Kwa muda sasa mijadala ya siasa nchini imetawaliwa na suala la ukomo wa mihula ya urais. Katiba inatamka wazi kuwa mtu atashika urais kwa kipindi cha muhula wa miaka mitano na anaweza kuchaguliwa tena kwa kipindi cha pili cha miaka mitano. Baada ya hapo, mtu huyo anapaswa kutoendelea kushikilia wadhifa huo kwa mujibu wa Katiba yetu.
Wiki iliyopita katika matukio mawili tofauti, Rais John Magufuli amelazimika kutamka hadharani kuwa hana mpango wa kubadili Katiba ili apate fursa ya kuwania nafasi hiyo kwa kipindi cha tatu. Tunaamini kauli yake hiyo ilitokana na baadhi ya watu ambao wanapendekeza Rais Magufuli angeongezewa kipindi kingine kuwapo madarakani kutokana na utendaji wake katika kuongoza nchi.
Ni vema rais ametoa kauli hii hivi sasa kwa sababu wakati fulani kauli yake yeye mwenyewe ilianza kuonyesha kana kwamba angependa kuendelea kuishikilia nafasi hiyo hata pale kipindi chache cha uongozi kitakapomalizika.
Rais Magufuli aliwahi kunukuliwa akijiuliza kwa sauti kwamba haoni kama kuna mtu ambaye ana uwezo wa kuyaendeleza mambo makubwa ambayo yeye ameyaanzisha.
Kuna baadhi ya watu wakaanza kuitafsiri kauli hiyo kama Rais Magufuli anaanza kujipigia debe ili aongezewe muhula mwingine ili kukamilisha mambo makubwa ambayo ameanza kuyatekeleza.
Aidha, huko nyuma zimekuwepo juhudi za kutaka kuwasilisha bungeni mapendekezo ya mabadiliko ya sheria mama ili kurefusha kipindi cha urais kiwe cha miaka saba badala ya mitano. Pia kumekuwa na juhudi za kutaka kuondolewa kwa ukomo wa rais kuwa madarakani.
Vilevile ipo kesi Mahakama Kuu ambapo mkulima mmoja ameiomba serikali kutoa tafsiri ya kifungu cha Katiba kinachoweka mihula ya urais. Taasisi kadhaa na watu binafsi wameomba kuunganishwa katika kesi hiyo.
Haya yote yalianza kujenga picha kuwa kuna harakati za kutaka kubadilisha vipengele vya Katiba kwa lengo la kuondoa ukomo wa rais kuwa madarakani.
Ni vema kuwa Rais Magufuli mwenyewe ameibuka hadharani na kutangaza kuwa hana mpango wa kubakia madarakani hata kwa dakika moja pale muda wake utakapokamilika.
Kwa kuwa mtu ambaye watu walipatwa wasiwasi kuwa ndiye anayelengwa katika harakati hizo za kutaka kubadilisha Katiba ameshatoa kauli ya kutotaka kuendelea kuwepo madarakani, hata Katiba ikibadilishwa hana mpango huo, ni vema sasa suala hili likafungwa ili tujikite katika masuala mengine muhimu kwa ujenzi wa nchi.
Mwisho