Baada ya kuelezwa kujiengua ndani ya kikosi cha Singida United ikielezwa hajalipwa baadhi ya stahiki zake, Kocha Hemed Morocco, amesema hakuna kilichoharibika.
Morocco amekuja na kauli ya kitofauti akisema hakuna tatizo lolote lililotokea baina yake na mabosi wa Singida, huku akisema atarejea muda wowote kuendelea na kibarua chake.
Kocha huyo ambaye kwa sasa yupo Zanzibar, ameeleza kuna mabo kadhaa hayakuwa sawa hivyo wapo kwenye mchakato wa kuyamaliza huku akisema si makubwa kwa kiasi cha kwamba yanaweza leta tatizo kubwa.
Awali ilielezwa kuwa Morocco hakulipwa baadhi ya stahiki ambazo walikubaliana na Singida United kitu ambacho kilipelekea akaondoka kuelekea kwao Zanzibar, lakini inaonekana kuna mazungumzo ya chini kwa chini baina ya pande mbili.
Juzi Singida kupitia kwa Mkurugenzi wa timu, Festo Sanga, alisema kuwa Morocco ameelekea Zanzibar kwa masuala ya kifamilia na akiahidi atarejea mufda wowote kuendelea na kazi.