Vyama vya msingi vya ushirika mkoani Kilimanjaro vinavyotumia kiwanda cha kukoboa kahawa cha Tanganyika (TCCCo), vipo katika wakati mgumu baada ya kahawa yao kutonunuliwa kwenye mnada unaoendeshwa na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB).

Kususiwa kwa kahawa hiyo, kunaweza kusababisha vyama hivyo kukabiliana na changamoto kadhaa ikiwamo kushindwa kurejesha  mikopo kutoka Benki ya Ushirika Kilimanjaro (KCBL). KCBL imekuwa ikivikopesha vyama hivyo kupitia mfumo wa stakabadhi za mazao ghalani.

Akizungumza na JAMHURI, Meneja wa muungano wa vyama 32 vya ushirika maarufu kama  G32, Gabriel Ulomi, amesema hatua hiyo inaweza pia kukidhoofisha kiwanda hicho.

Kahawa inaponunuliwa kwa wakati mnadani inarahisisha kurejesha mkopo kutoka KCBL, tofauti na hivyo urejeshaji huo unakuwa mgumu na kuwapo ongezeko la riba,” amesema.

Ulomi amedai kuwapo sababu za kutonunuliwa kahawa hiyo, ikiwamo viwango duni vya magunia yanayotumika kuhifadhi kahawa kwenye kiwanda hicho kinachomilikiwa kwa asilimia 54 na Chama Kikuu cha Ushirika Kilimanjaro (KNCU).

Hata hivyo, amesema kigezo hicho hakina mashiko na kupendekeza jambo la msingi katika ununuzi huo kuwa sampuli ya kahawa husika.

Kaimu Meneja wa TCCCo, Japhet Ndosi, amethibitisha kuwapo malalamiko ya wakulima wanaotumia kiwanda hicho kuhusu kahawa yao kususiwa katika mnada huo.

Hilo jambo lipo na limeshafika mpaka kwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro (Anna Mghwira), sasa sina mamlaka ya kulielezea kwa kina zaidi ya hapo,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Kiwanda hicho, Aloyce Kittau, ameahidi mara kadhaa kulitolea ufafanuzi suala hilo, lakini hadi tunakwenda mitamboni, ahadi hiyo hajaitekeleza.

Kwa mara ya mwisho, Kittau aliliambia JAMHURI, “Kesho asubuhi (Desemba 13, mwaka huu) nitakuwa ofisini kwa  Mkuu wa Mkoa, nikitoka nitakutafuta tuliweke sawa hilo jambo, kwa kweli hata sisi linatuumiza sana.”

Pamoja na ahadi hiyo, mwenyekiti huyo kila alipopigiwa simu hakuweza kupokea na alipotumiwa ujumbe mfupi kupitia simu yake ya kiganjani hakujibu.

Chanzo cha taarifa kimelieleza JAMHURI kuwa kahawa inayokobolewa TCCCo ilianza kususiwa katika mnada huo kuanzia Oktoba 12, mwaka huu. Hali hiyo ikajitokeza tena kwenye mnadala uliofanyika Oktoba 19, 26 na Novemba 2, mwaka huu.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa kahawa iliyosusiwa katika mnada wa pili, ilinunuliwa kwenye mnada uliofanyika Novemba 9, mwaka huu.

 KCBL WAFUNGUKA

 Meneja Mkuu wa KCBL, Joseph Kingazi, amesema kutonunuliwa kwa kahawa hiyo kutasababisha wakulima kutolipwa malipo ya pili ya kahawa wakati chama cha msingi cha ushirika kitavuka na deni na hivyo kukosa sifa ya kukopeshwa msimu unaofuata.

 “Hatua hii itawavunja moyo wakulima na kuwafanya wakauze kahawa yao kwa wanunuzi binafsi,” amesema.

Kingazi amesema vyama vya msingi vya ushirika havina budi kuitumia KNCU yenye uwezo wa kusimamia soko la kahawa, ili waweze kufikia azma ya kuuza zao hilo kwa faida kubwa bila ukiritimba.

Kwa mujibu wa Kingazi, mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani unataka wakulima kufanya makisio ya ukusanyaji wa kahawa kabla ya Mrajis kuthibitisha makisio hayo.

Ofisi ya Mrajis wa vyama vya ushirika hudhibitisha makisio ya ukusanyaji wa kahawa na kuweka ukomo wa madeni, na mara baada ya Mrajis kuthibitisha, benki hiyo inatoa mkopo kulingana na makisio ya kahawa watayonunua,” amesema.

Amesema msimamo wa KCBL ni kuona kahawa inauzwa kwa  muda mwafaka mnadani na kwa bei nzuri, ili kuviwezesha vyama hivyo kurejesha mkopo kwa wakati hivyo kuwa katika mazingira mazuri ya kuvuka msimu bila malimbikizo ya madeni.