Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia
Katika kuhakikisha dawa za kulevya zinatokomea nchini Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama, imefanikiwa kuteketeza hekari 535 za mashamba ya mirungi katika operesheni maalum ya ‘‘Tokomeza Mirungi’’ iliyofanyika katika vijiji vya Rikweni, Heikondi, Tae na Mahande vilivyopo katika kata ya Tae, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro.
Operesheni hii iliyolenga kukabiliana na kilimo cha mirungi imefanyika kwa siku saba mfululizo kuanzia tarehe 2 hadi 9 Julai, 2023 na jumla ya watuhumiwa tisa (09) wamekamatwa kuhusiana na uzalishaji, usafirishaji na biashara ya mirungi na watafikishwa mahakamani baada ya taratibu za kisheria kukamilika.
Operesehni hiyo imefanyika ikiwa ni siku chache baada ya Maadhimisho ya kupiga vita dawa za kulevya kufanyika Arusha ambapo mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliagiza jitihada zaidi ziongezwe katika vita dhidi ya dawa za kulevya nchini ili kuokoa jamii katika janga la dawa za kulevya.
Kamishna Jenerali DCEA, Aretas Lyimo amesema operesheni hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais Katika kukomesha kilimo cha dawa za kulevya hapa Nchini.
Mamlaka kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama itaendelea kufanya operesheni za mara kwa mara katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha kilimo cha Mirungi na bangi kinatokomea.
Operesheni hii ambayo umefanyika kwa muda wa siku nane ni endelevu na itaenda sambamba na utoaji wa elimu ili kujenga uelewa kwa jamii juu ya athari za mirungi na dawa nyingine za kulevya kwa wakazi wa vijiji hivi.
Pia elimu juu ya mazao mabadala pamoja na kuwawezesha kuzalisha mazao hayo. Hii itawafanya wananchi husika kuona fursa ya kulima mazao mengine na kuachana kabisa na kilimo cha mirungi,” amesema Jenerali Lyimo.
Aidha, amewakumbusha wananchi kuwa, kujihusisha kwa namna yoyote na uzalishaji, usafirishaji na uhifadhi wa dawa za kulevya ni kosa kisheria na adhabu yake inaweza kuwa kifungo cha miaka 30 jela au maisha endapo utakutwa na kosa hilo.
Pia sheria inaruhusu kutaifishwa kwa mashamba yaliyolimwa mirungi au bangi. Hivyo, tutahakikisha mashamba yote yatakayokutwa yamelimwa aina hizi za dawa za kulevya yanataifishwa.
Baadhi ya wananchi katika vijiji hivyo vinavyolima mirungi wameiomba Serikali kutoa elimu ya madhara ya dawa za kulevya hususani mirungi na kuahidi kuwa watafanya vikao kuhamasishana kuhusu hatari ya kilimo hicho na kwa pamoja washirikiane kuyafyeka na kuyaondoa kabisa mashamba yote ya mirungi katika maeneo yao.
Aidha, baadhi ya viongozi wa dini katika kata ya Tae wameeleza kuwa, wataendela kutoa elimu juu ya madhara ya mirungi kwa waumini wao. Elisante Senkondo mkazi wa kijiji cha Rikweni na mchungaji wa kanisa Assemblise of God amesema kuwa wako tayari kushirikiana na serikali kutoa elimu hiyo.
“Naiomba serikali itupe nafasi tukae na watu wetu katika nyumba zetu za ibada tuendelee kuwashauri kwa nguvu zaidi ili kwa hiari yao wenyewe waweze kukubali kutokomeza haya madawa ya kulevya” amesema Mchungaji Senkondo.
Naye kaimu mtendaji wa kata ya Tae Japhet Msengi ameeleza kuwa, wao kama viongozi wa kata wamefanya jitihada kadhaa kuhakikisha wananchi wao wanaondokana na kilimo cha mirungi, ambapo baadhi waliacha na wengine waliendelea kwa madai kuwa hakuna mazao mengine mbadala yatayowasaidia kujikimu kimaisha.
Hivyo,kufanyika kwa operesheni hii kutasaidia wadau wa kilimo kuona umuhimu wa kutoa utaalam katika kuzalisha mazao mengine ya kibiashara yanastawi katika maeneo haya.