Na Prudence Karugendo
 
KAMULI ni kijiji kilichomo Kata ya Kibilizi, Tarafa ya Rubale,  Bukoba Vijini, mkoani Kagera. Kwenye kijiji hicho kumejitokeza hisia na imani za kishirikina ambazo zimeanza kuwafanya wananchi kukosa amani na kuanza kuishi kwa mashaka makubwa kwa kila mwanakijiji kushindwa kuelewa ataionaje kesho!
 
Mwaka 2015, bibi mmoja mwenye umri wa miaka 80, Florida Anatori, pamoja na mwanae, Deusdedit Anatori, walilazimika kuyahama makazi yao baada ya baadhi ya wanakijiji wenzao kuchoma moto nyumba yake na kukatiwa migomba yote kwa kisingizio kuwa ni mchawi.
 
Kijana wake, Deusdedit Anatori, naye amehama kwake na kulazimika kupauza kutokana na kuharibiwa shamba la  migomba kwa madai hayo.
 
Seperatus Anatori Baweza ni mtoto mwingine wa bibi huyo. Katika maelezo yake anasema mama yake hajawahi kujihusisha na masuala ya kishirikina. Kwamba ilitokea tu kijana mmoja wa kijiji hicho cha Kamuli akaugua na kupoteza maisha.
 
Baweza anasimulia kuwa baada ya kifo cha kijana huyo, anayekisiwa kuwa na umri wa miaka 25, wanakijiji hawakutaka kujua chanzo kingine cha kifo hicho isipokuwa kumhisi bibi Anatoria kuwa ndiye mhusika mkuu wa kifo hicho. Kwamba ndiye aliyemroga kijana huyo na kumsababishia mauti!
 
Anasema kwamba tangu wahamie kwenye kijiji hicho miaka 43 iliyopita hazijawahi kujitokeza hisia za kwamba mama yao ni mchawi, muda wote wameishi kwa usalama na upendo na wana kijiji wenzao. Anashangaa na kujiuliza ni kwa nini jambo hilo litokee kwa mara ya kwanza wakati huu?
 
Baweza akaongeza kwamba ndipo baadhi ya wana kijiji wakajikusanya usiku na kwenda kwa mama yake kufanya ukatili wa kufyeka migomba yote shambani kwake. Watu hao walipoona bibi huyo hakuhamishwa na kitendo hicho cha kumkatia migomba yake, siku nyingine wakapanga tukio lingine usiku la kuchoma nyumba ya bibi huyo kwa lengo la kumuangamiza ndani ya nyumba.
 
Anasema bahati nzuri mama yake alinusurika kwa kukimbilia kwa majirani, wakati wahalifu hao wakiwa wameondoka kwa imani kwamba wamemmaliza bibi huyo.
 
Baada ya tukio hilo watoto na jamaa wa bibi huyo waliamua kulifikisha tukio la kinyama kwenye vyombo vya usalama, wakaliripoti kituo cha polisi.
 
Lakini  anasema jambo la kusikitisha polisi walipofika eneo la tukio hawakuchukua hatua yoyote pamoja na kwamba wapo watu waliokuwa wanatajwa wakihusishwa na tukio hilo la kinyama. Kwamba polisi hawakutaka kuwakamata wahusika katika jitihada za kupata ukweli wa ni kinanani walihusika.
 
Kiongozi pekee aliyefika kwenye tukio na kufanya juhudi za kumnusuru bibi ni Diwani wa Kata ya Kibilizi ambaye alimkimbiza kutoka sehemu hiyo na baadaye watoto wa bibi waliamua kumhamishia Dar es Salaam ambako ndiko anakoishi mpaka sasa.
 
Kuhusu hatua za kisheria Baweza anasema linakuwa gumu kwa sababu polisi mpaka sasa wanapiga danadana kwa kukataa kuwakamata washukiwa, na kwa vile lile ni kosa la jinai, wao kama familia wanajikuta hawana uwezo wa kulipeleka mahakamani.
 
Kwa upande mwingine, Leons Joseph, ambaye ni diwani wa kata ya Kibilizi anasema alipopata taarifa za Florida Anatori kufanyiwa kitendo cha kinyama alijitoa mhanga kwenda kunusuru maisha yake kwanza.
 
Diwani anasema kwamba alipofika kwenye eneo la tukio alikuta watu wamekasirika wakitaka kumdhuru bibi Florida, lakini kwa kutumia mamlaka aliyonayo ya udiwani alimbeba kwenye pikipiki na kumkimbiza mbali nje kabisa ya kikiji chake ambako palikuwa salama kwa watoto wa bibi huyo kumfanyia mipango ya kumhamishia jijini Dar es salaam.
 
Wananchi wa kijiji jirani na Kamuli, wanasema wakazi wa Kamuli ni watu washari wanaoishi kikatili wakisukumwa zaidi na imani za kishirikina kujichukulia sheria mikononi mwao. Kwamba ni watu wanaoonekana kutoogopa wala kufuata sheria za nchi kana kwamba wao wanalo taifa lao linalojitegemea!
 
Mbaya zaidi ni jinsi vyombo vya dola vinavyoichukulia hali hiyo, kutowakemea wananchi hao huku vikiwaacha wafanyie watakavyo kitu kinachochukuliwa kama kuwadekeza. Hali hiyo inatishia usalama wa eneo husika pale baadhi ya wananchi watakapoichoka na kuamua kujichukulia sheria mikononi katika kulipiza kisasi.
 
Mama na watoto wa bibi huyo, ambaye ni mjane kwa vile mume wake alishakufa muda mrefu uliopita, wanashangaa mama yao kuishi uhamishoni kana kwamba nyumbani kwake kuna vita ilhali nyumbani kwake ni kwenye nchi hii hii moja yenye amani na utulivu. Swali wanalojiuliza ni moja, kwa nini serikali ikubali bibi kama huyo apate manyanyaso na mahangaiko kama vile anatoka kwenye nchi yenye vita?
 
Jambo lingine ni kwamba kwa nini serikali iziachie hisia ovu za kishirikina zitawale kiasi cha kuwakosesha wananchi amani ya kuishi kwa usalama ndani ya nchi yao?
 
Baadhi ya watu wanasema kwamba jitihada zote zinazofanywa na serikali hii ya awamu ya tano ni za kuwafanya wananchi wajisikie wako salama na huru chini ya serikali yao, sasa inapowalazimu baadhi ya wananchi kuyakimbia makazi yao jitihada hizo chini ya Rais John Magufuli zinakuwa na thamani gani?
 
Kwahiyo wanachokiomba watoto, ndugu na jamaa wa bibi huyo ni serikali kuingilia kati suala la bibi huyo kunyanyaswa na watu wenye hisia ovu za kishirikina ili aweze kurudi nyumbani kwake na kumalizia muda wa maisha yake kwa amani na utulivu.