Moyo ni kiungo kimojawapo cha mwili wa binadamu. Vipo viungo vingi mwilini vikiwamo figo, ini, pafu na vinginevyo. Moyo wa binadamu daima hufikwa na madhila ya raha na tabu katika muda wote wa uhai.
Shida, simanzi, raha na misukosuko ni mambo yanayopita ndani ya moyo wa binadamu. Moyo wa binadamu hupata mitihani aina mbalimbali, kadhalika hupata majawabu mbalimbali, matamu na machungu. Hakika moyo huwa mzito au mwepesi kulingana na matukio ya mkasa.
Katika mazingira kama haya, nafsi ya binadamu imeweza kusanifu maneno mazuri au mabaya katika nyimbo, mashairi, tenzi, ngonjera na taarifa mbalimbali, kusifu au kukashifu: kukemea au kunasihi na hata kudiriki kukatisha tamaa au kuua moyo wa binadamu.
Moyo unapokata tamaa mafanikio ya kufanya kazi hayapo, na unapokufa uhai wa binadamu hutoweka duniani. Na hapo roho mbinguni na duniani hupata majuto. Moyo wa nani usiopata adha kama hizi?
Ukweli upo ugomvi baina ya ‘Hiari na Dhima’ ndani ya moyo wa binadamu. Binadamu anapotamani kutenda mema au maovu dhidi ya binadamu mwenzake, hiari na dhima hutokeza kila moja ikitamani nafasi hiyo. Ugomvi baina yao hulipuka na kuutia moyo katika fukuto la kutenda jambo hilo.
Hiari ni kukubali bila kulazimishwa. Ni radhia, ni ridhaa. Hiari ina nguvu ya kushawishi moyo kutenda jambo lolote hata kama jambo hilo litazaa mwana kidonda na mjukuu kovu. Je, moyo wako haujakushawishi kutenda jema au baya kwa masilahi yako?
Dhima ni wajibu mkubwa pamoja na uwezo wa kufanya jambo: ni madaraka ni wadhifa. Dhima hushawishi moyo kufanya jambo lolote kwa kujiamini hata kama jambo hilo litazaa mtoto hasira na mjukuu majuto. Je, moyo wako haujapata uwezo wa kutimiza wajibu kwa manufaa yako?
Kumbuka, ‘busara kubwa kichwani haina faida kama moyoni hauna chembe ya wema’ (Shaaban Robert). Moyo unapotawaliwa na chembechembe za wema, ugomvi baina ya hiari na dhima haupatikani na hapo ndipo unapopata ukamilifu wa mtu duniani ni tabia njema.
Nazungumza haya kutokana na kero zinazofanywa na baadhi ya watu kuruhusu nyoyo zao kutoa nafasi ya ugomvi baina ya hiari na dhima, na kufinyanga familia, makundi na jamii kuwa katika shaka. Je, haujaona watu wakichochea mioyo kuwa na shaka?
Ni vema Kutambua moyo hubeba lawama unaposhindwa kuzuia ugomvi baina ya hiari na dhima. Ndugu hugombana na mwishoni huelewana. Lakini tayari wamekwisha kuweka dosari katika udugu wao.
Si hayo tu, marafiki hunafikishana na mwisho hufarakana. Kadhalika wanandoa huzozana na kutukanana, hatimaye huchukiana na kuachana bila hata kuona aibu mbele ya jamii wala kuomba toba kwa Mwenyezi Mungu.
Tabu, shaka na wasiwasi hujaa nyoyoni mwa watu wanapokinzana na kulaumiana wakigombea madaraka, masilahi, utajiri na mapenzi. Matokeo ni watu kuteswa, kutekwa nyara, kupata makovu na vilema vya kudumu na pengine kuuawa.
Majawabu haya mabaya yanawezekana kufutwa katika orodha ya maovu pindi wanadamu tutakapokiri na kujaza chembe za wema nyoyoni mwetu. Kumbuka wema ni upendo, ni utu na ubaya ni ukatili na kisasi. Tia akilini.