Mpita Njia (MN) anawapongeza viongozi wote walioandaa Mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Mkutano huo umeshuhudia Rais John Magufuli akikabidhiwa kijiti cha kuwa mwenyekiti wa jumuiya hiyo muhimu sana kwa nchi za kusini mwa Afrika.

MN ameshuhudia kujipanga na kuendesha shughuli ya kuwapokea marais zaidi ya 10 kwa mpigo kwa ajili ya shughuli hiyo. Pamoja na pongezi hizo, MN ameona kasoro moja kubwa ambayo inahitaji kurekebishwa!

Kasoro hiyo ni ile anuani ya kitalu namba moja cha nchi inayoitwa Tanzania kubeba jina la Rais Barack Obama. Hakika inatia ukakasi kuona hata anuani ya Ofisi ya Rais inabeba jina la kiongozi huyo mstaafu wa Marekani.

MN anashauri mamlaka zifikirie namna ya kuondokana na jina hilo kwenye Ikulu yetu tukufu. Kuna wakati MN anawaza, ina maana walikosekana watu wa maana katika nchi yetu na hata nchi nyingine barani Afrika hadi ‘mamlaka’ ziamue kumtunuku Barack Obama sehemu nyeti ya nchi yetu?

Moja kati ya mambo yaliyomkera zaidi MN wakati wa shughuli za mapokezi na hata dhifa za Ikulu, ni pale ambapo kuna picha zilipigwa zikimuonyesha Rais John Magufuli akiwa na mgeni wake Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, huku nyuma yao kukiwa na kibao – Barack Obama Drive.

MN anafikiri kwa mtu ambaye hakuwa anafuatilia masuala yaliyokuwa yanaendelea hapa nchini anaweza kudhani Rais Magufuli alikutana na Rais Ramaphosa jijini New York ama Washington DC wakati uhalisia ni kwamba walikuwa Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam.

MN anaamini tunao mashujaa wengi ambao wanastahili kupewa heshima hiyo, ni wakati muafaka sasa kubadili na kurejesha heshima yetu. MN haamini kama viongozi wetu wanaweza kupewa heshima hiyo kwenye Ikulu ya Marekani ‘White House’.

Mpita Njia anapendekeza huyo Barack Obama atafutiwe barabara sehemu nyingine kuliko hiyo ya jirani na jumba takatifu. Nia ya waliompatia ‘heshima’ hiyo ili jina lake litumike inawezekana ilikuwa njema kabisa, ila maeneo hayakuwa sahihi, hivyo mamlaka husika sasa zianzishe mchakato wa kuondoa bughudha hiyo.