Kundi la wanamgambo la Hezbollah la nchini Lebanon, limethibitisha kuwa kiongozi wake na mmoja wa waanzilishi wake, Hassan Nasrallah ameuawa katika shambulizi la anga la Israel siku ya Ijumaa.
“Sayyed Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu wa Hezbollah, ameungana na mashahidi wenzake na wafiadini ambao aliwaongoza kwa takribani miaka 30,” ilieleza taarifa iliyotolewa na kundi hilo linaloungwa mkono na Iran.
Taarifa hiyo ya Hezbollah imeapa kuendeleza “vita vyake vitakatifu” dhidi ya adui yake Israel, na katika kuiunga mkono Palestina.
Mapema jeshi la Israel lilisema Hassan Nasrallah aliuawa katika shambulizi ”sahihi” la anga wakati wa mkutano wa viongozi wa kundi hilo kwenye makao yake makuu huko Dahiyeh, kusini mwa Beirut.
”Hassan Nasrallah ameuawa,” alitangaza msemaji wa jeshi la Israel, Luteni Kanali Nadav Shoshani, katika ukurasa wa mtandao wa X.
Duru karibu na kundi la Hezbollah limeliambia shirika la habari la Ufaransa, AFP kuwa mawasiliano na Nasrallah yalipotea tangu siku ya Ijumaa, wakati shambulizi lilipofanyika.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa imesema kulingana na taarifa walizo nazo ambazo zimethibitishwa, ni kweli Hassan Nasrallah ameuawa.