Katika miaka ya 1980, bendi moja ya muziki wa dansi hapa nchini ilitunga wimbo uliokuwa na kibwagizo cha “bomoa ee, bomoa ee, tutajenga kesho!”

Wimbo huo haukudumu si kwa kuwa uliachwa kuchezwa kwenye redio ya Taifa enzi hizo – RTD leo TBC, ila Serikali iliupiga marufuku kwa sababu haukuwa na maudhui yenye mwelekeo wa kuelimisha jamii.

 

Siku hizi hakuna wimbo unaopigwa marufuku. Nenda studio karekodi chochote utauza. “Nataka kulewa…” “Nani kamwaga pombe yangu… nauliza!” Jamii inajifunza nini kupitia nyimbo hizo? Kuna vijana fulani wa Kingoni walipata kuimba wimbo “Wanawake wazuri, wazuri wameolewa, wamebakia manungayembe” Weee! Walijuta nani aliyewatuma kutoka na singo hiyo!

 

Hizo zilikuwa enzi za maadili mema ya Kitanzania. Leo hii nani anashughulikia jambo lisilo na maslahi kwake? Sitaki kuzungumzia hili leo, kwa kupitia wimbo wa ‘Bomoabomoa tutajenga kesho’. Naanza makala haya kwa kuwakumbusha wasomaji wanaokumbuka wimbo huo na wale ambao hawakupata kuusikia, lengo ni kutaka kuufikisha ujumbe kwa Serikali yangu sikivu.

 

Japokuwa wimbo ule haukuwa unamaanisha ubomoaji ninaotaka kuuzungumzia, lakini athari za kibwagizo hicho kimenifanya niukumbuke na kupata jibu kuwa Serikali inajua fika kuwa ukibomoa leo, kujenga kesho itakuwa ni kazi ngumu.

 

Kazi ngumu kwa kabwela ambaye ametumia muda mwingi kuvuja jasho jingi hadi kufanikisha kujenga nyumba yake. Kuna aliyejenga baada ya kustaafu kazi, mwingine baada ya kuuza njugu, mwingine  baada ya kuuza dagaa bichi mitaani, mwingine baada ya kukopa.

 

Wapo waliorithi nyumba hizo kutoka kwa wazazi wao. Wapo waliouza mifugo na mashamba yao ili wapate sehemu ya kujistiri na familia zao.

 

Leo Serikali inampa fidia na kumwambia ama kajenge pale, au utajua utaenda kuishi wapi. Hapo anapofukuzwa kunatazamiwa kuiingizia Serikali mamilioni ya shilingi kwa miaka mingi na hivyo, kuongeza pato la Taifa na kuendelea kuwanufaisha wachache.

 

Sehemu hiyo inageuka lulu kwa wawekezaji na shubiri kwa mmiliki halali. Natambua kuwa ardhi ni mali ya Serikali, hivyo, Serikali inapohitaji ardhi hiyo kwa manufaa ya umma lazima waliopanga kwenye ardhi hiyo wataondolewa kwa namna yoyote ile.

 

Swali langu: Je, kuwaondoa watu kwa mabavu na kuwabomolea nyumba zao kwa kisingizio kuwa walishalipwa fidia, kuna manufaa gani kwa wahanga hao kama si kuwaletea usumbufu, kero, kuwaharibia mali zao na kuwaongezea umaskini wa kutisha? Je, Serikali inapata faida gani kuona watu wanafunga barabara na kubeba mabango ya kuilaani kuwa haiwatendei haki?

 

Ninatambua uwepo wa mabadiliko katika miundombinu pale Serikali na raia wake wanapopiga hatua za maendeleo kiuchumi na kijamii.

Maendeleo ya miji mingi, hususan iliyopo nchi za Dunia ya Tatu (Third World countries) huambatana na masuala mbalimbali yakiwamo; ujenzi wa miundombinu kama vile barabara, majengo, viwanda na masoko. Aidha, ujenzi wa viwanja vya ndege na vya michezo, uchimba wa madini, ujenzi wa mabomba ya maji, mafuta na hata gesi. Sasa hivi kumejitokeza mahitaji ya ardhi ya ujenzi wa bandari kavu.

 

Katika kutekeleza hayo, athari kubwa inayojitokeza ni kubomolewa kwa nyumba na kupokonywa mashamba kwa watu wa eneo husika ili kupisha ama uwekezaji, ujenzi wa barabara, viwanja vya ndege, upitishaji wa mabomba chini ya ardhi, au uchimbaji wa madini.

 

Linapotekelezwa mojawapo ya hayo, wahanga siku zote ni makabwela. Sijui itakuwaje siku ikigundulika gesi na mafuta chini ya jengo la Ikulu pale Magogoni?

Tanzania ni mojawapo ya nchi ambazo miji yake mikubwa na midogo bado haina mpangilio wa kudumu.

 

Ujenzi wa miji yetu bado ni holela. Hakuna mpangilio hata kidogo na hakuna ramani zinazoweka wazi miji, mathalani itakuwaje baada ya miaka kumi ijayo achilia mbali miaka hamsini ijayo. Ramani kama zipo basi zimefungiwa kwenye ofisi za watendaji Wizara ya Ardhi.

 

Kama rasimu inatembezwa kwa kila raia, kwanini ramani za miji yetu zikionesha mabadiliko ya siku za usoni zisichapwe na kusambazwa wananchi wajue?

 

Nikipata ramani inayonieleza kuwa mathalani baada ya miaka mitano au kumi ijayo Manzese Dar es Salaam, itakuwa ni eneo la viwanda, sitakuwa na sababu ya kwenda kununua nyumba au kiwanja na kujenga Manzese. Na haitakuwa rahisi kudanganywa na madalali. Ramani ya mipango miji ndiyo itakayokuwa dira yangu.

 

Serikali inapotaka kuwekeza mahali fulani, inachokifanya ni kukimbilia kuweka alama ya “X” kwenye nyumba na kufanya tathmini ya nyumba zilizomo kwenye eneo husika na kuwapa muda mfupi wananchi wa eneo hilo kujiandaa kuondoka.

 

Mara nyingi tumekuwa tukisikia malalamiko kuwa fedha inayotolewa ni ndogo, haikidhi gharama za mahitaji ya wakati huo. Vilio vya wengi ni kupewa fidia ambayo haitoshelezi gharama za ujenzi kwa sasa kutokana na thamani ya shilingi kushuka.

 

Leo hii wananchi wa mijini na mashambani wanalia kutokana na kuondolewa kutoka maeneo yao na kushindwa kujua hatima ya maisha yao itakuwaje baada ya kulipwa fidia isiyokidhi mahitaji, pia kuharibiwa mali zao. Tumesikia vilio vya baadhi ya wananchi baada ya kuvunjiwa nyumba zao ili kupisha uwekezaji.

 

Leo hii limejitokeza suala la bandari kavu na bomba la gesi. Bomoabomoa inaendelea na vilio vinaanza kusikika katika Jiji la Dar es Salaam. Achilia mbali suala la gesi na mafuta.

Je, Serikali haikuwahi kuwa na ndoto kuwa siku moja Bandari ya Dar es Salaam itahitaji kuwa na bandari kavu za kutosha ili kuhimili ushindani wa kibiashara uliopo kati ya Tanzania, Kenya na Msumbiji katika usafirishaji wa bidhaa zinazokwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Rwanda, Burundi, Malawi na Zambia?

 

Natambua wakati mwingine mabadiliko huendana na mahitaji ya wakati huo lakini kwa nini hakuna mipango ya siku za usoni? Ni maeneo mangapi yaliyokuwa na mapori na vichaka vya majambazi na vibaka ambayo leo hii yamejaa nyumba za kuishi watu?

 

Miaka 15 iliyopita kuna maeneo mathalani katika jiji la Dar es Salaam yalikuwa yanatosha kabisa kutengwa kwa ajili ya bandari na hata kujenga kiwanja cha ndege kidogo kwa ajili ya ndege za ndani na za nchi jirani na kilichopo kikabaki kwa ajili ya ndege kutoka nje ya Afrika badala ya kubomoa nyumba za Kurasini na za Kipawa.

 

Sasa Serikali itaendelea na kazi ya bomoabomoa na kulipa fidia na kupelekwa mahakamani mpaka lini?

 

Leo hii Kigamboni ni lulu. Hakuwafai tena wananchi waliopelekwa kuanzisha vijiji vya Ujamaa enzi ya Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius Nyerere. Sera ya uwekezaji ndiyo wimbo wetu mpya, wanaofaidika na sera hiyo ni mafisadi wachache.

 

Sasa Serikali inapaswa kufanya nini ili kuepukana na migogoro na malalamiko kutoka kwa wapigakura walioichagua na kuwa na imani nayo? Sitaki kubeza harakati zinazofanywa na Serikali katika kuleta maendeleo, ila nataka nitoe changamoto hizi ili Serikali iepukane na kadhia inayotokana na bomoabomoa.

 

Serikali inapotaka kuwaondoa wananchi wa eneo fulani, basi jukumu la kwanza ni kutafuta eneo na kampuni zitakazoweza kujenga nyumba za gharama nafuu kwa muda mfupi ili wahanga wahamishiwe kwenye nyumba hizo, si viwanja vitupu. Hii itapunguza hasira za wahanga, na kesi zitapungua mahakamani.

 

Mtu anaweza kuwa ana nyumba yenye thamani kubwa lakini ukimwandalia nyumba ya kufikia halafu akabakiwa na eneo la kujenga nyumba nyingine, kumlipa ziada kama fidia itakayolingana na thamani ya nyumba ya awali, hataamua kupanga mawe barabarani na kwenda mahakamani.

 

Serikali iweke wazi malengo yake ya baadaye katika maeneo yote nchini ambayo yamo kwenye mipango ya uwekezaji na ujenzi wa miundombinu. Ramani zitolewe kwa wananchi zenye kuonesha maeneo ya makazi, mashamba, viwanda, viwanja na hifadhi za Serikali.

 

Serikali iepuke utaratibu wa kulipa watu fidia na kuwaacha kuendelea kuishi katika maeneo hayo. Tumesikia watu wa Kurasini wakilalamika kuwa fedha wamezitumia katika kulipia watoto ada na matumizi mengine, hivyo hawana fedha na hawako tayari kuhama. Hili ni tatizo linalosababishwa na mamlaka husika chini ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

 

Aidha, Serikali ijaribu kuwa karibu na wananchi husika kuanzia hatua za awali za mpango wowote kwa kuwaelimisha, kisha kujiridhisha kuwa wananchi wameelewa malengo ya Serikali na kuondoka kwao hakutakuwa kwa kunung’unika.

 

Mbona maeneo ya vikosi vya majeshi yetu ya ulinzi na usalama yalitengwa kwa ukubwa unaokidhi mahitaji hata katika wakati huu tulionao? Eneo la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni moja ya mifano mizuri ya maeneo makubwa kwa matumizi ya wakati huo na baadaye.

 

Wamisionari wa Kikatoliki walielewa thamani ya ardhi na hivyo waliweza kuhodhi maeneo makubwa na walihakikisha na wanaendelea kuhakikisha kuwa maeneo yao hayavamiwi. Sasa kwa nini Serikali inashindwa kufanya yale yaliyowezekana wakati wa miaka ya 1960 na 1970?

 

Kama Serikali ya zama hizo iliweza kutabiri ongezeko la watu na kuweka miundombinu vizuri, leo hii mtazamo huu umezimwa na nini? Hivyo, yanayojitokeza katika miji ambayo haikupangwa vizuri, yasijirudie katika miji na maeneo ambayo yanaendelea kukua kutokana na ongezeko la watu na maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Haya yanawezekana.

 

Eric Z. Manzi

0763-400283

E-mail:[email protected]