Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam
WAZIRI wa Maliasili na Utalii Angellah Kairuki amesema kuwa takwimu za sasa zinaonesha kuwa takribani eneo la misitu lenye ukubwa wa hekta 469,000 kila mwaka linapotea nchini.
Amesema ni muhimu pia kwa wadau wote wa Misitu nchini kusoma kwa umakini Mkakati na Mpango Kazi wa Kitaifa wa Mianzi ili kupata picha ya tulipo sasa na kuhakikisha kuwa unatekelezwa ipasavyo ili kuendeleza misitu hapa nchini.
Waziri Kairuki ameyasema hayo leo Februari 19, 2024 wakati akizindua Mkakati wa Kitaifa wa Mianzi na Mpango kazi wake.
Amesema hali hiyo si nzuri na kama juhudi za pamoja hazitachukuliwa basi kasi ya kuenea kwa jangwa zitaathiri nchi na hatimaye kuchangia kwenye kuathiri dunia katika siku za usoni.
“Ili kukabiliana na hali hiyo, juhudi za kuendeleza miti ya mianzi ni jambo la muhimu, hivyo kila Mtanzania anapaswa kuhakikisha misitu inaendelezwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
“Ni matarajio yangu kuwa, iwapo Mpango Kazi huu utatekelezwa ipasavyo utawezesha kuendeleza uhifadhi na matumizi endelevu ya misitu ya zao la mianzi kwa maendeleo endelevu katika sekta nyingine,” amesema
Hata hivyo Kairuki amewaelekeza Chuo Cha Viwanda vya Misitu Moshi kwa kushirikiana na SIDO na wadau wengine washirikishwe kutafuta teknolojia za kisasa za kuchakata mazao ya mianzi ili kuyaongezea mnyororo wa thamani na kupata fedha nyingi kwa kuuza mazao hayo ndani na nje ya nchi.
“Hii ni fursa adhimu kwa sekta binafsi, kampuni, mashirika na wawekezaji kushiriki kikamilifu katika kuleta mapinduzi ya kilimo cha mianzi ili kuhakikisha Tanzania tunakuwa na malighafi ya kutosha ya kuweza kuendesha viwanda vya kuchakata mianzi na huku tukiuza hewa ya ukaa kwa ajili ya kuongeza pato la Taifa na mtu mmoja mmoja,” amesema.
Amewataka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kuhakikisha mbegu za mianzi hususani zile za kibiashara zinapatikana kwa urahisi ili wananchi na wadau wengine waweze kufikia malengo waliyojipangia.
“Ninaielekeza Taasisi ya Utafiti wa Misitu kufanya tafiti za kutambua maeneo sahihi ya kupanda aina mbalimbali za mianzi pamoja na kuiagiza Idara ya Misitu na Nyuki ifanye tafsiri ya nyaraka hizi mbili kwa lugha ya Kiswahili na kuzisambaza. Serikali itaweka mazingira wezeshi kwa wadau wote wa zao la mianzi ili kuhakikisha linaleta tija kwa Watanzania na Taifa kwa ujumla,” amesema Kairuki.
Naye Katibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk. Hassan Abbasi amesema mikakati mingi imeandaliwa cha muhimu ni utekelezaji hivyo watahakikisha wanasimamia ili yale mafanikio ya kiuchumi yaweze kupatikana.