Kila ifikapo Februari 14 watu wengi huadhimisha sikukuu ya wapendanao ulimwenguni, na utaratibu huu umedumu kwa karne nyingi ukihusishwa na utamaduni wa magharibi.
Watu huadhimisha siku hii kwa namna tofautitofauti ikiwa ni pamoja na kupeana zawadi kama vile maua mekundu,chokoleti pia kutoka na hata kwenda kupata chakula cha pamoja katika maeneo ya kustarehe kama vile hotelini au hata katika mgahawa.
Utamaduni huu wa kimagharibi umekuwepo tangu mwanzoni mwa karne ya tatu huko Ulaya na baadaye kusambaa ulimwenguni kote.
Hii leo ukiwauliza baadhi ya watu hususani vijana ni kwa nini huadhimisha siku hii kila ifikapo Februari 14 kila mtu atakwambia sababu zake na wengine huitafsiri siku hii kama siku ya kuwakumbuka watu wanaowapenda zaidi, lakini je umewahi kujiuliza siri iliyoko nyuma ya siku kuu ya Wapendanao?
Siku ya wapendanao kwa kimombo hufahamika kwa jina la Valentine Day historia yake imeanzia karne ya tatu huko Roma ikiwa ni heshima ya kumuenzi Kasisi wa Kanisa Katoliki aliyejulikana kwa jina la Valentine.
Inasemekana wakati huo kiongozi wa miliki ya Roma Kaisari aliyejulikana kwa jina la Cloudius II aliwapima askari wake kuwa wakakamavu na bora kwa kigezo cha ukapera yaani kutokuoa wala kuwa na familia na hivyo kuweka zuio la ndoa kwa askari hao.
Valentine ambaye alikuwa ni padri wa kanisa Katholiki na muumini wa jamii yenye kuwa na familia hakukubaliana na uamuzi wa Kaisari na hivyo kuendelea kuhamisha vijana kuwa na familia huku akiwafungisha ndoa kwa siri katika sehemu ya uficho chini ya kanisa.
Kaisari alikasirika sana mara baada ya kupata taarifa za askofu huyo kuendelea kuwafungisha ndoa vijana kwa siri na hivo kumtia hatiani kwa kukiuka maagizo na sheria na kuamuru Valentine akamatwe na auawe mara moja.
Akiwa gerezani Valentine alitokea kumpenda binti mmoja aliyekuwa akimtembelea gerezani hapo na hata kabla ya kuuawa Valentine aliandika na kumtumia binti huyo barua iliyokuwa na ujumbe uliosomeka kutoka kwa Valentine wako. Valentine aliuawa kwa kukatwa kichwa ikiwa ni amri ya Mfalme Claudius ll mnamo Februari 14, 270 Baada ya Kristo.
Mfalme Claudius ll aliamini kwamba kama askari wakibaki makapera bila kuoa basi angekuwa na jeshi imara sana kwa ajili ya kuendelea kutawala na kupanua miliki ya Roma, hivyo walishauriwa kutafuta wanawake kwa ajili ya kujiburudisha tu na si kuoana jambo ambalo halikumfurahisha Valentine kwa kuwa ilikuwa dhambi na kinyume cha maadili ya ukristo na hivyo kuendelea kufungisha ndoa kwa siri.
Inasemekana kuwa Askofu Valentine alisalia kwenye mioyo wa watu na miaka 200 baadaye kiongozi wa kanisa la Katoliki wa miaka hiyo Papa Gelsius alitangaza rasmi siku ya Februari 14 kama siku kuu ya kumkumbuka na kumenzi Askofu Valentine kama mtetezi na mpigania ndoa kwa wachumba wa kikristo.
Kumekuwa na mitazamo tofauti tofauti kuhusu namna ya kuadhimisha siku hii ya Valentine, baadhi wakidai kuwa siku hii ni kwa ajili ya wale walioko kwenye ndoa tu na wengine hudai kuwa ni kwa ajili ya watu wote hata ambao wako kwenye uchumba na hawajafunga ndoa ilimradi wanapendana hata hivyo hakuna utaratibu maalumu mpaka sasa unaoonesha ni wapi wanapaswa kusherehekea sikukuu hii kwani hii leo hata watoto husherehekea.
Ingawa Askofu Valentine alipinga ukapera na vijana kufanya ngono kiholela akiamini kuwa ni kinyume na maadili ya ukristo ndiyo maana akaamua kuhamasisha vijana kufunga ndoa ili kuepukana na uasherati pamoja na uzinzi.