyotamani tuwe kama hatujachukua hatua mathubuti.   Unaposhindwa kumfukuza mtu anayetakiwa aondoke, unaonesha uongozi dhaifu, ni kama unamruhusu nyoka kuishi chini ya kitanda cha mtoto wako, tafadhali usilie kama mtoto wako atang’atwa na kufa.


  Taifa hili liko hivi lilivyo kwa sababu ya viongozi walioko madarakani na chama tawala ambacho kimeshindwa kuwafukuza viongozi wabadhirifu, hizi ni dalili zinazoonesha kwamba uongozi wa chama hiki hauna uamuzi stahiki na Taifa letu na una udhaifu mkubwa.
  Nasikitika sana kwa sababu baadhi ya viongozi wanaotuongoza ni walaghai, wala rushwa, waongo, wenye maneno mengi lakini yenye utupu na wababaishaji. Aliyepata kuwa Waziri Tanzania, Arcardo Ntagazwa (1993) aliwahi kusema, “Tutakapokufa vizazi vijavyo vitafukua makaburi yetu ili vione vichwa vyetu viongozi vilikuwa na ubongo wa aina gani kwa sababu yaelekea hatufikiri sawasawa.”


  Nchi yetu Tanzania tunakupenda sana! Lakini nasikitika kwamba sipigi hatua yoyote ile kila kukicha. Tumekuwa waoga pasipostahili woga. Tumekuwa wakimya pasipostahili ukimya. Tumekuwa wanafiki pasipostahili unafiki. Tumekuwa mashabiki pasipostahili ushabiki.
  Sasa ni wakati wa kusema ukweli, sasa ni wakati wa kuushuhudia ukweli. Walio makaburini hawawezi kuhoji rasilimali za Taifa lao zinavyotumika, lakini sisi tulio hai uwezo huo tunao, sababu hizo tunazo, na muda huo tunao.
Kwa utamaduni tuliokuwa nao Watanzania, huko nyuma tulikuwa watu wa kupuuzia masuala ya msingi pengine ukimya wetu umewapa mwanya viongozi na Serikali inayotutawala kutuibia rasilimali zetu.


  Huu ni muda ambao Watanzania tunajiuliza, nani anakula dhahabu? Nani anakula tanzanite yetu? Nani anakula almasi yetu? Nani anameza gesi yetu? Nani anatorosha wanyamapori wetu? Nani anachukua mazao yetu bila kulipa?
  Denis Mpagaze, mwandishi wa kitabu cha Ethical Journalism: A Voice of the Voiceless anasema; “Hakuna habari inayozidi uhai, na mwandishi makini ni chukizo kwa watawala wenye mashaka.”
  Ninatambua kwamba kuna vita kwa wanaotenda mema, kuna vita kwa wale wanaoiongoza jamii kwenye njia ya uadilifu, lakini hapa nayanukuu maneno ya Etienne de la Boetie (1530-1563) kwamba “Amueni kutonyanyaswa na mtakuwa huru,” mwisho wa kunukuu.


  Kwa muda mrefu sasa Taifa letu viongozi wake wamekuwa wakitumia nyadhifa zao kutunyanyasa. Ni wajibu wangu kutumbua jipu ambalo linahitaji kutumbuliwa. Mchungaji Dag Heward Mills katika kitabu chake cha Viongozi na Uaminifu, anasema; “Tatizo la Afrika ni uongozi. Afrika inatatizwa na viongozi wabaya, na ubaya wao ni sawa na kumkaribisha shetani kwenye maisha yako. Nchi nyingi za Afrika zinapata viongozi ambao wanaiba rasilimali za mataifa yao. Viongozi wa nchi za Afrika wana utajiri binafsi kuliko wa nchi wanazoziongoza.”


  Ukweli ni sifa ya Mungu, maisha  tunayoishi Watanzania si saizi yetu. Hali hii inasikitisha sana na inaniuma sana na sijui itaisha lini, Watanzania tunaishi kwa mbinu ya ‘bora liende’.  Wakati wimbi kubwa la idadi ya Watanzania wakiishi maisha ya ‘bahati nasibu’ kuna wachache wanaishi maisha yasiyo na wasiwasi, wachache hawa wana uhakika kwamba wakiugua kidogo tu kuna pesa za kuwapeleka kutibiwa nje ya nchi, wana uhakika kwamba watoto wao watasoma kwenye shule za kimataifa.
  Watanzania wengi hawana uhakika na mafanikio yao walionayo na wanayotarajia kuyapata, ni ukweli usiohitaji hoja kwamba Tanzania aliyoiacha Mwalimu Nyerere siyo Tanzania ya sasa. Serikali iliyoko madarakani imejisahau kwa kiasi kikubwa. Kutokana na rasilimali zilizopo Tanzania  naamini  si  nchi  maskini. Tanzania bila umaskini inawezekana, vijana wa Kitanzania kupata ajira katika Taifa lao inawezekana,  Tanzania bila ufisadi inawezekana.


Kadiri ninavyozidi kutafakari mustakabali wa Taifa letu ndivyo machozi yanavyonitiririka kiasi cha kunifanya nisali sala fupi ili niendelee. Haya nasali; “Ee Mungu, tunakuomba utusaidie tuwakumbuke wenye njaa tunapokuwa na chakula, tuwakumbuke wagonjwa tunapokuwa na afya, tuwakumbuke wote wanaoteseka kwa sababu ya maisha kuwa magumu, tuwakumbuke wasio na nyumba za kulala, ee Mungu likumbuke na Taifa letu la Tanzania, Amina.”
  Mwaka 1995, mwasisi na mpigania uhuru wa Taifa hili, Mwalimu Nyerere, akihutubia Mkutano Mkuu wa CCM  mjini Dodoma, alisema hivi; “Watanzania wanataka mabadiliko, wasipoyaona, wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM.”


  Ni kweli Watanzania tunataka mabadiliko. Kwa kauli ya mwasisi huyu ni kwamba hata nje ya CCM kuna mabadiliko. Kwa kauli hiyo ya Mwalimu Nyerere ni kwamba hata bila CCM mabadiliko yapo. CCM ya sasa ina wanasiasa waongo, CCM ya sasa ina wala rushwa wengi, Serikali ya CCM sasa imeshindwa kuwaletea wananchi matumaini.
  Hii tena siyo ile CCM aliyoiacha Mwalimu Nyerere. Viongozi wa CCM wanajilimbikizia mali wao na familia zao. CCM sasa wanalindana, wanabebana kwa maovu. Leo hii kada wa CCM akikutwa na kashfa kubwa anaambiwa kwa upole ajiuzulu ili kukinusuru chama na siyo kulinusuru Taifa, lakini Mtanzania wa hali ya chini akikutwa na kosa dogo tu, anatozwa faini na kutumikia kifungo cha miaka kadhaa, huu ni unyanyasaji.


 Mwanafalsafa Phaedrus alipata kusema hivi; “Yeyote anayeonekana kwenye kosa la kughushi hawezi tena kuaminika hata kama anazungumza ukweli”.
  CCM wameghushi rasilimali zetu vya kutosha; now we want change in our country. Muda wa kunyanyaswa umetosha, muda wa kutishiana maisha sasa hivi haupo tena, sasa ni muda wa uwazi na uwajibikaji, muda wa kuongopewa umetosha, tumewachoka wanasiasa waongo.
  Tumechoka kuendelea na sera mbovu zisizo na dira, sasa ni muda wa mabadiliko katika kila nyanja. Tunapoelekea Uchaguzi Mkuu Watanzania tuhakikishe tunawachagua viongozi ambao wanatanguliza utaifa kwanza.
  Mwasisi wa chama cha Congress cha nchini India, Mahatma Gandh, aliwaeleza wanachama wake maneno haya; “Nipo tayari kufa lakini siko tayari kuua. Viongozi wa Congress kama hamtawatumikia raia kwa uadilifu jitayarisheni kukiua chama. Lakini msitumie vitisho au nguvu za dola au kuua vyama vinavyopinga, umma hautishwi kama tulivyokuwa hatukutishika na nguvu za wakoloni”.


 Maneno ya mwasisi huyu yametimia, mpaka tunavyozungumza sasa, Chama cha Congress hakipo madarakani.
 Rais wa Tatu wa Marekani, Thomas Jefferson, alipata kusema hivi, “The people have right to abolish a Government that does not support their interest”. Kwa tafsri isiyo rasmi anasema, “Umma (watu) una haki ya kuifutilia mbali serikali inayokwenda kinyume na matakwa yao na kujiwekea serikali mpya madarakani”.
 Na mwanamapinduzi John Locke katika maandishi yake maarufu ya Two Treatises of the Government ameandika hivi, “If the government fail to protect the right of the citizen the leaders of the government put themselves into the state of war with the people the people have right to overthrow that government and establish a better one”. Kwa tafsiri isiyo rasmi anasema, “Umma una haki ya kuiondoa serikali yoyote madarakani iliyoshindwa kulinda haki zake na kuiweka serikali iliyo bora zaidi, serikali isiyolinda haki za raia wake inatangaza vita na raia wake”.


  Hali hii sasa inaikuta Serikali ya CCM. CCM imelitawala Taifa letu  tangu tupate uhuru ikiwa ni zaidi ya miaka 50, lakini bado Tanzania ni nchi ya watu maskini wa kupindukia. Taifa lenye umri wa zaidi ya miaka 50 ni Taifa lililokwisha, linalopaswa kuwa na uchumi imara na siyo kutegemea kujiendeleza kwa misaada ambayo haiwasaidii wananchi.
  Serikali ya CCM imekosa dira, imeshindwa kuwaletea Watanzania maendeleo ya kweli na Tanzania yenye neema. Sasa Taifa letu limejitengenezea kundi jingine hatari la ‘wakoloni weusi na wenye ngozi nyeusi’ wanaotumia nyadhifa zao kuwaibia Watanzania rasilimali zao.
  Aprili 18, 1993, mwandishi Paul Johnson wa gazeti la Sunday New York Times la Marekani, aliandika hivi, “Ukoloni umerudi kwa ukaribu sana, nchi nyingine haziwezi kabisa kujiongoza zenyewe hasa nchi maskini za kusini mwa jangwa la Sahara, ambazo zitalazimika kujikabidhi kwa wakoloni walio watawala kwa kipindi cha kati ya miaka 50 hadi 100”.


  Kutokana na maoni na mtazamo wa mwandishi huyu, mambo aliyoyazungumza na kuyatabiri yameanza kutimia kwa kiasi kikubwa huku ‘wakoloni weusi’ ambao ni watawala wametoa fursa na mwanya wa kushirikiana na wakoloni wa zamani kufanikisha unyonyaji wao dhidi wananchi wao waliowaweka madarakani.
  Leo ninaikumbusha Serikali ya CCM maneno ya Jean Bodin (1530-1596) kwamba “Hakuna nguvu wala mali bila watu”. Leo ninataka kuiambia Serikali ya CCM hivi, “Historia itawahukumu na ukweli utawaweka huru.”
 Naye mwanaharakati Clarence W. Hail alipata kusema; “Unaweza kuuweka ukweli kaburini lakini ukweli hauwezi kukaa kaburini.”
 Wayahudi walipomuua Yesu Kristo walimweka kaburini wakifikiri wamemaliza kazi, lakini ni ukweli kwamba Yesu Kristo hakukaa kaburini, alifufuka, ukweli wa Yesu Kristo kufufuka ulishinda, baada ya Wayahudi kusikia kwamba Yesu Kristo amefufuka walijaribu kuwahonga walinzi pesa, eti waseme wanafunzi wake walimwiba wakati wao wakiwa wamelala.


  Uongo wao haukuwapeleka mahala popote hatimaye leo kanisa linazidi kuchanua kila iitwapo leo. Serikali  ya CCM  imefanikiwa kuwatawala Watanzania kwa muda mrefu, lakini ni ukweli kwamba Serikali hiyo haitawatawala Watanzania  miaka yote.
  Methali ya Kifaransa inasema hivi; “Watu binafsi watakufa lakini ukweli ni wa milele.”  Hulka ya Serikali ya CCM kuwanyonya Watanzania kwa kuwaibia rasilimali zao haitaisha kama Watanzania wasiponuia kuchukua uamuzi mgumu.
 Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipata kusema hivi;  “Mtu akionja nyama ya mtu, lazima ataendelea kula nyama za watu”.  CCM wameonja rushwa hawawezi kuiacha rushwa.
  Katika kitabu chake cha Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania, Mwalimu anasema; “Kwa bahati mbaya sana nchi yetu sasa rushwa imekuwa ndiyo ada. Badala ya kulaani rushwa watu wanamshangaa mtu asiyetaka rushwa na anaonekana ni mjinga asiyekwenda na wakati”.
 CCM wameonja ufisadi hawawezi kuuacha kirahisi. CCM wamelewa madaraka hawawezi kuyaachia hivi hivi.  


  Mchungaji Dag Heward Mills alipata kusema “Jihadhari na watu wasiobadilika kwenye himaya yako.” Kutokana na maneno hayo ni vigumu kuwafundisha uaminifu watu wanaoongozwa na kiongozi asiye mwaminifu.
  CCM hawabadiliki, mtoto wa nyoka ni nyoka. CCM wanatumia muda mwingi, nguvu nyingi katika kulinda na kutetea maovu. Serikali ya CCM imebaki kulazimisha uongo kuwa ukweli katika misingi inayoonekana wazi kabisa.
  Ismail Haniyeh naye katika matamshi yake alipata kusema,  “Baadhi ya watu hudhani kuwa ukweli unaweza kufichwa kwa kuuzuia kidogo au kuupamba, lakini kadiri muda unavyozidi kwenda kilicho cha kweli hudhihirishwa na uongo kutoweka”.
  CCM wameliingiza Taifa katika mikataba ya kilaghai kwa usiri mkubwa wakifikiri kwamba Watanzania hawatafahamu, na sasa mikataba hiyo iko wazi na kilichobainika ni wizi tu wa rasilimali za Watanzania. Macho ya Watanzania yako wazi yanautazama uongo wa Serikali ya CCM. Masikio ya  Watanzania yako wazi yanausikia uongo wa Serikali ya CCM.


  Mtanzania zinduka utetee rasilimali za Taifa lako, nchi imekuwa mali ya wachache, udanganyifu na wizi umeshika kasi, CCM imeshindwa kutuletea maisha bora Watanzania na ahadi zao za uongo hazipaswi kuvumilika tena.
  Yako wapi maisha bora kwa kila Mtanzania? Ziko wapi ajira milioni moja za vijana? Sasa ni uovu umetamalaki kila kona nchini. Maisha ya vijana wengi ni ya taabu na dhiki kubwa na ajira walizoambulia sasa ni kugeuzwa wendawazimu wanaookota chupa za plastiki mitaani. Aibu gani hii? Na sasa kimewadia kipindi kingine cha kupokea ahadi za uongo kutoka kwa msaka urais mwingine kutoka CCM, lakini tukiamka na kuutafuta ukweli tutashinda na zaidi ya kushinda dhidi ya udhalimu.
  Fred Mpendazoe katika kitabu chake cha Tutashinda  anaimba  ngojera hii:-


*Nionyesheni wataalamu wenye moyo wa uzalendo nami nitakuonyesha mikataba mibovu isiyo na maslahi kwa Taifa iliyotengenezwa na wataalamu wetu.
*Nionyesheni viongozi wenye uzalendo na huruma kwa raia nami, nitakuonyesha viongozi wanaopigania wawekezaji kutoka nje.
*Nionyesheni viongozi wa siasa wenye moyo  wa uzalendo nami, nitakukumbusha uuzaji wa mashirika  ya umma yaliyouzwa kwa bei ndogo na wanasiasa.
  Hakuna matumaini wala faraja ndani ya CCM. Ninachofarijika ni kwamba Watanzania hawajafunga ndoa na CCM, na wala CCM haina kibali cha kuwaongoza Watanzania miaka yote.


  Fanny Zooey alipata kuandika hivi, “Sauti ya umma ni sauti  ya ushindi, machozi ya umma ni sauti ya ushindi”. Na Wayahudi wana methali inayosema “Hakuna chozi linalodondoka bila jibu.” Uhuru wa Watanzania kwa mara ya pili uko njiani.
  Kila mtihani lazima uwe na mwalimu aliyehusika kuutunga. Madudu yanayofanywa na Serikali ya CCM yametungwa na wana-CCM wenyewe! Mwanamuziki Bob Dylan, siku moja aliulizwa swali na mtoto wake, ‘baba unapenda sana kuimba, je, siku ukilewa sifa za watu halafu ukawa unaimba vibaya utafanyaje?’ Baba yake alimjibu hivi, “Nitaacha kuimba.”     


  CCM walipoingia madarakani Watanzania walitarajia  kupata neema juu ya neema! kinyume chake wamevuna sakata la Richmond, Dowans, EPA, utoroshaji wa wanyama hai, Tegeta Escrow, uuzaji wa mashirika ya umma na uozo mwingine. Sasa CCM wamelewa madaraka, wanahujumu rasilimali za Watanzania.
  Mwanafalsafa Cicero alipata kuandika hivi, “Unapokuwa  mwongo jiandae kukosana na jamii yote.” Robert Kiyosaki katika kitabu chake cha Rich Dad, Poor Dad anasema, “Historia ni mwalimu mzuri.” Ubabe ambao Serikali ya CCM inautumia ipo siku utawagharimu.
  Watanzania tujiulize kauli kama hizi zina matumaini ama ubabe? Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, alipohoji kuhusu hali ya mustakabili wa nchi yetu aliitwa “tumbili” na makada wa CCM, hiyo ni dharau.


  Wananchi wa Kigamboni walipohoji kuhusu kupanda kwa nauli ya kivuko waliambiwa “asiyeweza kulipa nauli apige mbizi,” hiyo ni dharau na kebehi. Kitendo cha wananchi kuhoji uhalali wa kigogo kutumia ndege ya Serikali na kuambiwa mlitaka atumie punda, hii nayo ni  dharau.
  Hayo ni baadhi ya madudu yanayofanywa na viongozi wa CCM waliolewa madaraka na wasiotaka kusikia wala kugeuka. Mungu ibariki Tanzania.
 
Mwandishi wa makala hii, William Bhoke, ni mwandishi wa habari anayeishi mkoani Mara. Anapatikana kwa simu namba: 0783 994403/ 0757 852377