Maelfu ya Watanzania, ndani na nje ya nchi wameendelea kuomboleza kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (43), aliyefariki dunia pamoja na watu wengine wanne katika ajali ya helikopta iliyotokea wiki iliyopita.
Pamoja na Filikunjombe, wengine waliofariki dunia ni rubani wa helikopta hiyo, William Silaa, Plasdus Haule, na Egid Nkwera.
Chanzo cha ajali hiyo bado hakijatolewa na mamlaka zinazohusika na masuala ya usafiri wa anga, lakini mashuhuda wa ajali hiyo walisema waliona helikopta ikiripuka kabla ya kuanguka katika Pori la Selous. Filikunjombe alizikwa mwishoni mwa wiki nyumbani kwao Ludewa, katika shughuli iliyohudhuriwa na maelfu ya wananchi kutoka pande mbalimbali nchini.
Wengi wamlilia Filikunjombe
Watu mbalimbali wameshindwa kujizuia kuonyesha hisia zao kutokana na kifo cha mbunge huyo kijana aliyependwa na wanasiasa wa pande zote-CCM na vyama vya upinzani.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kwenye ukurasa wake wa facebook amesema: “Wanadamu, maisha yetu ni mafupi na yanapita kama moshi! Tuna kila sababu ya kujiuliza ni kwanini Mwenyezi Mungu ametuleta duniani na kutupa uzima! Kwa namna kubwa tunapaswa kujiuliza tutaacha jina na sifa gani baada ya maisha ya dunia na pia tumejiandaa vipi kwa maisha ya milele mbinguni!
“Filikunjombe ameishi maisha yake, na atabaki akiishi kwa muda mrefu sana wa siku za mbele kwa wana Ludewa! Ni jambo la kusitikitisha sana kila tunapofiwa na mmoja wetu, lakini huwa naumia sana kijana anapofariki bila kujali nafasi yake, lakini inaumiza sana pale ambapo kijana aliyefariki ni mzalendo na mwenye mafanikio mapana!
“Ameniliza sana DEO Filikunjombe, nilikuwa kwenye mafunzo nje ya nchi, na watu walishangaa kwanini natokwa machozi, na bado namlilia! Ni pigo kubwa sana kwangu kila tunapopoteza vijana hususani wale wenye nafasi ya kuitumikia nchi hii kwa masilahi mapana!
Maisha yetu ni mapana kuliko mipango yetu kama wanadamu, na kama wanadamu hatujaweza kutumia hata 10% ya vipawa na karama tulizopewa na Mungu, na waliofanikiwa sana haiyumkini wametumia si zaidi ya 20%! Maisha yetu ni zaidi ya maisha ya siasa, ni zaidi ya mhemuko wa siasa, ni familia, maisha ya kiroho, ni uchumi binafsi na pia mchango wako katika Taifa kama ambavyo DEO alivyotoa mchango wake kwa nchi yake kupitia uwakilishi wa Ludewa!
“Kweli kama nchi tumepigwa na vijana bila kujali vyama tumempoteza mmoja wetu na Mungu amlaze mahali pema peponi!
“Ningependa kama vijana tukawa na mtizamo mpana zaidi ya vyama na pilika za uchaguzi! Inaumiza kuona watu wanachukulia kifo kama kitu kidogo na hususani pale tunapokuwa tumempoteza kiongozi kijana mwenzetu! Hili halipaswi kuwa suala la mzaha na bado ukaendelea kujiita ni kiongozi!
“Vyama vya siasa ni kama mabasi na lengo letu ni kufika tuendako, na mbona sijaona abiria wakigombana kwa kuwa tu wapo mabasi tofauti! Kadi za vyama ni kama tiketi za mabasi, sera na uongozi ni kama huduma zilizomo kwenye basi pamoja na dereva wake!
“Dereva akikusumbua unapanda basi jingine, na kamwe hakuna uadui na abiria waliopo kwenye basi uliloliacha na wala konda wake!
“Mwisho, tunapaswa kuyatafakari kwa kina maisha yetu na sababu ya kuishi kwetu! Kwanini Mwenyezi Mungu amekupa siku za ziada kuliko DEO? Ni nini umejipanga kufanya katika maisha yako cha kukumbukwa kwako kwa ajili ya familia yako, jamii yako na Taifa lako!
“Umejiandalia maisha gani huko uendako ambako hakuna anayerudi! Kwanini tumekuwa na jitihada zinazoishia tarehe 25/10 kwenye vikatio? Kwanini tunatumia nguvu nyingi kutengeneza uadui, tunajifunza nini kila siku tunayopewa na Mungu? Celina, Mtikila, Kigoda, Makaidi na sasa Jembe DEO wameondoka, hivi maisha yetu yanaenda wapi? Vita za nini? Kebehi za nini? Tukibomoa nani atasimamisha ubomoaji na nani atajenga? Wewe utakuwa wapi?
“Napenda na kufurahia pale ninapoona watu wanatofautiana itikadi, lakini najisikia mnyonge pale ninapoona watu wanadhihakiana, wanaanza kuwa maadui! Kama waliotutangulia wangefanya hivi, basi nchi hii tusingeikuta hapa! Wapigakura wapo nje ya mitandao hii, hapa hakuna atakayebadilika kwa sababu ya Whatsup message, kwanini basi dhihaka?
“Kesho tutaweka wapi sura zetu baada ya uchaguzi?! Tunajifunza nini katika maisha mafupi ya DEO na wengine tunaowapenda, lakini waliotutangulia?
Muda uliobaki tuutumie kujenga uhusiano bila kuachana na itikadi za kila mmoja! Tunahitaji Tanzania yenye Umoja na Imara!
Mungu warehemu marehemu wote na tupe busara ya kutambua umuhimu na thamani ya nchi yenye Amani! Mwenyezi Mungu endelea kuibariki Tanzania na watu wake! AMINA! NKM.”
Ajali za helikopta
Jumamosi ya Novemba 29, 2014 marubani wanne (watatu wa Polisi na mmoja wa Wanyamapori) walipoteza maisha katika ajali ya helikopta ambayo bilionea mmoja wa Marekani alimpatia Waziri wa Maliasili na Utalii, licha ya kupigiwa kelele kwamba ilikuwa haifai kutumiwa.
Mara baada ya ajali, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alitamka kuwa: “Ingawa timu itaundwa kuchunguza, chanzo cha ajali hiyo kilikuwa ni ubovu wa helikopta yenyewe”.
Lakini tangu mwanzo – mara tu ilipowasili helikopta hiyo Aprili, mwaka huu – baadhi ya waliojua ufisadi na uongo kuhusiana na ujio wake (helikopta iliyojulikana kama helikopta ya Nyalandu) walitahadharisha kupitia baadhi ya magazeti, hasa JAMHURI kuwa helikopta ile lilikuwa ni janga, au bomu ambalo lingekuja kulipuka kwani ilikuwa ni chakavu kupita kiasi. Kitaalam tunaweza kusema ‘it was not air worth’.
Kwa nyakati tofauti, Kapteni Joseph Alphayo, mmoja wa marubani waliofariki, alilalamikia mchakato mzima wa uletwaji wa helikopta hii nchini kutoka Nairobi, Kenya.
Hazikupita siku nyingi, helikopta hiyo ilianguka eneo la Kipunguni, Dar es Salaam na kuwaua marubani watatu na ofisa wa Jeshi la Polisi.
Marubani hao ni Kapteni Alphayo wa Wizara ya Maliasili na Utalii, PC Josso Selestine, Mrakibu wa Polisi Kapteni Kidai Senzala na Mkaguzi wa Polisi Kapteni Simba Mussa.
Waziri wa Maliasili na Utalii anayemaliza muda wake kwa sababu anazozijua yeye, alileta “chuma chakavu” kwa jina la helikopta mpya; helikopta ambayo tangu siku ya kwanza wataalamu walieleza kuwa ilikuwa imepakwa rangi ili ionekane mpya!
Ninaomba kutahadharisha tena kuwa kuna vyuma chakavu viwili vililetwa na kupokewa na Nyalandu mapema mwaka huu. Pamoja na hiyo helikopta ambayo imegharimu maisha ya Watanzania wenzetu wanne, kuna ndege pale Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA). Viongozi wetu wakiendelea kuweka nta masikioni mwao na kupuuza tahadhari zinazotolewa juu ya ufisadi na hadaa za viongozi wanaopenda sifa, ndege hiyo nayo itaondoka na roho za Watanzania wengine.
JAMHURI tuliandika kuwa helikopta hiyo ni chakavu ilinunuliwa Kenya, lakini ikaonekana tumesema uongo au tuna nongwa na Waziri Nyalandu. Tukaweka uthibitisho wa invoice iliyotumika kununua mtumba huo. Lakini lazima pia tujiulize ilikuwaje helikopta hiyo chakavu ikabidhiwe kwa Nyalandu na sherehe hizo kuhudhuriwa na Balozi wa Marekani hapa nchini, Mark Childress?
Wasomaji wakumbuke, ni familia ya bilionea Buffet ambayo Nyalandu aliwahi kuitunukia Leseni ya Rais ya kuua wanyamapori 704. Mungu bariki, wanyama hao walipona baada ya Gazeti la JAMHURI kuandika na kutoa picha zilizowalazimu Wamarekani hao kuikimbia nchi.
Historia ya mtumba huo wa helikopta inaonyesha kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii iliupokea Juni 6, 2014. Aina yake ni Robison 44 Raven II.
Ilitolewa na Howard Buffett Foundation kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kusaidia mapambano dhidi ya ujangili. Helikopta hiyo ilikuwa imesajiliwa nchini Kenya kwa namba 5Y – HCB ikiwa ni ya Mamlaka ya Wanyamapori, yaani Kenya Wildlife Service (KWS).
Iliingizwa hapa nchini ikiwa na usajili wa namba za Kenya, lakini Agosti, jana ilirudishwa nchini Kenya baada ya Mamlaka ya Anga Tanzania (TCAA) kutoa maelekezo. Kilicholengwa kilikuwa kufuta usajili wa Kenya, kufanyiwa ukaguzi kwa lengo la kuwezeshwa kupata kibali cha kuruka katika anga ya Tanzania.
TCAA, kwa namna isiyoeleweka iliisajili na kupatiwa namba 5H-TWA na kupata leseni ya redio ya mawasiliano na kibali cha kuruka nchini.
JAMHURI tukabaini kuwa helikopta hiyo chakavu, ikiwa na namba 5H-TWA ilirejeshwa kutoka Kenya mnamo Novemba mwishoni na wiki moja baadaye ndipo ikaanguka jijini Dar es Salaam na kuua marubani na ofisa wa Polisi.
Ni mwaka mmoja sasa tangu kuanguka kwa helikopta hiyo, Serikali na vyombo vyake haijatoa sababu zilizosababisha ajali na vifo vya marubani na ofisa wa Polisi waliokuwamo.
Makamu wa Rais, Dk. Magufuli, wanusurika
Aprili, 2014 Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Ghalib Bilal, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Meck Sadick, na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleima Kova, walinusurika kifo katika ajali ya helikopta iliyotokea katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Viongozi hao walikuwa wakikagua madhara ya mafuriko. Helikopta hiyo ilikuwa mali ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Mkuu wa JWTZ, Jenerali Mwamunyange alisema ajali hiyo ilihusisha helikopta ya JWTZ yenye muundo wa Agusta Bell (AB 412) iliyotengenezwa Italia.
Alisema helikopta hiyo ilipangwa kuwazungusha viongozi hao katika maeneo yaliyoathiriwa na mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam na kusababisha maafa.
Alisema helikopta hiyo, ilipata ajali punde tu baada ya kuruka na kugonga ukuta.
“Ni kweli kwamba helikopta iliyopata ajali inamilikiwa na JWTZ…Hiyo ni ajali kama ajali nyingine yoyote. Imekuwa ni bahati mbaya wakati inaanza kuruka ikagonga ukuta wa jengo na kushuka chini….Mpaka sasa hatujajua sababu ya ajali hiyo,” alisema.
Aliahidi kwamba uchunguzi yakinifu kuhusu chanzo cha ajali hiyo utafanyika kwa kuhusisha wataalamu. Alisema helikopta hiyo ilikuwa ni miongoni mwa usafiri wa kutegemewa jeshini na ilifanyiwa majaribio Jumamosi na jana asubuhi na haikuonyesha tatizo lolote na kwamba imekuwa ikifanya kazi kwa muda mrefu bila matatizo yoyote.
Kamanda wa Polisi wa Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA), Selemani Hamisi alisema ndege hiyo imeungua kutokana na hitilafu, ingawa alisema yeye siyo msemaji kwa kuwa wapo viongozi wake wa juu.
“Nilikuwa wa kwanza kuruka wakati waokoaji wakiendelea kuokoa wengine waliokuwa ndani,’’ alisema Kova na kuongeza: “Tunawashukuru sana wale waliokuwapo nje ya helikopta hiyo kwani walisaidia tukashuka salama na kuendelea na majukumu yetu ya Taifa kama kawaida.’
Meneja wa JNIA, Moses Malaki alisema helikopta hiyo ilianguka baada ya kuruka kiasi cha mita 10 juu… “Ilibeba watu 11 wakiwamo waandishi wa habari na walinzi wa viongozi hao.”
Mchunguzi Mkuu wa Ajali za Ndege kutoka Wizara ya Uchukuzi, John Nyamwihura alisema asingeweza kutoa ufafanuzi kuhusu helikopta hiyo kwa sababu inamilikiwa na Jeshi.
Helikopta ya JWTZ yaanguka, yaua sita
Juni 2008, Helikopta iliyokuwa ikimilikiwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ilianguka na kuua abiria sita walikuwamo.
Ilikuwa ikitoka Arusha kwenda Dodoma. Aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Matei Basilio alithibitisha kutokea ajali hiyo.
Kamanda Basilio alisema kuwa ajali hiyo ilitokea saa sita mchana katika Kijiji cha Matevesi-Kisongo umbali wa kilometa 17 kutoka Arusha.
Waliofariki dunia ni rubani na fundi, mama na mtoto wa kike wa miaka 10 na maafisa wa JWTZ walikuwa wamepewa lifti kwenda Dodoma.
Nasari apata ajali
Julai 8, mwaka huu, Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nasari, alipata ajali wakati akiwa katika ziara ya kukagua shughuli za maendeleo jimboni mwake.
Watu walioshuhudia ajali hiyo walisema waliiona helikopta ikipoteza mwelekeo na kwenda kunasa kwenye mti kabla ya kuanguka chini. Hakuna aliyefariki dunia katika ajali hiyo.