Kundi la Hezbollah limetoa onyo kali kwa Waisraeli kuwataka wakae mbali na maeneo ya kijeshi kaskazini mwa Israel, hatua ambayo inalenga kuokoa maisha yao kutokana na mashambulizi yanayoendelea.
Onyo hilo limekuja baada ya kuongezeka kwa mashambulizi ya Hezbollah katika eneo hilo, ikijumuisha kurusha makombora kila siku.
Hezbollah inadai kwamba jeshi la Israel limeweka kambi zake za kijeshi ndani ya maeneo ya makazi kaskazini mwa nchi, maeneo ambayo sasa yanalengwa na makombora na ndege zisizo na rubani za Hezbollah.
Katika taarifa yake, Hezbollah ilisisitiza kuwa mashambulizi hayo yanawalenga moja kwa moja wanajeshi wa Israel, lakini raia wanaweza kuwa katika hatari kama wataendelea kuwa karibu na maeneo hayo ya kijeshi.
Katika wiki tatu zilizopita, mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya Hezbollah nchini Lebanon yanasadikika kuwa yamewaua makumi ya viongozi wa kundi hilo. Hata hivyo, Hezbollah imekuwa kimya kuhusu hasara iliyopata, lakini onyo hili linaonyesha kuwa kundi hilo bado lina uwezo wa kujibu mashambulizi kwa nguvu kubwa.
Hezbollah pia imeashiria kuwa mashambulizi yake yamekuwa machache, ikionya kuwa Israel haijashuhudia mashambulizi yote ambayo kundi hilo lina uwezo wa kufanya. Hadi sasa, bado haijulikani ni kiasi gani cha silaha za Hezbollah kimeharibiwa na mashambulizi ya hivi karibuni ya Israel.