Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza leo (Jumapili, Novemba 13, 2022) imetangaza kufunguliwa kwa dirisha la rufaa ili kutoa fursa kwa wanafunzi ambao hawakuridhika na viwango vya mikopo walivyopangiwa kuwasilisha taarifa za uthibitisho ili kuongezewa viwango vya mikopo kulingana na uhitaji wao.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru (pichani) amesema dirisha hilo la rufaa litakuwa wazi kwa siku saba (07) kuanzia leo, Novemba 13 hadi 20 mwaka huu na kuwa rufaa kutoka kwa wanafunzi zinapaswa kuwasilishwa kwa njia ya mtandao.
“Hadi leo (Novemba 13, 2022), tumeshawapangia mikopo wanafunzi wa mwaka wa kwanza wapatao 68,422 na tunafahamu kuwa kuna wanafunzi ambao kwa sababu mbalimbali, hawakukamilisha nyaraka muhimu kuthibitisha uhitaji wao, dirisha la rufaa ni fursa kwao,” amesema Badru.
Kwa mujibu wa Badru, lengo ni kutoa mikopo kwa wanafunzi wapya 71,000 katika mwaka wa masomo 2022/2023 na kuwasihi wanafunzi wanaowasilisha rufaa kusoma na kuzingatia maelekezo yaliyopo kwenye mfumo wa kuwasilisha rufaa.
Kuhusu malipo, Badru amesema HESLB fedha zilianza kutumwa vyuoni hata kabla ya wanafunzi kufika vyuoni na kuwa kazi hiyo ni endelevu na kuwashauri wanafunzi waliopangiwa mikopo kufika kwa maafisa mikopo wa vyuo vyao ili kukamilisha taratibu za kupokea fedha.
“Pale mwanafunzi anapoona amepangiwa mkopo kupitia yake ya SIPA (Student’s Individual Permanent Account), basi afike kwa afisa mikopo wa chuo chake ambaye yupo palepale chuoni ili awasilishe taarifa zake za benki na kupokea fedha,” amesema Badru.
Wakati huohuo, Badru amezishukuru taasisi za elimu ya juu na serikali za wanafunzi kwa ushirikiano wanaoipatia HESLB ambao umeendelea kuimarisha ufanisi katika kuwahudumia wanafunzi wanaonufaika na mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na Serikali kupitia HESLB.
“Kwenye huu mnyororo wa kuwahudumia wanafunzi, uongozi wa vyuo, serikali za wanafunzi na jumuiya yao ya TAHLISO ni wadau muhimu … na wamekuwa wakitupatia ushirikiano mkubwa, tunawashukuru sana,” amesema Badru.
HESLB ilianzishwa mwaka 2005 ikiwa na majukumu makuu mawili, kutoa mikopo kwa wanafunzi wahitaji wa elimu ya juu na kukusanya mikopo iliyoiva ambayo imetolewa na serikali kutoka mwaka 1994/1995.