Juma lililopita katika safu hii, nilizungumzia maneno mawili haki na batili. Haki inavyoelekeza jamii ya watu katika kweli, na batili inavyopotosha jamii hiyo katika dhuluma. Mgongano huo kifalsafa ubajenga hali ya ‘figisufigisu’ ndani ya jamii ya Watanzania.
Leo naelekeza fikira tena kuangalia jamii hii inavyosumbuliwa na kigonjwa kidogo kinachowafanya wakati fulani wasielewane na kufanya dunia kuwashangaa, kutokana na uhalisia wao.
Watanzania ni watu huru na timamu katika kuendesha maisha yao. Wamejaa hekima na busara katika mazungumzo yao, uweledi na ushupavu katika shughuli zao za kila siku. Dunia inawaelewa hivyo hata kuwapa sifa, Tanzania ni kisiwa cha amani.
Kabla ya kutaja kigonjwa kinachowasumbua Watanzania hawa, ni hekima kurejea msemo wa Kiswahili usemao, ‘Heri ya mchawi kuliko mwongo.’
Mchawi ni mtu anayesadikiwa kuwa anaweza kuwadhuru watu kwa kuwaroga; mlozi, kaini. Mwongo ni mtu mwenye tabia ya kutosema kweli; mdanganyifu, mzushi, kidhabu, ayari, laghai (kutoka Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Toleo la 3).
Heri ya mchawi. Mchawi hudhuru au kuroga mtu kwa wakati mmoja, kama bunduki inavyotoa risasi na kudhuru tu. Kuliko mwongo. Mwongo hudanganya watu kwa wakati mmoja, kama kalamu inavyoelimisha watu kwa wakati mmoja.
Mwongo hutumia akili na ulimi wake kulaghai watu – ama kwa kutosema kweli au kuzusha jambo litakaloleta mfarakano na kuvunja utulivu na pengine kutia watu katika mapigano, vita au mauti. Mambo kama hayo tumesikia na kushuhudia katika familia zetu na katika mataifa mbalimbali duniani.
Mwongo ni hasidi na ana maneno matamu ya kuvutia watu wa rika yoyote. Huchonganisha watu na kuwatawanya. Daima hujifanya mwema, mtetezi na mkarimu. Hujifanya rafiki na kukutendea mema pasi na wewe kutambua kuwa ana yake dhamira ya kukutenganisha na watu wako wa moyoni kumwambia.
Katu mwongo hatoki katika mazingira ya watu, kama alivyo kupe na mkia wa ng’ombe, mpaka pale atapotimiza azma yake ya kuwazushia mambo na kuwagawanyisha. Mchawi hayupo hivyo. Yeye atadhuru mtu kwa kuroga. Kamwe hatawagawa watu kama unavyogawa karanga na peremende kwa watoto.
Baada ya kueleza hayo, narejea maelezo yangu ya awali kuwa Watanzania nawaona kama wanasumbuliwa na kigonjwa kidogo kinachowafanya wakati fulani wasielewane. Kigonjwa hicho ni uwongo; kusema uwongo. Baadhi yetu hawasemi kweli katika kujenga na kuendesha nchi hii.
Hiki ni kigonjwa kibaya. Kinavyouguzwa na kulelewa kitaleta hatari katika umoja wa Watanzania. Katika siku hizi chache kupitia vyombo vya mawasiliano, tumesikia migongano ya kauli za viongozi wetu zikikinzana juu ya Taifa letu limo katika hali ya uhaba wa chakula na njaa katika sehemu mbalimbai.
Viongozi wa Serikali wanasema hakuna njaa ila kuna upungufu wa chakula katika maeneo fulani fulani. Viongozi wa siasa wanasema nchi imo katika njaa. Kila upande unatoa maelezo ya kukidhi haja. Watanzania tumebaki kuduwaa nani kati yao wanasema kweli. Jibu la muda tusubiri ripoti ya utafiti kuhusu chakula nchini.
Ukweli kauli mbili hizi zinasigana. Kimantiki kauli moja itakuwa ya kweli na nyingine ya uwongo. Kama hivyo ndivyo, kwa nini? Viongozi mnafanya hivyo kwa maslahi ya kwenu au ya kwetu sote? Tukumbuke tuko kama wajenji tunajenga nyumba moja. Vipi tugombee fito? Tunauma?
Kiongozi unaposema uwongo, wafuasi wako tukueleweje? Una nia ya kutujenga au una dhamira ya kutubomoa? Hivi isingekuwa busara kwanza viongozi wa pande mbili hizo kuwa meza moja na kutoa jawabu moja badala ya majawabu mawili yenye hasi na chanya.
Naamini wakati umefika sasa viongozi wetu kuacha kulea kigonjwa hiki kidogo ambacho huko mbele kinaweza kuleta madhara. Uongozi ni kuonesha njia, kuwa na busara, upendo na uvumivu katika kila jambo. Si kuzusha wala kutaka sifa. Sifa ina faida na hasara.
Raha iliyoje viongozi wetu mnapokuja mbele yetu wananchi muwe mmejiandaa kutuletea ukweli si hisia wala ulaghai. Tukumbuke amani na utulivu havijengwi na uwongo bali hujengwa na kweli.