Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), linakwenda kufanya uchaguzi wake, huku aliyekuwa Rais wa Shirikisho hilo, Jamal Malinzi, akiwa miongoni mwa wagombea ambao mpaka wikiendi walikuwa wamechukua fomu za kugombea tena nafasi ya uongozi.

Malinzi amekuwa Rais wa TFF, katika kipindi cha miaka minne iliyopita, baada ya kurithi mikoba ya mtangulizi wake, Leodegar Tenga, ambaye aliliongoza Shirikisho hilo katika vipindi viwili na kuleta hamasa kubwa miongoni mwa wadau wa mchezo wa soka.
Kamati ya Uchaguzi ya TFF, imetangaza kuanza kwa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho unaotarajiwa kufanyika Agosti 12, 2017 mjini Dodoma.
Mpaka kufikia sasa kuelekea uchaguzi huo tayari vigogo katika uongozi wa soka wamejitokeza kuomba ridhaa ya kuliongoza Shirikisho hilo, waliojitokeza ni pamoja na aliyewahi kuwa Rais wa Klabu ya Yanga, Imani Madega, pamoja na aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa kilichokuwa Chama cha Mpira Tanzania (FAT), kabla ya kubadilishwa kuwa Shirikisho, Michael Wambura, yeye akiwania nafasi ya Makamu wa Rais.

Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Jamal Malinzi, amefanya mengi, yakiwamo yaliyowafurahisha wadau wa soka na yapo yaliyowakarahisha. Yaliyowakarahisha yanaweza kutumika kama kigezo cha kutaka kuzuia azma yake ya kurudi TFF kama Rais.
JAMHURI, limeipitia ilani yake ya uchaguzi ya miaka minne iliyopita, na kufanya tathmini ya aliyoahidi pamoja na utekelezaji wake, aliahidi mpira kuchezwa tangu ngazi ya chini hadi juu, pamoja na ukuzaji wa soka la vijana ambalo lingekuja kuwa suluhisho kwa timu zote za Taifa.

Katika ahadi hiyo, amehakikisha mpira unachezwa katika ngazi zote, ikiwamo kuanzishwa kwa ligi ya wanawake, ligi ambayo imekuwa na msisimko mkubwa baina ya mashabiki wa soka nchini.
Ahadi nyingine ilikuwa ni kuifanya TFF, miongoni mwa taasisi zinazoheshimika ndani na nje ya nchi, katika hilo ameshindwa kufanikiwa, maana katika kipindi cha utawala wake, tulishuhudia punde tu baada ya kuingia madarakani ofisi za TFF, zilihama kutoka Uwanja wa Karume, na kupelekwa katika moja ya majengo ya kifahari katika Mtaa wa Ohio.
Ofisi hizo hazikudumu katika Mtaa wa Ohio, zilirudishwa Karume, huku miezi michache baadaye tukishuhudia msuguano baina ya Mamlaka ya Mapato Tanzania na TFF, kuhusu kodi, jambo ambalo lilisababisha TRA kuzuia hata akaunti za Shirikisho hilo kama mkakati wa kuhakikisha madeni yanalipwa.

Sehemu ambayo kwa hakika Malinzi amefanikiwa, ni kwenye eneo la ufundi, ambako idadi ya makocha wenye ngazi ya daraja la kwanza, wameongezeka kutoka wawili hadi 16, hiyo maana yake ni kwamba klabu zitafaidi matunda ya kupata walimu wenye sifa zinazokubalika ndani na nje ya nchi.

Eneo jingine ambalo ameonesha kufanikiwa ni kufufua mashindano ya Kombe la FA, mashindano ambayo katika utawala wake yamechezwa miaka miwili, huku klabu za Azam na Simba zikilitwaa kombe hilo kwa kupokezana.
Jambo jingine ambalo Malinzi mwenyewe amekuwa analitumia kama karata yake ni kuanzisha timu imara ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys, hilo ni jambo ambalo pengine limemletea yeye heshima hata kuteuliwa kuwa miongoni mwa wajumbe 11 katika kamati maalumu ya mageuzi ya muundo wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF).
Malinzi amekuwa na udhaifu katika kushughulikia tuhuma za rushwa ndani ya TFF, kuvuruga michakato ya uchaguzi, katika hilo la kuvuruga mchakato wa uchaguzi, lengo likiwa ni kuandaa safu yake kuanzia mikoani, JAMHURI linaona kuandaa safu katika uchaguzi siyo tatizo, lakini tatizo ni mbinu zilizotumika kuandaa safu hiyo.

Tuhuma za rushwa, ni eneo ambalo limeutia doa uongozi wa Malinzi, huku wadau wa soka wakishuhudia baadhi ya viongozi wa TFF wakipandishwa kizimbani kujibu tuhuma za rushwa zilizokuwa zinawakabili.
Miongoni mwa tuhuma za rushwa ni pamoja na zile za baadhi ya vigogo ndani ya TFF kuomba rushwa ya shilingi milioni 25 kwa viongozi wa Klabu ya Geita, ili ipate nafasi ya kupanda daraja na kucheza Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Hali hiyo ilisababisha hadi Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuingilia kati na kusababisha baadhi ya waliokuwa viongozi ndani ya TFF kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zilizokuwa zinawakabili.
JAMHURI litaendelea kuwachambua wagombea wote watakaojitokeza kuwania nafasi hiyo.