Wapo Watanzania wengi ambao tumeiga desturi ya mwanzoni mwa mwaka ya kupongezana na kuombeana mema katika mwaka unaoanza.
Ni jambo jema bila shaka, lakini nimegundua pia ni desturi inayoweza kuzua kero na ugomvi baina ya watu.
Nimekuwa na utaratibu wa muda mrefu wa kutunza kumbukumbu ya kila mtu ninayewasiliana naye kwa simu au kwa njia ya ujumbe wa maandishi na inapofika tarehe 1 Januari natuma salamu za heri ya mwaka mpya kwa wote ambao wamo kwenye kumbukumbu nilizotunza.
Mwaka huu nimepigwa butwaa na majibu ya baadhi ya watu niliowapelekea salamu. Kwanza, kwa sababu baadhi yao tumewasiliana mara chache sana na hawakutunza kumbukumbu ya namba yangu kwenye simu zao, wengi hutaka kufahamu mimi ni nani.
Najitahidi kuwajibu wote na kurudia maelezo kuwa nimewahi kuwasiliana nao na nimetunza namba zao kwenye simu yangu. Lakini idadi ya ninaowajibu ni kubwa na sifanikiwi kuwajibu wote kwa sababu natuma ujumbe kwa watu zaidi ya 1,500. Kwa ninaowajibu, wapo wanaonifahamu, lakini wapo wengine wengi ambao wananifahamisha kuwa hawanifahamu.
Baadhi yao, kwa lugha ambayo haifanani kabisa na nia yangu njema ya kusambaza salamu za heri, huniambia kinagaubaga kuwa hawataki kupokea salamu zangu na nifute kabisa kumbukumbu ya namba zao kwenye simu yangu.
Mmoja aliniambia kuwa yeye anawaza namna ya kutafuta pesa ya kula halafu mimi najaribu kumwambia kuwa kuna mambo mema kwenye Mwaka Mpya. Aliniambia anaona kama namtumia salamu za kishetani.
Majibizano yote haya, ambayo yalikuwa, ama kwa njia ya mazungumzo ya simu, au kwa ujumbe mfupi wa maandishi, yaliniacha hoi nikijiuliza inakuwaje vigumu kusema tu ‘asante’ hata kama hufahamu ni nani anayekutumia hizo salamu.
Lakini inawezekana mimi pia nilichochea mkanganyiko. Ujumbe wangu, ‘Heri ya Mwaka Mpya’, uliandikwa kwa Kiswahili, Kiingereza, Kitaliani (lugha tatu ambazo ninazimudu kwa kiasi fulani) halafu nikatumia mtandao kutafiti lugha nyingine saba ambazo sizifahamu na kuziongeza kwenye mlolongo wa ujumbe wangu. Hizo lugha nyingine zote saba hazikuwa za Kiafrika.
Walioelewa msingi wa salamu zangu walianza kunijibu kwa Kihaya, Kinyiramba, na kwa lugha nyingine wanazozifahamu. Wale ambao hawakuelewa nia yangu waliniuliza maana ya ujumbe wangu na ni wengi kati ya hao ambao hawakutaka kabisa niwatumie tena salamu zozote.
Nilipata hisia kuwa upo mgongano wa kiutamaduni. Nilimuuliza Mzanaki mwenzangu anayemudu Kizanaki kunielimisha namna ya kusema ‘Heri ya Mwaka Mpya’ kwa Kizanaki. Hakuwa na jibu. Ilikuwa ni kama nimemuuliza swali la mtihani ambalo mwalimu hakuwahi kufundisha darasani.
Alikiri kuwa hafahamu neno la Kizanaki lenye maana sawa na ‘heri’. Sikushangaa. Ingawa yawezekana lipo neno linaloshabihiana na ‘heri’ nina hakika kuwa desturi ya kutakiana mema pindi unapoanza mwaka haimo ndani ya mila na desturi za Kizanaki.
Kama ipo ndani ya mila na desturi za makabila mengine itakuwa ni desturi ambayo tumeiga kutoka kwa wakoloni na jamii nyingine, au kutokana na dini tulizopokea. Kwa jamii za Magharibi historia inaeleza kuwa ni mfalme mkuu wa Kirumi, Juliasi Kaizari aliyeboresha mfumo wa kalenda wakati wa utawala wake na kuanzisha utaratibu wa kuhesabu mwanzo wa mwaka kuanzia tarehe 1 Januari.
Mwaka 1570 Papa Gregori wa XXIII alifanyia marekebisho kalenda iliyoanzishwa na Kaizari na kuanzisha mfumo ambao unaofahamika kama Kalenda ya Gregori na ambao unatumika hadi sasa katika sehemu nyingi. Dini ya Kiislamu nayo ina mfumo wa kalenda ambao nao pia huadhimisha mwaka mpya.
Miongoni mwa vielelezo vya tofauti kubwa ya mifumo hiyo miwili ya kalenda na jinsi gani jamii zetu ziliweka kumbukumbu za tarehe muhimu za matukio ni kukosekana kwa kumbukumbu za vizazi na vifo, hasa kwa wazee wetu. Bibi yangu mzaa baba alipofariki dunia mwaka 1997 ilikadiriwa alifariki akiwa na umri wa miaka 105, bila kuwapo kumbukumbu sahihi ya siku mahsusi ya kuzaliwa kwake.
Enzi zake nina hakika masuala muhimu yalikuwa siku, na misimu. Salamu muhimu, mpaka leo, ni umelalaje? Isingewezekana enzi hizo mtu kuulizwa ana mipango gani ya mwaka mpya.
Baadhi ya waliozaliwa walipewa majina yaliyoambatana na msimu, au tukio muhimu wakati wanazaliwa. Katika hali ya maisha ya kila siku ni misimu ya kilimo ambayo ingebeba umuhimu mkubwa zaidi kuliko tarehe mahsusi ya kuanza au kumaliza mwaka.
Kama leo hii kuna watu wananikasirikia kwa kuwatumia salamu za Mwaka Mpya siyo jambo la kushangaza kwa sababu ni mapokeo ambayo yanapaswa kueleweka na kukubalika kwa pande zote mbili.
Pamoja na desturi hii kunigombanisha na baadhi ya watu siiachi, ila nachukua tahadhari kuhakikisha kuwa nikipata tena fursa mwakani nitaongezea lugha zetu za asili kwenye mlolongo wa salamu.
Lakini naanza mwaka na somo muhimu kuwa nia njema ina uwezo wa kujenga uhusiano pamoja na uwezo wa kuubomoa. Labda nitatanguliza salamu zangu zijazo na ombi: “Samahani, naomba idhini yako kukutumia salamu za ‘heri ya mwaka mpya.’
Kwa wasomaji wa makala hii, kunradhi, lakini heri ya Mwaka Mpya.