Waziri mkuu wa zamani wa Tanzania, Cleopa David Msuya, anaamini kwamba Uchaguzi Mkuu wa tano baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini, utafanyika Oktoba kama ulivyopangwa.
Bosi huyo wa nchi aliyeshika wadhifa huo uliokwenda sambamba na umakamu wa rais kwa vipindi tofauti vya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, na Ali Hassan Mwinyi, anasema: “Rais Jakaya Kikwete ataondoka Oktoba,” tofauti na watu wanavyomfikiria.
Msuya ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 82, alizungumzia hilo baada ya kuombwa kutoa maoni yake juu ya wasiwasi uliotanda kwa Watanzania na kubebwa na viongozi mbalimbali wa vyama vya upinzani waliotoa angalizo juu ya kufanyika kwa uchaguzi huo.
Katika mahojiano hayo yaliyochukua takribani saa tatu, Msuya alitulia, akatafakari akasema: “Kijana… (akiwa na maana mwandishi aliyemtaka atoe maoni yake) …tuachie vyombo vifanye kazi yake.”
Wasiwasi wa vyama vya siasa na baadhi ya makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni kasi ya uandikishaji au usajili wa wapigakura katika uchaguzi wa mwaka huu unaofanywa na Tume ya Uchaguzi (NEC).
“Muda uliobaki (NEC) wanaweza. Hii ni kwa sababu lengo ni kuandikisha watu na kama wanavyosema sasa kwamba mashine kama 8,000 ziko nchini. Ni suala la kusambaza na kuandikisha watu, nafiri uchaguzi utafanyika mwaka huu,” anasema Msuya.
Anasema kwamba pamoja na kuwa na imani hiyo, bado wadau hawawezi kuondolewa kwenye jukumu la kuuliza kama inawezekana. Tume au Serikali ijieleze kikwelikweli uwezo wake kama inaweza au haiwezi.
Katika hilo ndipo kwa mara nyingine Msuya anakumbuka kauli yake juu ya kuwaambia wananchi kuwa kila mmoja atabeba msalaba wake mwenyewe.
Anasema kwamba wakati huo akiwa Waziri wa Fedha katikati ya miaka ile ya 1980 wakati Mwalimu Julius Nyerere anaondoka madarakani na kuingia Ali Hassan Mwinyi, kulikuwa na hali mbaya ya kiuchumi na alichofanya ni kuwaambia wananchi ukweli kwamba “jamani tuna shida.”
“Lakini shida ya sasa watu hawaelezwi ukweli kama fedha ziko au haziko. Kama ziko mbona vifaa havitawanywi, inaelekea kuna kitu hapa ambacho hakielezwi vizuri,” anasema.
Anasema kwamba ni wakati mzuri kwa nchi wafadhili kuwabana kama watakuwa wazito kusema ukweli juu ya hali halisi kama uchaguzi upo au haupo.
“Uwezo wa kutubana wanao, maana wanajua zaidi wale kwa sababu sehemu ya akiba yetu mmeweka huko. Kama mna madeni kama yale ya makandarasi wakubwa wanaodai mapesa anajua kwa sababu kampuni nyingi ni za kwao na wana mabalozi wao hapa,” anasema.
Anasema, “Kama taasisi zetu za hospitali nguvu ya Serikali ni jinsi inavyobeba jamii na wewe kwa kueleza ukweli ili muende pamoja na wajue mnachukua hatua gani. Hii inawezekana, inawezekana kabisa. Sasa usambazwaji wa vitu hivi kuna kigugumizi cha NEC.”
Kwa Msuya, anasema kwamba hata mpango wa kuunganisha kupiga kura ya maoni kwake yeye haoni tatizo. “Uzuri ni kwamba inapunguza gharama kwa kufanya pamoja.”
Kuhusu kujitokeza idadi kubwa ya makada wa CCM kuwania nafasi ya urais, Msuya, ni kama alibashiri juu ya hilo akisema, “Suala la mgombea ni suala la chama, lakini nikiri ndani ya CCM tumechanganyikiwa kidogo. Si kama zamani. Vurumai.”
Anasema kwamba katika mapinduzi yanayotakiwa yafanyike ndani ya CCM na mwenyekiti mpya anayekuja itakuwa kazi yake ni kupangua msingi ‘ahilaikia’.
“Kwa mfano’ Labor Party (Chama cha Leba) ya Uingereza wanajua kwamba akitoka huyo anaingia huyo, na kadhalika. Hii pia ipo hata kwa Wamarekani katika vyama vya Republican na Democratic.
“Lakini kwa vyama vyetu hivi vinahitaji kuiga utaratibu wa Frelimo kwa sababu unajenga uongozi, unaunganisha uongozi na kulea viongozi. Inabidi kuanza upya maana hii system (mfumo) imeparaganyika. Ipo kazi ya kufanya,” anasema.
Anasema kwamba kazi ya uongozi ni kufanya uamuzi mgumu na kwa upande wake anaamini kwamba atapatikana kiongozi mzuri, kwani inategemea uthabiti wa uongozi wa chama.
Anasema kwamba kiongozi wa kugawa fedha kwa sasa hatakuwa na nafasi kwa sababu watu kwa sasa wamefundishwa kuchukua fedha na hawatakuja kujali.
“Watu wataunga mkono mgombea wa chama ambaye anakubalika ndani na nje ya chama. La maana zaidi CCM, tuwaombee watutafutie viongozi wenye sifa nzuri,” anasisitiza.
Anasema kwamba nchi kwa sasa inachukia mtu anayehusishwa na rushwa, kula fedha za umma – ufisadi.
“Hii chuki cuts right across (inagusa moja kwa moja) jamii yote. Vyama vyote. Jamii wakiona unatembelea gari zuri unaona wazi sura za watu zinasema, zinaonesha chuki ya kutumia usafiri huo,” anasema.
Anasema, kwa mfano, kwa sasa mtu akiingia mjini hata akiwa na gari ambayo mtu kama yeye (waziri mkuu mstaafu) amepewa na Serikali, unakuta watu wanavyokuangalia vibaya.
“Iko chuki, wanakuona wewe kama ni miongoni mwa watu unayekula fedha za umma. Iko chuki. Kuna chuki, watu wanaona wazi kuna watu wanakula na kuna ufisadi,” anasema.
Anasema kwamba jukumu la Rais Jakaya Kikwete kwa sasa na timu yake ndani ya CCM ni kutafuta mtu ambaye anaonekana kwamba mlengo wake ni kutoa utumishi siyo kula.
“Siyo kupata cheo kwenda Ikulu, maana kuna watu wanataka kwenda Ikulu ili waite marafiki zao ili wagawane mali. Lakini kusema kwamba mimi nakwenda pale nikahudumie Watanzania wana shida zao. Watu wanatafuta mtu aina ya akina Nyerere hivi. Ni mtu gani atayejitolea? Ahangaike, atuhudumie sisi tundokane na shida zetu na matatizo yetu.
Anasema kiongozi huyo ni mtu ambaye anaelewa uchumi. Asaidie kwenda mahali rasilimali watu zikatumika hasa baada ya kupatikana wasomi hawa kutoka shule na vyuo vingi vilivyofunguliwa.
Anasema kwamba kazi ya kukuza uchumi ni muhimu na kama nchi ikikosa mtu itaingia kwenye matatizo makubwa hasa ikizingatiwa kuwa anatakiwa kuwa mtu wa masuala ya uhusiano wa kimataifa.
Anasema kwamba tathmini yake katika uchaguzi unaokuja wa 2015, CCM itashinda ingawa kwa sasa ni vigumu kwake kubashiri kiwango cha asilimia, ila itavuka asilimia 50.
“Hii ni kwa sababu mpaka sasa pamoja na kelele zote zinazopigwa, sijaona chama chochote cha upinzani, hivi vilivyosajiliwa, vyenye kutukuka hapa kama Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi ambavyo ni vikubwa, sijaona ambacho kina sera za kuizidi CCM,” anasisitiza.
Anasema; “Lazima nikiri CUF upande wa Zanzibar pale wamejenga ngome fulani, lakini Chadema sehemu za mijini huko Bara wamefanya hivyo, kama Iringa, Musoma, Moshi, Mbeya, Mwanza, Arusha. Wako kwenye urban areas (maeneo ya mijini) tu, lakini vijiji na wilayani hawako.”
Anasema kwamba CCM kuna tatizo kwa baadhi ya viongozi watendaji ndani ya Serikali na ndani ya chama wanaofanya watu wachukie. Ukiacha hizi sura mbovu za watendaji, CCM bado inakubalika sana kwa watu wengi. Bado wanapenda CCM.
“Mimi mtazamo wangu nafikiri, Katibu Mkuu wa chama, Abdulrahman Kinana, amefanya kazi kutembea na kujikosoa, hali ambayo imesaidia sana watu kuwa na imani na chama. Watu wanakubali hata ndani ya chama na Serikali wanaona kazi yake. Wanaikubali.
“Amekuwa mkali kwa watendaji wabovu hata kwa mawaziri wazito ambao hawashughulikii matatizo ya mahindi, sukari na mambo mengine yanayofanya Serikali ikasemwa vibaya,” anasema.
“Wakitupatia mtu tofauti, kwa hizi hisia zinazojengeka vichwani mwa watu na makundi mbalimbali, itakuwa taabu kwelikweli,” aliendelea kuonya Msuya.